INEC, Serikali, vyama vya siasa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi
- Chama ambacho hakitasaini kanuni hizo za maadili hakitashiriki uchaguzi.
- Kanuni hizo zinapaswa kusainiwa na kila chama cha siasa na kila mgombea kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi.
Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama vya siasa na Serikali wanatarajiwa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi yatakayotumika kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kesho Aprili 12, 2025.
Mkurugenzi wa uchaguzi wa INEC hiyo Kailima Ramadhan aliyekuwa akizungumza leo Aprili 11, 2025 na vyombo vya habari jijini Dodoma amesema chama cha siasa ambacho hakitasaini maadili hayo hakitaruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo.
Hata hivyo, Ramadhan amebainisha kuwa maadili hayo yameandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 162 (1), (2) na (3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024.
Kwa mujibu wa Ramadhan vifungu vinaitaka INEC baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali kuandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali kanuni za maadili ya uchaguzi zitakazoainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni za uchaguzi, uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake.
Ramadhan ameongeza kuwa kifungu hicho kinaelekeza kuwa kanuni za maadili zitasainiwa na kila chama cha siasa na kila mgombea kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi, Serikali na INEC na zitapaswa kuzingatiwa na wahusika wote waliosaini.
Ameongeza kuwa tayari maandalizi yote muhimu yameshafanyika na mawasiliano yameshafanyika baina ya INEC, Serikali na vyama vya siasa. na kwamba kinachosubiriwa ni kuwasili kwa wahusika jijini Dodoma kwa ajili ya kusaini kanuni hizo za maadili kesho.
Aidha, amesisitiza kuwa zoezi hili litafanyika kwa siku moja tu, na kwamba baada ya hapo chama ambacho hakijasaini kanuni hizo za maadili hakitapata fursa ya kusimamisha wagombea.
Katika hatua nyingine, Ramadhan amefafafanua kuwa, INEC inaendelea vizuri na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kwamba tayari imekamilisha awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Utiaji saini huo unakuja wakati ambao Chama cha Demokrasia na Maendeleao (Chadema) kupitia mwenyekiti wake Tundu Lissu wametangaza kususia uchaguzi iwapo ajenda yao mageuzi haitasikilizwa.
Ingawa mpaka sasa mwenyekiti huyo wa Chadema ameshikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukamatwa katika ziara yake ya kuhamasisha ajenda ya chama hicho ya hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi.
Sanjari na hilo Ramadhan amewambia waandishi maandalizi ya uboreshaji wa daftari kwa awamu ya pili yanaendelea ambapo tume inatarajiwa kutangaza ratiba ya zoezi hilo hivi karibuni.
Uboreshaji huo wa awamu ya pili kulingana na Ramadhan yamezingatia kifungu cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 ambacho kinaipa tume jukumu la kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili.
Tayari INEC imekamilisha awamu ya kwanza ya uboreshaji wa daftari ambao ulifanyika nchi nzima kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 hadi tarehe 25 Machi, 2025.
Latest



