Majaliwa aongoza mamia mazishi ya Ndugai Dodoma
- Ahimiza kuyaenzi mema aliyoyatenda.
- Serikali yaahidi kutekeleza agizo la kujenga makumbusho Kongwa.
Arusha. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaongoza mamia ya Watanzania kuupumzisha mwili wa aliyekuwa Spika wa Bunge na Mbunge wa Kongwa Job Yustino Ndugai ikiwa ni siku tano tangu afariki dunia Agosti 6 mwaka huu.
Safari ya mwisho ya kiongozi huyo aliyelitumikia jimbo la Kongwa kwa miaka 25 imehitimishwa leo Agosti 11, 2025 saa sita mchana ikihudhuriwa na viongozi wa kitaifa wanafamilia na Watanzania kutoka maeneo mbalimbali.
Kabla ya mazishi, mwili wake ulifanyiwa ibada maalum kisha Watanzania wakapata nafasi ya kuuaga na baadae alipigiwa mizinga 21 kama ishara ya heshima ya utumishi wake ikifuatiwa na kuweka mashada ya maua katika kaburi lake.
Akizungumza baada ya shughuli za mazishi kukamilika Majaliwa amewataka Watanzania kumuenzi kwa kuendeleza mema yote aliyowahi kuyafanya pamoja na shughuli za maendeleo alizozianzisha katika jimbo la Kongwa.
“Hatuna budi kuyaenzi mazuri aliyoyatenda wakati wa uhai wake, wakati wa utumishi wake ikiwa ni njia ya kumuombea kwenye nyumba yake ya milele lakini pia tunalo jukumu kubwa la kumuombea hayati, kaka yetu kiongozi wetu mheshimiwa Job Ndugai huko alipo aweze kuala mahali pema,”amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka shada la maua katika kaburi la Hayati Job Ndugai Kongwa, Dodoma leo Agosti 11, 2025.Picha|OWM.
Pamoja na hayo, Majaliwa amesema kuwa Serikali italisimamia agizo la ujenzi wa makumbusho ya kupigania uhuru wa nchi za Afrika Kusini kama ilivyoagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan jana Agosti 10, 2025.
Rais Samia alisema kujengwa makumbusho hayo kutasaidia kueelezea mchango wa Wilaya ya Kongwa katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, ikiwa ni sehemu ya kuenzi ndoto za Spika mstaafu, hayati Job Ndugai.
“Maono ambayo ni vema yakafanyiwe kazi ili mchango w Kongwa kwenye ukombozi wa Kusini mwa Afrika utambu vizuri zaidi. Kwa wale wenye sekta zinazohusika katika kumuenzi ndugu yetu huyu, hilo naomba lifanyiwe kazi,” alsema Rais Samia akishiriki ibada ya mazishi ya Ndugai jana Agosti 10, 2025.
Pamoja na hayo Majaliwa amewashukuru Watanzania wote waliojitokeza kushirikiana na familia hiyo kuandaa utaratibu wa mazishi pamoja na kutoa pole kwa mke wa marehemu, watoto pamoja na wajukuu.
Latest