Magufuli: Uwepo wa mahakama unaongeza uhuru kwa wawekezaji
- Asema Serikali itaendelea kujenga mahakama kuwapa uhuru wafanyabiashara na wawekezaji.
- Asema mahakama zinawahakikishia usalama wa mali zao na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali itaendelea kujenga mahakama katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania ili kuwapa uhuru wafanyabiashara na wawekezaji kuendesha shughuli zao na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Dk Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Desemba 18, 2019) katika uzinduzi jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Zimamoto la Wilaya ya Chato mkoani Geita, amesema mahakama ni sehemu muhimu kwa watu kupata haki zao na kusuluhisha migogoro kwenye jamii.
“Mahali penye mahakama, hata wafanyabiashara na wawekezaji hujisikia huru kufanya shughuli zao za biashara na uwekezaji kwa kuwa wanakuwa na uhakika wa usalama wa mali zao, hii inasaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi,,” amesema Rais Magufuli.
Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuvutia wawekezaji kuwekeza nchini ikiwemo kuboresha miundombinu ya usafirishaji na utoaji huduma ili kuhakikisha maeneo yote ya uzalishaji yanafikika kirahisi.
Uwepo wa mahakama pia unaweza kusaidia kutafsiri na kutatua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wawekezaji katika shughuli zao nchini.
Zinazohusiana:
- Tanzania yatajwa kwenye nchi 10 za mwisho matumizi ya Tehama
- Mahakama Tanzania ni mwendo wa kidijitali utoaji wa huduma
Aidha, Rais amesema ujenzi wa mahakama ni muhimu pia katika kuharakisha upatikanaji wa haki za wananchi, na Serikali itaendelea kujenga mahakama za kisasa kulingana na upatikanaji wa fedha
“Ni matumaini yangu kuwa ujenzi wa mahakama hivi utasaidia kuharakisha uendeshaji wa kesi na hivyo kupunguza mrundikano wa mahabausu katika magereza yetu,” amesema Rais na kubainisha kuwa zaidi ya nusu ya watu waliopo magerezani katika nchi yetu ni mahabusu ambao wanasubiri kusikilizwa kwa kesi zao.
“Kabla ya msamaha nilioutoa (Siku ya kuadhimisha Uhuru wa Tanzania Desemba 9, 2019) magereza yetu yalikuwa na watu 35,803 ambapo wafungwa walikuwa 17, 547 na mahabusu walikuwa na idadi kubwa kuliko wafungwa walikuwa 18,256,” amesema Rais.