Madereva wa daladala, bodaboda watofautiana kujikinga dhidi ya virusi vya Corona

March 18, 2020 1:59 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi yao wasema hawana elimu ya kutosha kijikinga na ugonjwa huo ikiwemo kutumia vitakasa mikono na barakoa.
  • Wengine wasema wamechukua hatua ya kunawa mikono lakini changamoto ni mrundikano wa watu kwenye magari.
  • Waiomba Serikali iwapelekee elimu ya kujikinga mtaani.

Dar es Salaam. Wakati idadi ya wagonjwa wa ugonjwa wa virusi vya Corona ikiongezeka Tanzania, uelewa wa njia sahihi za kujikinga na ugonjwa huo miongoni mwa madereva wa daladala na bodaboda umekuwa tofauti huku wengine wakikiri kutokuelewa matumizi sahihi ya barakoa na tishu wakati kukohoa. 

Mpaka kufikia leo Tanzania imethibitisha kuwa na wagonjwa watatu wa virusi hivyo kutoka mmoja na kwanza aliyeripotiwa Machi 16, 2020. 

Takwimu za Shirika za Afya Ulimwenguni (WHO) za hadi jana (Machi 17, 2020) zinaeleza kuwa watu 179,112 wameambukizwa ugonjwa huo duniani huku waliofariki wakifikia 7,426. .

Wakiongea na Nukta ( www.nukta.co.tz) leo, baadhi ya madereva wa bodaboda kituo cha Victoria madereva wa daladala katika stendi ya Makumbusho jijini Dar es Salaam wamekiri kutokuchukua tahadhari zinazopendekezwa na wataalam wa afya.

Hussein Juma ambaye ni dereva wa bodaboda amesema amesikia virusi hivyo vinasambaa kwa kasi lakini yeye mwenye hatumii barakoa (mask) na vitakasa mikono (sanitizers) wakati akisafirisha abiria wake. 

“Nimepakia abiria watano tangu asubuhi lakini hakuna hata mmoja aliyevaa barakoa (kifunika uso/mask). Watu wenyewe hawana hata mpango nazo,” amesema Juma na kubainisha kuwa bado hajui kwa undani elimu ya kujikinga na ugonjwa huo.

Amesema yeye na baadhi ya madereva wenzake bado wanatumia leso kwa ajili ya kukohoa na kupigwa chafya, jambo linalowaweka katika hatari ya kupata ugonjwa huo ikiwa utazidi kusambaa katika maeneo ya umma.

Sababu nyingine inayomfanya dereva huyo asivae barakoa hasa anapokuwa katika mkusanyiko wa watu wengi ni kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo katika kipindi hiki ambacho kila mtu anahangaika kujilinda na maambukizi ya ugonjwa huo.  

“Zamani zilikuwa bei rahisi kwa sababu hazikuwa na dili. Sasa hivi ukitaka nyingi (boksi moja) zinaanzia Sh20,000 na wapo wengine wanaouza Sh80,000,” amesema Juma na kuongeza kuwa “sisi wa hali ya chini tutakufa kibabe.”

Hata baada ya tahadahri za kuchukua kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona kutolewa, Watanzania wanaendelea na shuguli kama kawaida bila ya kuchukua tahadhari. Picha| Rodgers George.

Wakati Juma akionyesha kuwa na uelewa mdogo wa ugonjwa huo na tahadhari zake, mwenzake Idrisa Rajabu amesema anafahamu kazi ya barakoa na vitakasa mikono lakini kutokana na uwezo wake anatumia maji kusafisha mikono yake. 

Amesema kwa sababu anaipenda familia yake, kila akirudi nyumbani anahakikisha ananawa mikono na kuepeka kuwagusa kwa sababu anakuwa amegusa na watu wengi katika shughuli zake.

Nukta imetembela  stendi ya daladala ya  Makumbusho na kukuta shughuli za usafiri zikiendelea kama kawaida na hakuna vifaa vya kunawia mikono licha ya kuwa imekuwa na muingiliano mkubwa wa watu.

Kondakta wa daladala inayofanya safari zake Makumbusho hadi Mawasiliano katika Halmshauri ya Ubungo, Bashiri Mgambo amesema abiria wenyewe wanaposwa kunawa mikono majumbani na wao kazi yao ni kuwasafirisha tu. 

“Kuweka maji kituoni ni vigumu. Bora sisi ambao abiria anapanda mmoja mmoja magari mengine abiria wanagombania.

“Wengine wanapitia dirishani sasa uwaambie wanawe kwanza utaweza?” amehoji Mgambo ambaye licha ya Serikali kuwataka wasijaze sana watu kwenye magari yao.

Mgambo ambaye amefanya kazi ya udereva kwa miaka 15 amesema waliofanikiwa kuchukua tahadhari kituoni hapo ni mama ntilie ambao wateja wakiingia na kutoka kwenye vibanda vyao lazima waoshe mikono.


Zinazohusiana 


Abiria wanaotumia kituo hicho watoa neno

Baadhi ya abiria walioongea na Nukta wamesema hilo ni janga la dunia na wanamuachia Mungu kwa sababu hali ya usafiri katika jiji hilo ni hatarishi kwa watu kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali.  

Anna Raphael(55) ambaye ni mjasiriamali wa mboga mboga na matunda maeneo ya Tabata amesema yeye janga hili anamuachia Mungu kwani hadi sasa hakuna analoweza kulifanya.

“Cha kwanza ni Mungu. Kwa nguvu zetu hatuwezi,” amesema Anna ambaye amesema anatufuata tahadhari zilizotolewa na Serikali za kunawa mikono lakini hawezi kununua barakoa.

Nini kifanyike kuongeza uelewa wa Corona

Madereva wa bodaboda na daladala wamesema ni vema Serikali ikaongeza elimu na hamasa ya njia sahihi za kujikinga na ugonjwa huo kwa sababu bado watu wengi wanapotoshwa na hawapati taarifa sahihi. 

“Madaktari wapite mtaani wasisubiri mpaka watu waende hospitali wakiwa wagonjwa,” amesema dereva wa bodaboda Seif Chilala wa kituo cha daladala Victoria.

Kwa upande wao, madereva wa daladala wamesema ikiwa Serikali inataka wasijaze abiria kwenye magari yao, waongee na wamiliki wa magari ili wapunguze mapato wanayowasilisha kila siku baada ya kazi ili kuwapunguzia mzigo.

“Kwa bosi unatakiwa kupeleka 100,000. Wengine ndiyo 90,000 kwa daladala na kwa muelewa kabisa ndiyo 80,000. Utaifikishaje hiyo pesa kama kwa tripu moja unapata Sh7,000? Ni lazima ujaze tu watu kwenye gari.

“Kabla hawajafikia hayo maamuzi, wawaelimishe mabosi kwanza,” ni kauli ya Mgambo.

Enable Notifications OK No thanks