Magufuli atoboa siri za Tanzania kutekeleza mradi wa Stiegler’s Gorge

December 12, 2018 9:55 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Katika mradi huo zitajengwa kuta kubwa mbili zenye urefu wa mita 1,025 na kimo cha mita 131, bwawa la kutunza maji lenye urefu wa kilomita 100 na upana wa kilomita 25 na kituo cha kufua umeme. Picha| Construction Review Online.


  • Amesema walitumia vigezo vikubwa yaani uhakika wa chanzo chenyewe, gharama za utekelezaji, gharama za uzalishaji pamoja na tija na kubaini kuwa mradi huo ndio unaifaa Tanzania kwa sasa.
  • Mradi huo unatakelezwa katika pori la akiba la Selous ambalo baadhi ya wadau wamekuwa wakipinga kuwa utaathiri mazingira na viumbe waliopo eneo hilo.
  • Miongoni mwa miundombiniu muhimu ya mradi huo ni bwawa la kutunza maji lenye urefu wa kilomita 100 na upana wa kilomita 25 lenye uwezo wa kubeba maji mita za ujazo bilioni 35.2.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameeleza sababu za Serikali kuendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler’s Gorge licha ya kupingwa na baadhi ya watu akisema una gharama ndogo za uzalishaji ukilinganisha na vyanzo vingine na utapunguza bei ya umeme na kuchochea shughuli za maendeleo.

Kwa muda mrefu sasa baadhi ya watetezi wa mazingira wamekuwa wakipinga ujenzi wa mradi huo mkubwa nchini wakileleza kuwa utaathiri mazingira na viumbe vilivyopo katika pori la akiba la Selous ambalo mwaka 1982 lilipewa hadhi ya kuwa urithi wa dunia na Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (Unesco).

Lakini leo (Desemba 12, 2018) wakati akitoa hotuba baada ya kushuhudia utilianaji saini wa ujenzi wa mradi huo baina ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni mbili kutoka Misri, Rais Magufuli amesema Serikali ilifanya uchambuzi wa kina kabla ya kuamua kuutekeleza na kubaini kuwa utakuwa suluhu kwa mahitaji ya sasa ya nishati.

Kampuni ya Arab Contractors ikishirikiana El Sewedy Electric imepewa kandarasi ya kujenga mradi wa umeme utakaojengwa katika bonde la Mto Rufiji na kugharimu Dola za Marekani bilioni 2.9 sawa na zaidi ya Sh6.5 trilioni.

Katika uchambuzi huo, Dk Magufuli amesema waliangazia vyanzo vyote vya nishati vilivyopo nchini kama upepo, makaa ya mawe, madini ya urani, gesi asilia, na mafuta na kulinganisha na mahitaji ya sasa ya nishati hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda.

“Baada ya kutafakari kwa kina hususan kwa kutumia vigezo vikubwa yaani uhakika wa chanzo chenyewe, gharama za utekelezaji (Investment costs), gharama za uzalishaji (generation costs) pamoja na tija tulibaini kuwa mradi huu ndio unaifaa zaidi nchi yetu kwa sasa,” amesema Rais. 

Amesema mradi huo utakaozalisha Megawati 2,115 ni wa uhakika kwa kuwa una uwezo wa kuzalisha umeme kwa zaidi ya miaka 60 na utatumia maji yanayotoka katika mtandao wa mito iliyopo kwenye mikoa yenye wastani mkubwa wa mvua.

“Gharama zake za utekelezaji sio kubwa sana ukilinganisha na vyanzo vingine, kama nilivyosema mradi huu utagharimu Sh6.5 trilioni ukitumia vyanzo vingine kutekeleza mradi huu kuzalisha megawati 2,115 tungetumia fedha nyingi sana,” amesisitiza Rais.

Kuhusu gharama za kuzalisha, ameeleza kuwa uniti moja ya umeme wa maji ni Sh36 ukilinganisha na vyanzo vingine ambavyo ni ghali ikiwemo mafuta ambacho hugharimu Sh446, ikiwa ni mara 12 zaidi ya ule unaozalishwa na maji.

Kutokana na uwekezaji huo, Rais amesema uzalishaji wa umeme nchini utaongezeka zaidi kutoka uzalishaji wa sasa wa megawati 1,560 na utakapokamilika bei ya umeme itapungua na kuwaletea wananchi nafuu ya upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa kuchochea shughuli uchumi ikiwemo viwanda, kilimo, umwagiliaji na michezo. 

Mpango wa Serikali ni kufikia uzalishaji wa umeme wa megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 na hatimaye megawati 10,000 itakapofika mwaka 2025.


Zinazohusiana: Rais Magufuli akosoa mapendekezo ya ripoti ya mazingira Stiegler’s Gorge


Rais Magufuli ametumbilia mbali maoni ya wakosoaji wa mradi huo wanaouhusisha na uharibifu wa mazingira akieleza kuwa “umeme wa maji ni rafiki wa mazingira” na kwamba eneo litakalotumika kutekeleza mradi huo ni dogo kati ya asilimia 1.8 hadi asilimia 2 la eneo lote la hifadhi ya Selous.

Sambamba na hilo utapunguza ukataji wa miti inayotumika katika vyanzo vya kuni na mkaa zaidi na wakazi wa mjini katika matumizi ya nyumbani.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema mkandarasi wa mradi huo atakuwa na majukumu makuu manne ya kujenga kuta kubwa mbili zenye urefu wa mita 1,025 na kimo cha mita 131, “kujenga bwawa la kutunza maji lenye urefu wa kilomita 100 na upana wa kilomita 25 lenye uwezo wa kubeba maji mita za ujazo bilioni 35.2”.

Kazi nyingine, Dk Kalemani amesema ni kujenga mtambo mkubwa wa kuzalisha umeme utakaokuwa na mitambo tisa na kila mmoja utazalisha megawati 235 zitakazofikisha megawati 2,115.

 Kazi ya nne ni kujenga kituo cha kufua umeme mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda chenye msongo wa kilovoti 400.

Utiaji saini wa mkataba huo umeshuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Waziri Mkuu wa Misri, Mostafa Madbouly ambapo amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kuwaomba  watanzania kushikamana hadi hapo mradi huo utakapokamilika.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV