Mahakama Tanzania yazidi kujiimarisha kidijitali utoaji wa huduma

January 24, 2022 11:13 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba  Johari Simizi (kushoto) akionyeshwa namna mahakama zinavyotumia mitandao katika kuendesha kesi wakati alipotembelea banda la mahakama katika wiki ya sheria jijini Mwanza. Picha|Mariam John.


  • Yaanza mikakati ya kutumia akili bandia.
  • Itasaidia kuboresha usikilizwaji wa mashauri na hukumu. 

Mwanza. Huenda kasi ya usikilizaji na utoaji hukumu katika mahakama za Tanzania ikaongezeka baada ya mhimili huo kuanza mchakato kutumia mfumo wa akili bandia (Artificial Intelligence) ili kurahisisha shughuli za mahakama.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Godfrey Ndege akizungumza katika banda la Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Januari 24, 2022 katika uzinduzi wa wiki ya sheria, amesema mfumo huo utahusisha mashine maalumu (robot) zitakazowekewa sheria zote ili ziweze kusikiliza kesi za pande mbili na kutoa maamuzi.

“Mashine hizo zitarishwa sheria mbalimbali na zitakuwa na uwezo wa kusikiliza, kuchakata kisha kutoa maamuzi,” amesema Hakimu Ndege

Ndege amesema mfumo huo utarahisisha utendaji wa mahakama na kupunguza msongamano wa watu mahakamani.

Mbali na mfumo huo pia mahakama ipo kwenye majaribio ya kutumia mfumo wa taarifa (tanzii) ambao utampa fursa mtu kusikiliza na kufuatilia hukumu sehemu yoyote anapokuwa.

Amesema watendaji wa mahakama watakuwa wanachukua maamuzi yatakayotolewa na mahakama, wanayasafisha kisha wanayaingiza kwenye mtandao huo.

“’Kazi itakayokuwa inafanywa na watendaji wa mahakama ni kuprint (kuchapisha), kuskani kisha kusafisha maelezo ya pande zote mbili baada ya hapo zitapandishwa kwenye mfumo huo kwa ajili ya kutolewa hukumu,” amesema Ndege.

Amesema kwa wale watakaohitaji maamuzi yaliyotolewa na  mahakama kuu kwa ajili ya matumizi mengine mfano mahakama za chini wataingia kwenye mfumo huo na kuzikuta.


Zinazohusiana: 


Mbali na mifumo hiyo pia, baada ya ugonjwa wa Uviko-19 kuingia nchini, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilianza kusikiliza kesi za watuhumiwa kwa njia mtandao (video call) ambapo  kunakuwa na Tv mbili upande wa magereza na upande wa hakimu kisha kesi huanza kusikilizwa.

Naibu Msajili wa Kanda ya Mwanza, Chiganga Tengwa amesema wameanzisha mfumo huo ili kupunguza msongamano wa watu mahakamani lakini pia kupunguza gharama za kusafirisha wafungwa kwenda mahakamani kusikiliza kesi.

Amesema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba mwaka 2021, jumla ya kesi 1,403 zilisikilizwa na mahakama hiyo ambapo kati ya hizo kesi 1,306 zilisikilizwa kwa njia ya mtandao.

“Kesi 97 hazikuweza kusikilizwa kwa njia ya mtandao kutokana na unyeti wa kesi hizo kwa kuwa zilikuwa zinajihusisha na mauaji,” amesema Tengwa.

Amesema mahakama inaendelea kuboresha usikilizwaji wa kesi ili kuwapunguzia wananchi gharama na muda wa kwenda kufuatilia ambapo pia iko na mpango wa kuanzisha kituo jumuishi kitakachokuwa na jengo la jaji mkuu, hakimu, mahakama kuu na mahakama ya Mwanza ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW