Madhara ya matumizi ya dawa za nywele, mawigi kwa wanawake

August 14, 2020 2:13 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Mbali na ufifishaji wa ubora wa nywele, wengi huishia kupata vidonda kichwani kutokana na baadhi ya dawa kuwaunguza.
  • Wataalamu wasema matumizi ya dawa hizo kwa muda mrefu zinaweza kusababisha saratani.
  • Kujiamini, kujipenda na kuwa na amani bila ya kuwa na nywele bandia ni kati ya vitu wanavyovikosa wanawake wanaotumia dawa.

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wanawake wakipaka dawa za nywele maarufu kwa Kiingereza kama ‘relaxers’ inaweza kuonekana kama urembo wa kawaida kabisa. Lakini urembo huo kuna wakati una gharama zake zikiwemo za kiafya na kisaikolojia kutokana na baadhi kuhusisha kiasi fulani cha kemikali. 

Wataalamu wanaeleza kuwa matumizi ya dawa kama relaxers yana athari ambazo mtumiaji wa dawa hizo anazipata baada ya kufurahia nywele laini zikiwemo figo kuchoka na magonjwa kama saratani na hata matatizo ya uzazi.

Dk Elizabeth Lema,,mtaalamu wa masuala ya afya kutoka Kliniki ya utunzaji wa afya kwa njia za asili (Natural health care clinic) iliyopo Victoria jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa kushamiri kwa matumizi ya bidhaa za kulainisha nywele miongoni mwa wanawake ni sababu kubwa inayochochea matatizo yanayowakumba baadhi yao.

Daktari huyo ambaye anatibu watu kwa kutumia mimea na matunda, anasema dawa nyingi za kulainisha nywele zinakuwa na kemikali ambazo siyo nzuri kwa mwili wa binadamu.

“Zamani kesi za uvimbe kwenye vizazi hazikuwepo kabisa, baada tu ya kushamiri kwa matumizi ya vipodozi na bidhaa zenye kemikali, matatizo ndipo yalipoanzia,” anasema Dk Lema ambaye pia ni mdau wa vipodozi asilia. 

Mara nyingi, dawa hizo ambazo wanawake huwekewa wanapoenda saluni zimekuwa zikiwapatia matokeo ya muda mfupi ya kunng’arisha nywele na kuzifanya zionekane kama za wanawake wa nchi Magharibi kama Ulaya au America. Hata hivyo, mara kadhaa, meli ya urembo huo huenda mrama.

“Inaunguza! inakuunguza ngozi ya kichwa. Kwa mara ya kwanza, nilivumilia maumivu lakini baadaye nilikuja kukuta dawa imeniunguza kichwa. nilikuta vidonda kichwani,” mkazi wa Rufiji mkoani Pwani, Zamdazitta Kumbakumba ambaye kwa sasa ameamua kubaki na nywele asilia.

“Haiwezi kuwa salama kuweka vitu kama hivyo kichwani japo wapo watu ambao kwao inafanya kazi vizuri. Kwangu niliungua, nikalazimika kunyoa na kuanza upya,” anasema dada huyo ambaye ni Mhandisi wa masuala ya usalama anayeishi wilayani.

Dk Lema amesema, unachokiweka nje ya mwili wako, kinaingia karibia asilimia 60 ndani ya mifumo yako ya mwili. Picha| Hype hair. 

Mbali na kuungua kichwa ambalo ni jambo linatokea endapo dawa (relaxer) itabaki kichwani kwa muda mrefu, kuna madhara mengine yanayoambatana na kuweka dawa pamoja na kuvaa mawigi au kushonea nywele bandia.

Dk Lema anasema mwanadamu siyo kitu kilichotengenezwa maabala kwani ni kiumbe kilichotokana na “nature” (asili) hivyo pale anapotumia vitu vya kemikali, lazima vitaingiliana na asili yake.

“Kitu kimoja kikubwa ambacho kimeathirika na kinaendelea kuathirika na matumizi ya kemikali haswa za ngozi na nywele ni homoni. Miaka ya zamani tulikuwa hatusikii ‘Fibroid’ (uvimbe tumboni” miaka ya sasa Fibroid ndiyo imekuwa stori. Kila mtu ana homoni zisizowiana (balance),” anaeleza Dk Lema.

Mtaalamu huyo anaeleza kuwa matokeo ya kutokuwepo na uwiano wa homoni mwilini ndiyo sababu kubwa ya mtu kuonekana mtu mzima kuliko umri wake, kutokupata ujauzito na hata hedhi kuruka ruka kwa baadhi ya wanawake pamoja na kufeli kwa figo.

“Tunakula kemikali, tunapaka kemikali, tunatumia kemikali kwenye nywele zetu. Wanaoenda saluni, wanaelewa, unapoweka zile dawa, kuna zingine zinakuunguza kabisa. Unatakiwa kujua kitu kimoja, unachokiweka nje ya mwili wako, kinaingia karibia asilimia 60 ndani ya mifumo yako ya mwili.

Ndiyo maana siku hizi figo zinafeli sana kwa sababu watu hawafikiri kuwa kitu wanachopaka ni sawa na wanachokula,” anaeleza Dk Lema ambaye amesema katika wagonjwa anaowahudumia, huwaangalia vipodozi wanavyovitumia na kuona kama kina uwiano na matokeo hasi ya vipodozi wanavyovitumia.

Dk Elizabeth Lema ni Mtaalamu wa masuala ya afya kutoka kliniki ya utunzaji wa afya kwa njia za asili (Natural health care clinic) iliyopo Victoria jijini Dar es Salaam ambaye pia ni mdau wa vipodozi asilia. 

Gharama za kisaikolojia

Mbali na changamoto za kiafya, zipo baadhi ya changamoto ambazo zinaishia kuwakumba wanawake wengi katika shughuli zao za kila siku.

“Kuna mwanamke ambaye akitembea bila wigi au mywele anajiona kuwa siyo mwanamke bado. Apate wigi au rasta zimfikie hadi mgongoni hapo ndo mnaweza kuelewana. 

Niliwahi kuwa na mahusiano na mwanamke ambaye sikuwahi kuona nywele zake halisi. Kichwa chake kilikuwa bandika bandua,” anasema Yohana Kulwa Mkazi wa Buzuruga jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa Kulwa, mpenzi wake huyo alikuwa na mawigi mengi mbali na mitindo ya kusukwa aliyokuwa akijihusisha nayo.

“Nilimwambia mbona wewe ni mzuri tu bila hizo nywele lakini alisema bila hizo mambo kichwani hajisikii kabisa,” ameongeza Kulwa.

Pia, Dk lema anasema kemikali zinapoingilia mifumo ya homoni mwilini, zinaingilia pia mifumo hisia na ni chanzo kikubwa cha kuwa na mihemko (moods) isiyoeleweka.

“Ukiwa na hormonal imbalance (homoni zisizokuwa na uwiano) unakuwa ni mtu ambaye haueleweki unakuwa na furaha mara hasira kwa sababu kemikali zinaingilia hisia zako,” anasema Dk Lema.


Zinazohusiana:


Matumizi mabaya ya fedha yananyowatesa kina baba na familia

Mussa Mazuri mkazi wa Kasamwa mkoani Geita anasema mke wake ni mtu ambaye anajali nywele zake.

Mazuri anasema “kila siku nakuta dawa mpya ya nywele mezani unakuta nyingine hata haijaisha. Ukimuuliza anakwambia ameshauriwa na shoga yake akanunue hiyo inajaza nywele na kuzizuia zisikatike. Unatikisa tu kichwa unaendelea na yako.” 

Kinachomuuma zaidi Mazuri anahisi kuwa tabia ya kubadili badili dawa za nywele zinachangia kuongeza matumizi yasiyo ya lazima ndani ya nyumba ukiachana na hatari za kiafya.

Kisa cha musa kimefanya uwepo ulazima wa kuwasikiliza wanaume ni kipi wanafikiria kuhusiana na nywele za wanawake. Unahitaji kuyafahamu nawazo yao? Usikose makala ijayo.

Enable Notifications OK No thanks