Magufuli aagiza makinikia yaliyozuiwa bandarini kupigwa mnada

January 24, 2020 11:53 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni makontena zaidi ya 200 ya mchanga wa dhahabu yaliyokuwa yanasafirishwa nje ya nchi na iliyokuwa kampuni ya dhahabu ya Acacia. 
  • Asema fedha zitakazopatikana zitakuwa za kampuni ya Twiga Minerals Corporation Limited.
  • Ashuhudia utiaji saini wa mikataba tisa na kampuni ya Barrick. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza makontena ya mchanga wa madini ya dhahabu maarufu kama makinikia yaliyokamatwa katika Bandari ya Dar es Salaam mwaka 2017 yauzwe na fedha zitakazopatikana zitakuwa za kampuni ya Twiga Minerals Corporation Limited.

Kampuni hiyo inayosimamia migodi mitatu ya North Mara, Buzwagi na Bulyanhulu iliyokuwa chini ya kampuni ya Acacia, ilianzishwa hivi karibuni na inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Barrick.  

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Januari 24, 2020) Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa utiaji saini wa mikataba tisa kati ya Tanzania na Barrick, amesema baada ya kuhitimisha mivutano ya muda mrefu ya mapato na kampuni hiyo sasa ameruhusu makinikia yaliyokamatwa yauzwe. 

“Makubaliano hayo yamemaliza mivutano kati ya pande zote mbili. Na kwa kuanzisha kampuni hii ya Twiga nataka kuwahakikishia kuwa yale makontena (ya mchanga wa madini wa dhahabu) ambayo yako bandarini ambayo tuliyashika sasa mkatafute wabia wazuri muuze mpate faida ya kampuni ya Twiga,” amesema Dk Magufuli.

Machi 2 mwaka 2017, Rais Magufuli alipiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini ya dhahabu nje ya nchi akisema kuwa ni wizi kwa sababu mchanga ukifika huko unachambuliwa na kupatikana dhahabu.

Hata hivyo, Rais hajazungumzia kama umeondoa marufuku ya usafirishaji wa mchanga huo nje ya nchi ama la. 

Rais John Magufuli leo (Januari 24, 2020) Ikulu jijini Dar es Salaam ameshuhudia utiaji saini wa mikataba tisa kati ya Tanzania na Barrick. Picha|Mtandao.

Amesema anafahamu kuwa mchanga huo wa madini ya dhahabu ulikuwa unauzwa kabla ya kusafirishwa nje ya nchi na mnunuzi anajulikana na alilipa tayari sehemu ya fedha lakini anaweza kununua tena. 

“Pamoja na stori kwamba zinapelekwa kwenye kuyeyushwa it was not true (ilikuwa siyo kweli), yalikuwa yanauzwa yakiwa bado yako huku na mnunuzi ninamjua na alikuwa amelipa asilimia fulani. 

“Sasa kama huyo mnunuzi anataka kununua anunue kwa sababu tunajua faida itakayopatikana ni kwa ajili ya kampuni yote,” amesema Rais Magufuli.

Baada ya Rais John Magufuli kuzuia usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi, baadhi ya watu wakiwemo wanaharakati walijitokeza na kupinga hatua hiyo wakidai itaikosesha Serikali mapato.

Akizungumzia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Barrick baada ya majadiliano ya zaidi ya miaka mitatu, amesema ni ushindi mkubwa kwa Watanzania kwa sababu wanaenda kufaidika na rasilimali ya madini. 

“Kwa hiyo imagine (fikiria) kutoka kwenye share ya zero (hisa sifuri) mpaka ukapate asilimia 16, lakini pia faida itakayokuwa inapatikana ni 50/50 ni ushindi mkubwa kwa maendeleo yetu,” amesema Rais. 


Zinazohusiana:


Mikataba tisa yasainiwa kwa wakati mmoja

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, ameitaja mikataba iliyosainiwa mbele ya Rais Magufuli kuwa ni Mkataba wa Msingi wa Makubaliano, Mkataba wa Menejimenti na Utoaji Huduma, Mkataba wa Wanahisa wa kampuni ya North Mara na Mkataba wa Wanahisa wa kampuni ya Twiga, 

Mikataba mingine ni Mkataba wa Wanahisa wa kampuni ya Bulyanhulu, Mkataba wa Wanahisa wa kampuni ya Pangea Buzwagi, Mkataba wa Maendeleo wa Mgodi wa North Mara,  Mkataba wa Maendeleo wa Mgodi wa Bulyanhulu na Mkataba wa Maendeleo wa Mgodi wa Buzwagi.  

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Barrick wamekabidhi hati ya umiliki wa hisa za Serikali za asilimia 16 katika kampuni ya Twiga kwa Msajili wa Hazina. 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold,  Dk Mark Bristow amesema kampuni hiyo itajifunza kwa makosa iliyoyafanya nchini Tanzania miaka 10 iliyopita kama watashindwa kujifunza hawastahili kuendelea na shughuli uchimbaji madini nchini. 

“Sisi wawekezaji tunapokuja katika nchi kama hii tuna jukumu kubwa la kuchimba rasilimali ya Taifa si kwa faida yetu tu bali kwa faida pia ya Taifa na wadau wengine. Wadau hao siyo tu wanahisa bali wananchi na ndiyo maana ni wajibu wetu kulipa kodi,” amesema Dk Bristow. 

Enable Notifications OK No thanks