Lissu arejea Tanzania, apokewa na maelfu ‘airport’

July 27, 2020 1:49 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Amewasili majira ya saa 8 mchana saa za Afrika Mashariki akitokea Ubelgiji kupitia Addis Ababa, Ethiopia.
  • Lissu alijeruhiwa vibaya Septemba 2017 baada ya kupigwa risasi 16 mwilini wakati akirejea nyumbani kwake jijini Dodoma.
  • Kwa kipindi chote hicho amekuwa akipatiwa matibabu ikiwemo kufanyiwa upasuaji kadhaa mwilini mwake nje ya nchi. 

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) upande wa Tanzania Bara Tundu Lissu amewasili nchini baada ya kukaa ughaibuni kwa takriban miaka mitatu alikokuwa akipatiwa matibabu kutokana kujeruhiwa vibaya na risasi mapema Septemba 2017.

Lissu, ambaye anawania nafasi ya urais ndani ya chama chake, amewasili majira ya saa 8 mchana saa za Afrika Mashariki akitokea Ubelgiji kupitia Addis Ababa, Ethiopia.

Maelfu ya wafuasi wa Chadema, viongozi na wanafamilia wa Lissu, walimpokea kiongozi huyo, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki kabla ya kuvuliwa ubunge na Bunge huku wakimwita “rais, rais, rais”. 

Lissu alijeruhiwa vibaya Septemba 2017 baada ya kupigwa risasi 16 mwilini wakati akirejea nyumbani kwake jijini Dodoma. Kwa kipindi chote hicho amekuwa akipatiwa matibabu ikiwemo kufanyiwa upasuaji kadhaa mwilini mwake.

Hadi sasa watuhumiwa waliomdhuru Lissu hawajakamatwa licha ya Rais John Magufuli kuagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina.

Mapema asubuhi wafuasi na viongozi mbalimbali wa Chadema walianza kukusanyika katika maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hatimaye kuruhusiwa na polisi kuingia mpaka aneo la tatu la abiria.


Soma zaidi:


Tangu jana alipoanza safari, Lissu amekuwa akitwiti kila hatua ya safari yake ikiwemo leo asubuhi.

“Sasa napanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia namba ET805 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole. Tukutane Dar es Salaam baada ya saa tatu hivi,” Lissu aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter mapema leo asubuhi.

Lissu amepokelewa na umati wa wafuasi wa Chadema licha ya onyo la polisi mwishoni mwa wiki kuwa “kusanyiko” hilo halikuwa halali.

Msemaji wa Chadema Tumaini Makene aliiambia Nukta mapema Jumatatu kuwa “hatuendi kufanya kusanyiko bali tunaenda kumpokea mpendwa wetu”.

Lissu ni miongoni mwa makada saba wa Chadema wanaowania kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika nafasi ya urais.

Wagombea hao wanasubiri chama hicho kumpitisha mgombea mmoja wapo atakayechuana na Rais Magufuli aliyeteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa asilimia 100 kugombea kwa kipindi cha pili na cha mwisho.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW