Mafundi sanifu zaidi ya 500 kugonganisha vichwa Mwanza wiki hii
- Watakutana kujadili namna ya kuendeleza ubunifu Tanzania
- Pia kupata uzoefu kwa wabunifu waliofanikiwa akiwemo Masoud Kipanya.
Mwanza. Zaidi ya mafundi sanifu 500 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wanatarajia kukutana jijini Mwanza kujadili masuala mbalimbali yanayohusu tasnia yao ikiwemo kuendeleza ubunifu ili kutafuta suluhu kwa changamoto zilizopo nchini.
Miongoni mwa watakaohudhuria katika majadiliano hayo ni Mtangazaji wa redio na mchora katuni Masoud Ally (Masoud Kipanya) ambaye amezindua gari linalotumia umeme ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB), Bernard Kavishe amesema katika majadiliano hayo pia kutakuwa na maonyesho ya kibunifu.
“Tumeona ipo haja ya mwandishi huyo kushiriki kwenye mkutano huu, Kipanya ni mbunifu ana mawazo mengi mazuri atakuja hapa tutampa nafasi atazungumza na tutatoa nafasi kwa gari lake kuonekana,” amesema Kavishe.
Katika mkutano huo utakaofanyika Mei 4 na 5, 2023 jijini Mwanza ambao utafunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi-Ujenzi, Balozi Aisha Amour, pia kutakuwa na viapo kwa wahandisi ambao hawajaapa pamoja na maonyesho ya ubunifu yakiwemo magari ya umeme yaliyobuniwa na Watanzania.
“Bodi ina utaratibu wakuwakutanisha mafundi sanifu kwa kuwa ndio askari wetu wa mstari wa mbele wajadili tasnia yao, mchango wao katika maendeleo ya Taifa kwa sababu tasnia hizi hazipoi ni kama zimewekewa amira kila uchwao,” amesema.
Katika hatua nyingine Kavishe amewaonya wahandisi pamoja na waajiri wao wanaofanya kazi zinazohusu tasnia hiyo bila leseni akidai bodi hiyo itafikia hatua ya kuchapisha majina ya wahandisi waliosajiliwa ambao watatakiwa kufanya kazi.
“Hatutangulizi fimbo, sasa hivi tunafanya kama ushawishi lakini tutafika mahali tutatoa mkeka, tutatoa PDF jamani hawa ndio unaweza kufanya nao kazi, kama mtu hayupo kwenye hii huyo ebu muangalieni tena lakini tutatoa muda wa kutosha watu wajitokeze wauhuishe leseni,” amesema.