Kutoka ombaomba Kariakoo hadi mfanyabiashara: Simulizi ya mjane anayepambana na maisha Dar

January 23, 2020 4:01 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Alipata msamaria mwema aliyemwanzishia biashara ya kuuza “ice cream” baada ya kumkuta akiomba Kariakoo
  • Biashara hiyo inamsaidia kutunza familia yake na kupambana na changamoto za kiuchumi za kila siku jijini hapa.
  • Baadhi ya wataalamu wa saikolojia wamesema uwezekano wa watu wenye historia kama Rehema kufanikiwa ni mkubwa na kwamba wasikate tamaa bali waendelee kupambana na maisha.

Dar es Salaam. Ilikuwa ni kawaida kumkuta pembezoni mwa barabara za Kariakoo mchana na usiku akiomba wasamaria wema wamsaidie chochote ili aweze kupata angalau chakula chake na cha watoto wake wawili. 

Mitaa hiyo ‘busy’ zaidi jijini Dar es Salaam, kwa kifupi, ndiyo ilikuwa nyumba yake mama huyu mjane, lije jua, ije mvua.

Rehema Hashim, maarufu kama ombaomba katika mitaa ya  Kariakoo, alijikuta akiingia katika maisha hayo Februari mwaka 2018 baada ya kumpoteza mumewe aliyekuwa akiishi naye Mwembe Yanga wilayani Temeke. 

Kwa takriban miaka miwili shughuli yake kuu ilikuwa ni kuwaomba wasamaria wema wampatie chochote asukume siku licha ya kuwa mwenye nguvu na afya njema. Kuishi mjini akiwa na wanawe wawili ilikuwa ni mzigo kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kupata angalau Sh100 ya kuwanunulia wanawe kitumbua. Mme wake alikuwa kila kitu. 

Kuomba tu haikuwa kazi lakini masaibu aliyokutana nayo katika mitaa hiyo imebaki kuwa kovu katika maisha yake kiasi cha kushindwa kunisimulia. 

“Kuna kimoja hicho sitakisahau kwenye maisha yangu…lakini kwa sasa siwezi kusema,” amesema Rehema huku akiinamisha uso chini na kupoteza furaha aliyekuwa nayo awali wakati tukianza mahojiano katika kituo cha daladala Makumbusho jijini Dar es Salaam.  

Changamoto nyingi zilijitokeza katika “shughuli” hiyo ya uombaji ikiwemo kugeuza maji ya kunywa pekee kuwa chakula kikuu  pamoja na watoto wake.

Ukosefu wa fedha ulichangia Rehema kumpoteza mtoto wake mmoja baada ya kuugua bila ya matibabu. Kutokana na hali yake ya ufukara, Rehema hakuwa na namna zaidi kushuhudia mtoto wake akipoteza maisha baada ya kuugua ugonjwa ambao haujui kutokana na kutompeleka hospitali.

Rehema akiwa kwenye harakati za kuuza ice cream za ukwaju katika Kituo cha Daladala Makumbusho jijini Dar es Salaam. Picha| Tulinagwe Malopa.

Hayo ndiyo maisha ya kila siku ya Rehema katikati ya Jiji

Novemba 15 mwaka jana akiwa katika “shughuli” yake ya kuombamba alimuomba chochote mtu aliyekuwa akipita moja ya mitaa ya Kariakoo. Tofauti na alivyozoea, mwanamume huyo alikataa kumpatia hela badala yake alimfanyia “surprise”. 

“Mama, japo sina kikubwa…sitakupa pesa. Twende nikajaribu kukutafutia kitu kitakachokuingizia japo kidogo cha kula,” msamaria huyo alimwambia Rehema.

Bila Rehema kujua alikokuwa akielekea, msamaria huyo alimshika mkono mpaka katika duka kubwa la kuuzia ice cream la Bakhresa Kariakoo lililopo kilomita chache kutoka mahali alipokutwa akiomba kila siku.

Wakati akisubiria kupewa msaada huo ambao mara nyingi alizoea kuwa ni fedha, alishtukia akipewa deli lililo na ice cream 20 na kuambiwa akatafute pesa ya kula pamoja na watoto wake.

Hapo ndipo maisha ya Rehema yalipobadilika kutoka hali ya kukosa chochote kwa siku mpaka sasa akiwa na uwezo wa kupata chakula cha kulisha familia yake.

Siku hiyo hiyo baada ya kupatiwa msaada huo, Rehema alianza biashara bila kujali nguo alizokuwa amevaa kwa wakati ule kuwa zingewakimbiza wateja. 

Hata hivyo, hakuanzia biashara hiyo katika eneo la “kazi” yake ya zamani badala yake alienda katika Kituo cha daladala Makumbusho huku madereva na abiria katika kituo hicho wakiwa wateja wake wakubwa.

Kwa kuwa alikuwa hajazoea kufanya biashara, ilikuwa ni vigumu kuingia mtaani kila asubuhi na kuanza kuuza bidhaa hizo zilizopata umaarufu zaidi jijini Dar es Salaam siku za hivi karibuni. 

