Maadhimisho ya Tanzanite yaahirishwa kupisha maombolezo ajali ya Mv Nyerere

TULINAGWE MALOPA 0949Hrs   Septemba 24, 2018 Habari
  •  Madini hayo yaligunduliwa miaka 51 iliyopita na Mvumbuzi, Jumanne Ngoma eneo la Mererani, Manyara.
  • Maombolezo ya ajali ya Mv Nyerere yasitisha shughuli za maadhimisho.
  • Mzee Ngoma amshukuru Rais John Magufuli kwa kutambua kazi yake na kumpa pesa ya matibabu.

Dar es Salaam. Taasisi ya Tanzania Founder Foundation (TAFFO) imeahirisha kuadhimisha miaka 51 ya kugunduliwa kwa madini ya Tanzanite ili kuungana na watanzania katika maombolezo ya watu waliofariki katika ajali ya Mv Nyerere iliyozama Septemba 20 mwaka huu katika Ziwa victoria.

 TAFFO ilianzishwa mwaka 2013 ikiwa ni sehemu ya kuenzi na kutambua mchango wa mgunduzi wa madini ya Tanzanite, Jumanne Ngoma. 

 Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Asha Ngoma amesema kutokana na msiba uliotokea katika Ziwa Victoria, maadhimisho hayo hayakufanyika kama kama ilivyopangwa, badala yake wamekutana na wanahabari ili kuelezea kinachojiri.

 “Taasisi ya Tanzania Founder Foundation leo imeona iadhimishe siku hii kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu madini haya ikiwa ni pamoja na kutoa historia fupi kwa kutathmini tulipotoka na tulipo kwa sasa ikiwa ni pamoja na kuudhihirishia ulimwengu kuwa madini ni fahari yetu na urithi wetu Tanzania.

Amesema hatua ya Serikali kujenga ukuta wa Mererani ili kulinda utoroshaji wa madini hayo ni mzuri kwasababu inalenga kuwanufaisha watanzania na rasilimali zilizopo nchini.

 “Hatua ya Serikali kumtambua rasmi mgunduzi wa madini hayo na kujenga ukuta kulinda madini ni hatua nzuri ya kuyaongezea thamani,” amesema Asha.


Zinazohusiana:


Ukuta huo wenye urefu wa kilomita 24.5 na urefu wa mita tatu kwenda juu umejengwa kuzunguka mgodi wa madini ya Tanzanite huko Mrerani, mkoa wa Manyara, kaskazini mwa Tanzania umejengwa kufuatia agizo lililotolewa na Rais John Magufuli, kama jitihada za kudhibiti na kuzuia utoroshwaji wa madini hayo, ambayo yanapatikana nchini Tanzania pekee.

Mvumbuzi wa madini hayo, Jumanne Ngoma, amesema anamshukuru Rais John Magufuli kwa kutambua mchango wake wa katika sekta ya madini na kumpatia pesa za matibabu, “Namshukuru sana Rais kwa kuniunga mkono kwa kazi ya mikono yangu.”

Mzee Ngoma alianza utafiti wake katika kijiji chake cha Makanya, Wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro ambapo aligundua Madini ya Gypsum. Baadaye alijiendeleza zaidi na kupata elimuya madini na kuamua kwenda Merarani, katika eneo la Lalouo kijiji cha Naisunyai kufanya utafiti wa yale mawe aliyoyaona wakati anachunga mifugo ya baba yake. 

Mwaka 1967 Januari, aliamua kuyapeleka mawe hayo katika ofisi ya madini Moshi kwa uchunguzi lakini alishauriwa ayapeleke Dodoma.

Mnamo Septemba 23, 1967 maabara ya Dodoma ilithibitisha kuwa ni madini ya Zoisite ambayo kwa wakati huo hayakuwa na soko, lakini wakashauri huenda yakawa na soko siku zijazo.

Mnamo Mwaka 1984, Serikali ya Jamhuri ya muungano ilimtambua rasmi Mvumbuzi ya madini hayo na kuyapa jina la "TANZANITE" jina lililotokana na jina la nchi, yaani Tanzania na Zoisite na likapatikana jina hilo na kutunikiwa cheti cha uvumbuzi katika sherehe ya siku ya wafanyakazi zilizofanyika mkoani Mbeya.

Mwenyekiti wa taasisi TAFFO, Asha Ngoma (katikati) akizungumza na Wanahabari leo kuhusu maadhimisho ya miaka 51 ya madini ya Tanzanite. KUshoto ni Mvumbuzi wa madini hayo, Mzee Jumanne Ngoma pamoja watendaji wengine wa Taasisi hiyo. Picha| Michuzi blog.

Related Post