Majaliwa atoa tahadhari msimu mpya ununuzi wa korosho 2019
- Amewaagiza wakuu wa mikoa inayolima zao hilo wasiruhusu kuingizwa kwa mfumo mpya wa ununuzi ambao haujaeleweka kwa wadau na wanunuzi.
- Msimu wa korosho kwa mwaka huu unatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
- Watakaotumia kangomba kununua korosho, moto utawawakia.
Dar es Salaam. Wakati msimu wa korosho kwa mwaka 2019 ukitarajia kutangazwa hivi karibuni, Serikali amewaagiza wakuu wa mikoa inayolima zao hilo wasiruhusu kuingizwa kwa mfumo mpya wa ununuzi ambao haujaeleweka kwa wadau na wanunuzi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekuwa akizungumza jana (Oktoba 2, 2019) mkoani Mtwara amesema msimu wa korosho kwa mwaka huu unatarajiwa kutangazwa hivi karibuni, hivyo ni vema wakuu wa mikoa inayolima korosho wakajiandaa vizuri ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.
“Mabadiliko ya mifumo yalitolewa na baadhi ya viongozi ambao siyo waaminifu, Serikali iko macho itawachukulia hatua viongozi wa vyama vya ushirika wasiokuwa waaminifu. Tunataka mfumo wenye manufaa ndiyo utumike,” amesema Majaliwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali imewataka wafanyabiashara kutojihusisha na ununuzi wa korosho kwa njia ya zisizo halali ikiwemo kangomba.
”Kangomba imepigwa marufuku, watakaojihusisha moto utawawakia huko huko . Tunataka wakulima wenyewe ndio wanufaike,” amesema Majaliwa jana alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliyopo Mtwara.
Zinazohusiana:
- Namna tani zaidi ya 200,000 za korosho zitakavyonunuliwa na Serikali
- Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage joto la korosho likipanda
- Kwanini ufuatilie mjadala wa bei ya korosho?
Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wakulima wa korosho kuendelea kujiimarisha na wahakikishe wanajiwekea akiba kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kubangua korosho cha Yalin kilichopo katika eneo la Msijute mkoani Mtwara na kukagua kazi ya ubanguaji pamoja na kuzungumza na watumishi wa kiwanda hicho ambao waliishukuru Serikali kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda.