Si kweli: Chadema yaandika barua ya siri kushiriki Uchaguzi Mkuu
Dar es Salaam. Huenda wewe ni miongoni mwa watu waliokutana na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, hususan mtandao wa Facebook zikidai kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeandika barua ya siri kutoa maelekezo kwa makatibu wote wa chama hicho nchini kushiriki Uchaguzi Mkuu. Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebainisha kuwa habari hiyo si ya kweli.
Taarifa hii ya upotoshaji imesambaa ikionekanama kama barua rasmi lililoandikwa na Chadema ikiwa na mhuri rasmi pamoja na sahihi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika ikitoa maelekezo ya ushiriki wa Uchaguzi Mkuu kwa makatibu wa Chadema kote nchini.
Barua hiyo potoshi imesambaa ikiwa ina mhuri wa ‘SIRI’ ikieleza kuwa maelekezo hayo yanatakiwa kufanyiwa kazi kwa siri kufuatia zuio lililowekwa na Mahakama Juni 10, 2025, kuzuia Chadema, viongozi wake, na wanachama wake, kushiriki au kupanga shughuli yoyote ya kisiasa hadi kesi ya mzozo ndani ya chama kuhusu usambazaji haki wa rasilimali za ndani itakaposikizwa.
“Tunakuletea maelekezo maalum kutoka Makao Makuu ya Chama kuhusu maandalizi ya wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kwa kuzingatia hali ya kisiasa ilivyo sasa na zuio ambalo chama kimewekewa katika baadhi ya shughuli zake, unakumbushwa kuwa mchakato huu ufanyike kwa siri kubwa, kwa umakini wa hali ya juu na bila kuvuja kwa taarifa kwa watu wasiohusika.
Lengo ni kuhakikisha usalama wa wanachama, wagombea watarajiwa, na mafanikio ya mkakati wa kisiasa wa chama chetu,”. Imesomeka barua hiyo.
Aidha, barua hiyo imesambaa ikieleza kuwa mchakato huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kuimarisha msimamo wa Chadema wa “No Reform, No Election” lakini pia imeeleza kuwa ni maandalizi ya kimkakati ya Chadema itakapo ruhusiwa kusaini kanuni za maadili za uchaguzi chama kushiriki uchaguzi.
Barua hiyo iliendelea kutoa maagizo kwa kila kanda kuhakikisha inapendekeza majina ya wagombea wenye sifa, maadili, na uaminifu kwa misingi ya Chadema ifikapo tarehe 12 Agosti 2025.

Katika hatua nyingine ili kufanikisha adhma ya kufanya taarifa hiyo potoshi ionekane kuwa ya kweli, limesambazwa chapisho feki lenye mfanano na chapa ya Chombo cha Habari cha Mwananchi likiwa na Kicha cha Habari kinachosema ‘Maria Sarungi Asema: CHADEMA Hawapaswi Kuaminika Tena,”’.
Katika chapisho hilo, limetumika chapisho linaloonekana kuwa limechapishwa na Sarungi katika akaunti yake rasmi ya Mtandao wa X (zamani Twitter) likiambatana na barua feki inayosambaa linalosomeka, “CHADEMA ni wanafiki wa kiwango cha juu !! Hadharani wanapiga kelele za “NO REFORMS, NO ELECTION” huku nyuma ya pazia wanatuma barua kwa msajili kuomba kushiriki uchaguzi. Wanakataza wengine wasishiriki, wakati wao wanajiandaa kimyakimya! Huu ni usaliti !!”
Ukweli ni huu
Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebainisha kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote zimesambazwa ili kupotosha.
Nukta Fakti imewasiliana na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ambaye barua inayosambaa imeonekana kusainiwa nae na amekanusha na kusema kuwa barua hiyo ni feki.
“Ni feki na hakuna ukweli wowote kwenye taarifa hizo,” amesema Mnyika.
Aidha, Nukta Fakti imebaini kuwa aina ya mwandiko (fonts) uliotumika kwenye barua inayosambaa si mwandiko unaotumiwa katika barua rasmi za Chadema.
Katika hatua nyingine uchunguzi umebainisha kuwa chapisho la Mwananchi linalosambaa ni feki, halijachapishwa na chombo hicho cha habari kinachoaminika nchini na halipo kwenye akaunti rasmi za mitandao ya kijamii ya chombo hicho.
Pia, Nukta Fakti imegundua kuwa ushahidi wa chapisho la mtandao wa X la Sarungi uliotumika kama chanzo cha taarifa kuunga mkono kusambaa kwa taarifa ya barua feki ni batili, halijachapishwa na Maria Sarungi, halipo kwenye akaunti rasmi ya mwanaharakati huyo na aina ya mwandiko unaoonekana kwenye chapisho si mwandiko wa kwenye machapisho halisi ya mtandao wa X.
Latest