“Madereva daladala ndio marafiki zangu wakubwa hapa kituoni na ndio wanaoniungisha kwa kiasi kikubwa. Ni moja ya vitu vinavyonitia moyo kuendelea,” Rehema ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz).


Zinazohusiana: 


Hivi sasa Rehema ni miongoni mwa wafanyabiashara wadogo maarufu  wa ice cream za ukwaju katika kituo cha mabasi cha Makumbusho.

Biashara hiyo inamsaidia kutunza familia yake na kupambana na changamoto za kiuchumi za kila siku jijini hapa.

Kuingia katika biashara ndogondogo kulimfanya Rehema abadili maisha yake kutoka kulala na njaa mpaka sasa ambapo anaweza kuingiza angalau Sh10,000 kwa siku. Licha ya kuwa kwa wengine kiasi hicho kinaweza kuwa ni fedha kidogo, kwa sasa anaweza kulisha watoto wake pamoja na kupata mahitaji yote muhimu kwa siku ikiwemo kupanga chumba anachoishi na Mwananyamala A.

“Siku moja niliwaza na kusema mimi na watoto wangu wawili ni wa kufa tu. Watoto walikuwa wanalia njaa na sijui natoa wapi chakula cha kuwapa. Namshukuru sana yule baba amebadilisha maisha yangu kwa kiasi kikubwa,” amesema Rehema.

Rehema mwenye umri wa miaka 37 hakuwahi kuwaza kama siku moja angepata mtu anayeweza kumwinua na kumfikisha mahali alipo kwa sasa kwa kuwa anaona tumaini la maisha kuliko hapo awali alipojiona dhaifu.

“Nikitathmini mahali nilipokuwa na sasa napata majibu kwamba kumbe maisha yanaweza kubadilika kwa mtu yoyote kwani sikuwahi kuwaza kama siku moja ningefika hapa nilipo,” amesema Rehema.

Anatamani siku moja amwone tena msamaria yule amshukuru kwa wema wake lakini kwa sasa hawezi tena kwa kuwa wakati huo hakuwa na simu na wala hakuchukua namba ya simu. 

Kibaya zaidi ni kwamba hata hakuuliza jina lake kwa kuwa baada ya kukamilisha msaada huo alitokomea na kumtakia kheri. 

Biashara hiyo inamsaidia kutunza familia yake na kupambana na changamoto za kiuchumi. Picha| Tulinagwe Malopa.

Kutokana na kupenda biashara hiyo na kutamani kuendelea zaidi, hivi sasa Rehema ana uwezo wa kuchukua deli zima la ice cream za Azam lenye uwezo wa kujaza ice cream 50 kila moja akiuza kwa Sh500. Hii ina maana kuwa iwapo biashara itamnyookea, Rehema ana uwezo wa kuuza hadi Sh25,000 kwa siku. 

Amesema mara nyingi kwa siku ana uwezo wa kuuza karibu robo tatu ya deli hilo au kumaliza mzigo kabisa kutokana na jitihada alizonazo katika kusambaza bidhaa hizo na urafiki wa karibu anaojenga kwa wateja wake mpaka kuwashawishi kununua.

Changamoto anayopata katika biashara hiyo ni pamoja na mzigo kutokuisha baadhi ya siku zenye mvua na kimlazimu kuzigawa bure kwa marafiki wa jirani kutokana na kukosa  jokofu kuhifadhi zisiharibike. Iwapo angekua na jokofu, huenda hasara hiyo angeiepuka.

Rehema anaamini biashara hiyo itamfikisha mbali zaidi siku zijazo ikiwemo kufanikisha ndoto yake ya kujenga nyumba ya vyumba viwili kwa ajili yake na watoto wake ili kukwepa gharama anazoingia kwa ajili ya kulipa kodi.

Rehema anawasihi wanawake kujishughulisha na biashara ndogondogo bila kutegemea waume zao tu kuleta chakula nyumbani kama alivyokuwa akifanya yeye kipindi cha uhai wa mumewe.

Baadhi ya wataalamu wa saikolojia wameiambia Nukta kuwa uwezekano wa watu wenye historia kama Rehema kufanikiwa ni mkubwa na kwamba wasikate tamaa bali waendelee kupambana na maisha.

Kutokana simulizi ya Rehema, Mwanasaikolojia kutoka Shirika la Jamii Live, Aman Mwaipaja amesema kwamba uwezekano wa mama huyo kufanikiwa zaidi ni mkubwa kwa kuwa ameonesha utayari wa kubadilika kutoka mazingira magumu kwenda kwenye hali nzuri zaidi.

“Sio kazi rahisi sana kumtoa mtu kwenye ulimwengu wa kuwa ombaomba na kuwa kwenye ulimwengu mwingine wa pili kutokana na namna akili ilivyojizoesha,” amesema Aman.

Amesema ni watu wachache wenye tabia ya kuombaomba au kujiuza huwa ni vigumu kuondoka katika mazingira hayo hivyo inapaswa watu wajitoe kuwasaidia kisaikolojia na kifedha ili waweze kunyanyuka kimaisha kama Rehema.

Enable Notifications OK No thanks