Rais Sami: Reli ya kisasa itajengwa kwa mkopo
- Amesema ni lazima reli hiyo ijengwe.
- Serikali itakopa fedha na siyo kodi za ndani kuijenga reli hiyo.
- Ataoa maagizo mazito kwa watendaji wanaoijenga.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwa vyovyote itakavyokuwa ni lazima ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka jijini Dar es Salaam hadi mkoani Mwanza ukamilike kwa wakati na fedha zitakazotumika katika ujenzi huo siyo kodi za ndani bali ni mikopo yenye masharti nafuu.
Rais Samia amesema reli hiyo ina umuhimu mkubwa katika uchumi wa nchi kwa sababu itarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo ndani na nchi jirani, hivyo lazima ijengwe kama ilivyokusudiwa.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amebainisha kuwa uwekezaji wa ujenzi wa vipande vinne kati vitano vya awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo umefikia Sh14.7 trilioni ukijumlisha na kodi na hatakubali fedha hizo zipotee bure bila kukamilisha mradi.
“Tusipoendelea na reli hii tukakamilisha, fedha hizi tulizozilaza pale chini zitakua hazina maana,” amesema Rais Samia na kusisitiza kuwa ni lazima Serikali ikope fedha kukidhi mahitaji ya mradi huo.
“Kwa hiyo kwa njia yoyote kwa vyovyote tutakopa, tutaangalia njia rahisi zitakazotufaa za kukopa kwa sababu fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo wala kwenye kodi tunazokusanya ndani,” amesisitiza Rais Samia.
Rais Samia aliyekuwa akishuhudia utiaji saini mkataba wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) awamu ya tatu kipande cha Makutupora hadi Tabora leo Desemba 28, 2021 Ikulu, Jijini Dar es Salaam amesema atashauriana na wataalam wa masuala ya fedha ili kupata mikopo yenye masharti nafuu inayolipika.
“Niwaombe ndugu zangu mnaosimamia hii sekta twendeni, mimi niko pamoja nanyi tutasimama kuangalia mikopo inayotufaa tukiongozwa na Gavana wa Benki Kuu na Waziri wa Fedha yuko hapa atatuongoza mikopo gani itatufaa tutachukua tumalize reli hii muda uliopangwa ili iweze kutengeneza fedha tulipe mikopo tunayochukua,” amesema.
Soma zaidi:
-
RC Mwanza aagiza haki itendeke ulipaji fidia ujenzi reli ya kisasa
-
Wizi wa mafuta reli ya kisasa wamkera waziri
Kipande cha reli ya kisasa kutoka Mukutopola hadi Tabora kina urefu kilomita 368 na ujenzi wake utagharimu Sh4.41 trilioni huku ujenzi wake ukisimamiwa na mkandarasi Yapi Merkezi kutoka nchini Uturuki.
Mkandarasi huyo anajenga vipande vitatu kati ya vitano vya reli hiyo yenye mtandao usiopungua kilomita 2,561 ikiunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Katavi na nchi zisizokuwa na bandari (Rwanda, Burundi na Congo DRC).
Atoa maagizo mazito
Rais Samia ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kumpata mkandarasi kukamilisha kipande kilichobaki cha Tabora -Isaka na kipande kipya cha awamu ya ujenzi wa reli ya SGR kutoka Tabora hadi Kigoma.
“Nitoe maelekezo kwamba tunapokwenda kumaliza (reli ya SGR) kipaumbele kitolewe kwa yale matawi yanayotuunganisha na nchi za jirani ili tuweze kurahisisha biashara zetu, kuingia kwenye masoko jirani,” amesema.
Ujenzi wa reli hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2017, amesema lazima uwe wa kimkakati hasa kuifikia nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Congo DRC) kwa sababu ni nchi yenye fursa nyingi inayokimbiliwa na watu wengi.
“Tunapozubaa sisi hapa, Tanzania hatupo peke yetu, tumepakana na nchi kadhaa, njia tunazozitumia sisi kujenga reli, kupanua bandari nchi jirani zinafanya hivyo hivyo na mbio zetu ni kuikimbilia Congo DRC kwa sababu ni soko kubwa,” amesema Rais huku akiagiza ujenzi wa reli ya kisasa lazima uende kwa kasi ili ikamilike mapema.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitembea kwenye mfano wa reli ya Kisasa itakayojengwa kutoka Mwanza hadi Isaka mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika sherehe zilizofanyika Fela mkoani Mwanza leo tarehe 14 Juni, 2021. Picha| Michuzi.
Aidha, ameagiza kasi ya ununuzi wa vifaa vitakavyotumiwa na reli hiyo yakiwemo mabehewa iendane na kasi ya ujenzi wake ili itakapokamilika ianze kutoa huduma kwa wakati.
Sambamba na hilo ameagiza wizara inayohusika na ununuzi wa vifaa hivyo, pia izingatie ubora wa vifaa vya reli vinanunuliwa na kuhakikisha vinaendana na thamani ya fedha zilizotolewa.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Msanja Kadogosa amesema lengo la reli hiyo ni kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji nchini ususani sekta ya reli ambapo itabeba mzigo wa mpaka tani 10,000 kwa mkupuo sawa na uwezo wa maroli 500 ya mizigo na kuokoa muda wa usafirishaji abiria na mizigo.
Pia itachangia katika ongezeko la ajira kwa wazawa katika sekta na fani mbalimbali na uboreshaji wa huduma za kijamii ikihusisha ujenzi wa shule, vituo vya afya na ujenzi wa barabara katika maeneo yanayopitiwa na mradi huo.