Madeni kwa nchi maskini: ‘Kisu’ katikati ya moyo wa kujikwamua kiuchumi
- UN yaomba usitishaji kwa muda ulipaji wa madeni ya nchi maskini.
- Hiyo itazisaidia kujikwamua kutoka katika janga la Corona (Uviko-19).
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) António Guterres ametangaza mambo makuu manne ya kusaidia kukabiliana na madeni katika nchi maskini duniani ikiwemo usitishaji kwa muda ulipaji wa madeni wakati huu zinajikwamua kutoka katika janga la Corona (Uviko-19).
Guterres amesema “machungu yanayokumba nchi maskini kutokana na madeni yaliyozigubika ni sawa na kisu kinachochoma kwenye moyo wa dunia wa kujikwamua. Nchi haziwezi kujijenga upya vyema iwapo zitarudishwa nyuma na madeni.”
Katibu Mkuu huyo aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa 15 wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo na biashara (UNCTAD) nchini Barbados jana amesema anaunga mkono tangazo la hivi karibuni la Shirika la Fedha Duniani (IMF) la kutenga Dola za Marekani bilioni 650 kwenye mpango wa haki mahsusi za ukopaji (SDR).
Amesema fedha za SDR ambazo hazijatumika zielekezwe kwenye nchi zilizo hatarini zaidi na zinazohitaji fedha hizo zikiwemo zile za kipato cha kati.
“Pili tunafahamu kuwa nchi zinatwamishwa na gharama za ulipaji madeni, kwa hiyo tunahitaji kuongezwa muda zaidi wa mpango wa kundi la nchi 20 au G20 wa kusitisha ulipaji madeni hadi mwaka kesho. Mpango wao unasaidia kupunguza janga la madeni,” amesema Guterres.
Amesema kusitisha ulipaji madeni si jawabu linalotosheleza kwa nchi zote. Nchi zitahitaji unafuu wa madeni unaohusisha wadeni wa umma na wale wa kibinafsi.
Ili kufanikisha hilo Katibu Mkuu huyo amerejea wito wake wa kuangaliwa upya kwa mfumo wa kimataifa wa ukopeshaji ikiwemo kupunguza madeni hasa kwa nchi za kipato cha kati ili ziweze kuondoka katika mzunguko mbaya wa madeni.
Jambo la nne ni kuleta pamoja sekta ya umma na sekta binafsi ili kuendeleza mbinu bunifu za ufadhili za kuchochea kurejea kwa vitega uchumi vya sekta binafsi kama ilivyokuwa kabla ya janga la Uviko-19, hali ambayo itatochea kujikwamua kiuchumi.
Guterres amesema mambo hayo manne yatasaidia kuhakikisha hakuna serikali inalazimika kuchagua kati ya kulipa deni na kuhudumia wananchi wake.
Mkutano mkuu wa UNCTAD hufanyika kila baada ya miaka nne na mara ya mwisho UNCTAD14 ulifanyika jijini Nairobi nchini Kenya mwaka 2016.