Magufuli ‘awawashia moto’ waliochukua fedha za wafanyabiashara Morogoro
Rais John Magufuli akizungumza na wafanyabiashara wa soko kuu la Morogoro baada ya kulifungua leo Februari 11, 2020 mkoani Morogoro. Picha|Msemaji Mkuu wa Serikali.
- Ni baadhi ya watendaji waliowatoza fedha za ziada wafanyabiashara waliopata vizimba katika soko kuu la Morogoro lililopo mkoani Morogoro.
- Awataka warudishe kama wanapenda kuendelea na kazi zao.
- Asema soko hilo ni kitovu cha maendeleo.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka baadhi ya watendaji wa manispaa ya Morogoro kurejesha fedha za ziada walizowatoza wafanyabiashara waliopata vizimba katika soko kuu la Morogoro lililopo mkoani Morogoro.
Dk Magufuli ametoa maagizo hayo leo Februari 11 alipozindua soko hilo lilipo Manispaa ya Morogoro lenye maduka 304, vizimba 900, eneo la maegesho ya magari madogo 150 na magari makubwa 50.
Pia lina eneo la maegesho ya bajaji, pikipiki na baiskeli, stoo 36 za mitumba pamoja na sehemu ya kutupa takataka.
Amesema wapo wafanyabiashara waliopewa vizimba vyao bila tatizo lakini wengine walipewa vizimba kwa kukodishwa na madalali na baadhi ya madalali hao ni wafanyakazi wa Manispaa ya Morogoro.
“Vizimba vinatakiwa kulipwa Sh20,000 kwa mwezi yeye anatozwa na mfanyakazi wa manispaa anaitwa Aika, analipa Sh50,000 kwa mwezi, sifahamu huyo Aika kama yupo hapa… nimeshatoa maelekezo kama bado huyo Aika anapenda kazi na wale wafanyakazi wengine wa manispaa kama bado wanapenda kazi hizo fedha zote walizozichukua za watu waliowakodisha pale ‘wazitapike’ kuanzia leo,” amesema Rais Magufuli.
Zinazohusiana:
- Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage joto la korosho likipanda
- Serikali yatoa maagizo mazito kwa wanunuzi wa korosho
Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema kama mfanyakazi wa manispaa anaweza akala kamisheni ya Sh30,000 kila mwezi kwa kutumia jengo la Serikali ambalo hajawekeza hiyo ni rushwa.
“Kwa hivyo najiuliza maswali mengi uongozi wa hapa Morogoro ukoje? Ninasikia Mkuu wa Wilaya anaunda tume ya nini… ya nini ukahangaike kuunda tume ya kuchunguza wakati ukichukua kibanda uangalie kwa saa tano utaona tu…
“Sasa tume nayo ukailipe hela na posho, nataka uozo huo uliomo humu kwenye soko kuanzia leo ukome,” amesisitiza Rais.
Ujenzi wa soko hilo la kimkakati kwa mujibu wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Joseph Nyamhanga, ulianza Juni 20, 2018 na kukamilika Julai 20, 2020.
Ujenzi wa soko hilo umegharimu Sh17.6 bilioni zinazojumuisha Sh14.9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wenyewe na Sh 2.6 bilioni ambazo ni malipo ya ongezeko la thamani.
Uwepo wa soko hilo una manufaa mengi kwa maendeleo ya wakulima na wafanyabiashara kwa sababu wanapata maeneo mahususi ya kuuza bidhaa zao lakini pia wananchi wanapata eneo la kupata huduma na Serikali inakusanya kodi katika soko hilo.
Latest
