Kwa nini uzime simu unapokuwa kituo cha mafuta?
- Utaepusha mlipuko wakati mafuta yanawekwa kwenye gari.
- Watumiaji wa vituo wanasema hawana elimu hiyo.
- Serikali, wadau waombwa kutoa elimu kuhusu suala hilo.
Mwanza. Je, ushapita kwenye kituo cha mafuta na kuona tangazo au alama inayokutaka kuzima simu na injini ya gari? Au lile tangazo la kulipia mafuta kwa kutumia simu ya simu mkononi?
Alama hizo zimewekwa katika vituo vyote vya mafuta ikiwa ni tahadhari wanayopaswa kuchukua watumiaji wa vituo hivyo ili kujikinga na hatari yoyote inayoweza kutokea.
Jijini Mwanza, ongezeko la vyombo vya moto linaakisi ukubwa wa biashara ya uuzaji wa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.
Hata hivyo, uelewa wa alama hizo muhimu bado ni mdogo kwa madereva na hata wanaotoa huduma hiyo yaani wauzaji.
Nukta habari imeshuhudia madereva wanaofika katika baadhi ya vituo vya mafuta wengi hawazingatii alama hizo, magari hayazimwi na huku wengine wanaendelea kuzungumza na simu.
Ni tofauti kidogo kwa madereva wa bodaboda na bajaji. Wao walipofika kituoni walionekana kuzima vifaa vyao vya moto kisha zoezi la kujaziwa mafuta likaendelea.
Alama za tahadhari zinazopatikana katika vituo vya mafuta zimewekwa kuwaepusha watu na madhara ya kulipuka kwa mafuta ya petroli au dizeli. Picha| Mariam John.
Kwa nini kuzima simu wakati unaweka mafuta?
Alama hizo ambazo hubandikwa pembeni ya mashine za kujazia mafuta zina lengo moja tu la kutoa tahadhari ya kutokea kwa mlipuko endapo vifaa vya kielektroniki na umeme vitashika moto.
Kuzima injini ya gari na kutokutumia simu wakati unajaza mafuta kwenye gari ni njia mojawapo ya kuepuka madhara ya kulipuka kwa matanki ya mafuta.
Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo amesema kuwa alama hizo hazikuwekwa kama mapambo na kuwa zinatoa elimu kwa wananchi kuchukua tahadhari pindi wanapokuwa kituo cha mafuta kuepuka madhara ikiwemo vifo na majeraha.
Akizungumzia suala la kuzima simu, Kaguo amesema simu ina betri ambalo hutumia umeme hivyo wakati simu ikiita hutumia umeme mwingi ambao unaweza kusababisha mlipuko wakati mafuta yanajazwa kwenye gari.
Amesema matumizi ya simu yanaweza kusababisha mlipuko kutokana na mionzi inayotoka kwenye simu kukutana na hewa yenye petroli.
“Kwenye pampu za mafuta kuna mvuke ambao ukishabiiana na cheche kidogo zinaweza kuchangia umeme unaotoka kwenye simu kusababisha mulipuko,”amesema Kaguo.
“Wanapoingia kwenye kituo cha mafuta wazime simu zao ili kuepusha mulipuko unaoweza kutokea,” amesema Kaguo.
Pia malipo yanayofanyika kwa njia ya simu yafanyike mita chache kutoka ilipo mashine ya kujazia mafuta au ofisini ili kuepusha msuguano wa simu na pampu za mafuta.
Matumizi ya simu kwenye vituo vya mafuta siyo salama kwa sababu yanaweza kusababisha mlipuko. Picha| Mariam John.
Alama hizo bado ni kitendawili
Kukosekana kwa elimu kuhusu alama hiyo kumewafanya madereva na watoa huduma kutoweka kipaumbele katika suala hilo na kujiweka katika hatari ya kusababisha mlipuko.
Yakubu Mwaimamu ni dereva taxi jijini hapa, huku akiachia tabasamu ameeleza hana uelewa wa kutosha kuhusiana na suala hilo na kuwa anachojua anapofika hapo hutakiwa kuzima injini ili awekewe mafuta.
“Huenda wanahofia kuwa tukiwekewa mafuta wakati injini iko wazi kuna uwezekano wa dereva kutoroka bila kulipa fedha au huenda kuna tatizo ambalo huenda linaweza kuchangia mulipuko kwenye kituo,” amesema Eliesa Eliasi ambaye huenda katika vituo hivyo kupata huduma ya mafuta.
Latest