Hatari inayowakabili wauzaji, watumiaji mafuta ya vibaba Mwanza

November 28, 2023 7:36 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuharibikiwa kwa vyombo vya moto na kupoteza mali.
  • Ewura yatoa rai kwa wananchi kujiepusha na uuzaji wa mafuta kwa njia hiyo.
  • Yawataka wananchi kujenga vituo rasmi maeneo ya vijijini kwa kuwa masharti yamerahisishwa.

Mwanza. ‘Vituo vya mafuta bubu’, ndilo jina tunaloweza kuvipa vituo hivi ambavyo huuza mafuta ya vyombo vya moto kama dizeli na petroli hususan katika maeneo ya vijijini kwa kuyapima katika makopo ya ujazo tofauti na kuyahifadhi kwenye maguduria.

Ukosefu wa vituo vya mafuta rasmi katika maeneo ya vijijini ndio sababu ya uwepo wake ambapo licha ya  kuwa mkombozi kwa kusaidia upatikanaji wa huduma ya mafuta ni wazi kuwa watumiaji pamoja na wauzaji wapo katika hatari.

Miongoni mwa hatari hizo ni pamoja na kupoteza maisha au mali iwapo itatokea ajali ya moto na wakati mwingine vyombo vya moto huharibika kutokana na mafuta hayo kutokuwa na ubora unaotakiwa.

Makoja Robert, Mkazi wa Kijiji cha Misasi wilayani Misungwi ameiambia Nukta Habari kuwa anatumia mafuta hayo kwa sababu hakuna kituo cha mafuta rasmi kilichopo eneo hilo.

 “Siwezi kuzungumzia kuhusiana na ubora wake ingawa mimi naona ni sawa tu na ule wa kwenye vituo vya mafuta kwa kuwa vyombo vinawaka na tunavitumia,” anasema Robert.

Pamoja na kuwa ubora wa mafuta hayo si wa kuaminika kutokana na namna yanavyohifadhiwa, Robert amebainisha kuwa wakati mwingine huuziwa mafuta ya magendo ambayo yameibwa kwenye ujenzi wa miradi ya Serikali.

“Tunapata huduma lakini wakati mwingine ni hatari kwa wauzaji kwani baadhi yao sio waaminifu wanaiba mafuta lakini kwa wananchi ni hatari pale unaweza kutokea moto madhara makubwa yanaweza kujitokeza,” amesema Robert ambaye ni dereva wa pikipiki maarufu kama boda boda.

Mfanyabiashara wa mafuta akiwa ameyaweka karibu na njia kutafuta wateja katika Kijiji cha Misasi wilayani Misungwi. Picha l Mariam John/Nukta 

Mafuta ya vibaba bei juu zaidi

Tofauti na vituo vya mafuta rasmi ambavyo huuza bidhaa hiyo kwa bei elekezi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), wauzaji wa vituo bubu huuza kwa bei ya juu zaidi kwa kuwa hawasimamiwi au kudhibitiwa na mtu yoyote.

Mathalani katika Kijiji cha Misasi, wilayani Misungwi, lita moja ya petroli huuzwa kati ya Sh3,500 hadi Sh4,000 bei ambayo ni kubwa zaidi ukilinganisha na bei elekezi ya Sh3,419 kwenye vituo rasmi.

Mafuta ya dizeli ndio huuzwa juu zaidi kati ya Sh3,700 hadi 4,200 kwa lita, ilihali bei elekezi katika vituo rasmi kwa mwezi Novemba ni Sh 3,519.


Soma zaidi : Faida, hatari za uzazi njia ya upasuaji kwa wanawake Tanzania


Biashara hiyo si halali

Tito Kaguo, msemaji wa Ewura mkoa wa Mwanza amewataka wananchi kuacha kuuza mafuta kwa njia hiyo isiyo  halali ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo kuharibikiwa na vyombo vyao vya moto.

”mafuta yanayokaa juani kwa muda mrefu yanapoteza ubora na yanapowekwa kwenye chombo cha moto injini lazima iharibike,” amesema Kaguo.

Kaguo amesisitiza kuwa wauzaji wengi huuza kinyemela kwa kuwa hawana leseni zinazowatambulisha kufanya biashara hiyo  kwa sababu hawatambuliki kisheria hivyo ni vyema halmashauri zinazowasimamia zikaendelea kutoa elimu kwa wananchi kusitisha utoaji wa huduma hiyo.

Wauzaji wanasemaje?

Mmoja wa wauzaji wa mafuta ambaye hakupenda jina lake litajwe ameiambia Nukta Habari kuwa wanalazimika kuuza kwa bei ya juu zaidi ya elekezi kufidia gharama za usafiri ili wapate faida.

Muuzaji huyo ambaye amekiri kutokuwa na leseni ya kutoa huduma hiyo, kwa siku huuza kati ya lita 50 hadi 60 za mafuta, hivyo ndoto yake ni kujenga kituo rasmi cha mafuta, atakapopata mtaji wa kutosha.

“Ndoto yangu ni kujenga kituo cha mafuta kwenye eneo hili kwakuwa uhitaji ni mkubwa kwani kwa siku moja unaweza kuuza hata lita 50 hadi 60…Lengo letu ni kusogeza karibu huduma za mafuta kwa wananchi lakini pia tunayahifadhi ili kuhakikisha hatari yoyote haitokei kwenye jamii…,” amebainisha.

Hata hivyo, baadhi ya wanunuzi wa mafuta hayo, akiwemo Shelembi Manoni Mkazi wa Misasi wilayani Misungwi, wamelalamika kuhusiana na kuuziwa mafuta pungufu tofauti na vipimo rasmi kwa kuwa vyombo wanavyopimia mafuta hayo ni vidogo kuliko kiwango halisi.

 “Kipimo cha lita moja kimepunjwa, unakuta mafuta yake ni madogo tofauti na unayonunua kwenye kituo cha mafuta,” amebainisha Manoni.

Mafuta yakiwa kwenye chupa tayari kwenda kuuzwa katika maeneo ya vijijini. PichalMariam John/Nukta Africa

Uongozi wa kijiji wanena

Mwenyekiti wa Kijiji cha Misasi, Shija Ndamayape amekiri uwepo wa uuzaji mafuta kwenye vibaba kwenye kijiji chake ambao si halali licha ya kuwa hakuna madhara yaliyowahi kutokea.

“Miaka ya nyuma watumishi kutoka halmashauri walikuwa wanakuja kuzungumza na wauzaji hao kuwaonya wasifanye biashara hiyo kwakuwa sio halali na ni hatari lakini pale wanapoondoka na wao wanarudisha madumu yao kuendelea na biashara hiyo,” amesema Ndamayape

Itakumbukwa mwaka 2021 na 2022  moto uliosababishwa na mafuta ya petroli uliteketeza nyumba za wavuvi katika visiwa vya Nyamango na Kasalazi katika Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza.

Ingawa hakukuwa na madhara ya kwa binadamu, lakini moto huo uliteketeza mali zote za wavuvi zikiwemo vyavu za kuvulia dagaa na samaki na kusababisha hasara kwa wavuvi hao.


 Soma zaidi : Utafiti:Zaidi ya watanzania milioni sita hawatumii vyoo


Ewura watia neno

Kwa upande wake Meneja wa Ewura Kanda ya Ziwa George Mhina amebainisha kuwa kwa sasa wamejikita kutoa elimu na kuhimiza wananchi kujenga vituo vya mafuta rafiki vijijini.

Kwa mjibu wa Mhina kwa sasa utaratibu wa kuanzisha kituo cha mafuta maeneo ya vijijini umerahisishwa zaidi.

“ili uweze kujenga kituo cha mafuta maeneo ya mjini lazima uwe na hati kutoka halmashauri au jiji, kibali cha mazingira kutoka Baraza la Mazingira (Nemc), vile vile masharti ya ujenzi lazima uweke zege kwa kipimo kikubwa na paa la juu liwe zito tofauti na kijijini ambapo masharti hayo yameondolewa,” amesema Mhina.

Mhina ameongeza kuwa masharti mengine yaliyoondolewa ni ulazima wa kuwa na hati ya eneo ambapo sasa mhusika atatakiwa tu kuwa na mukhtasari wa kijiji.

“Hatuhitaji paa kama vituo vya mafuta vya mjini, , zege lake pia litakuwa la kawaida na kwamba wataalam walipokaa wakabaini kuwa ukiwa na kiasi cha Sh50 milioni unaweza ukajenga kituo cha mafuta kikawa na pampu mbili za petroli na diseli,” amebainisha Mhina.

Mifumo na ada za kuomba ujenzi wa vituo hivyo nao umerahishwa kwani muhitaji  anaweza akaomba kibali kupitia kwenye mfumo akiwa mahali popote.


Soma zaidi: Mwandishi wa Nukta Africa ashinda tuzo ya takwimu ya NBS 2023


Mikopo kwa wanaohitaji ujenzi

Aidha Kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya kuwakopesha wale wanaohitaji kujenga vituo vya mafuta maeneo ya vijijini.

Mwananchi ambaye hatamudu vigezo na masharti yaliyowekwa kwenye mwongozo wa uombaji wa leseni za ujenzi wa vituo vya mafuta kijijini vinavyotolewa na Rea unaweza ukakopeshwa kiasi hicho cha fedha na ukafanikiwa kujenga kituo.

Meneja huyo ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa hiyo ili wananchi waweze kuepuka kununua mafuta kwenye vidumu na kuepuka hatari na majanga yanayoweza kujitokeza.

Enable Notifications OK No thanks