Kutana na mwanamke mjasiriamali anayeboresha maisha ya watoto, wanawake Tanzania
- Ni Flora Lauwo, mkazi wa Mwanza na mjasiriamali wa masuala ya urembo.
- Amekuwa mstari wa mbele kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake Kanda ya Ziwa.
- Historia aliyopitia ndiyo imemfanya awe mchapakazi na jasiri kwenye jamii.
Mwanza. “Huenda ningesoma ningekuwa mtu mkubwa na ningeweza kuisaidia jamii hususani watoto wanaonyanyaswa na wazazi au walezi wao, “
Ni maneno ya Flora Lauwo, mwanamke jasiri ambaye anafanya kazi ya ujasiriamali wa masuala ya urembo na kuisadia jamii katika nyanja mbalimbali hususan katika kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Mama huyo wa watoto wawili alizaliwa miaka 40 iliyopita Rombo wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro ambapo kwa sasa anaishi Mtaa wa Lumala jijini Mwanza, eneo ambalo limemfanya kuwa maarufu ndani na nje ya mji huo kutokana na shughuli za kijamii anazozifanya.
Chuma kinachopitishwa kwenye moto mkali ndicho chuma imara zaidi, maisha ya utotoni mithiri ya kambi ya jeshi ndiyo yaliyomfanya kuwa imara kwenye utafutaji na kuitetea jamii yake.
Haikua kazi rahisi kuvuka vigingi, mbigiri na kila aina ya miiba aliikanyaga kuyafikia mafanikio ambayo hivi sasa anajivunia kuwa mwanamke jasiri mwongoza njia.
“Niliajiliwa kazi ya saluni ambayo nililipwa sh30,000 kwa mwezi, fedha ambayo ilikuwa ndogo ukizingatia tayari nilikuwa nimeondoka nyumbani nimepanga kwangu na ni mdada nahitaji kuvaa vizuri na vitu vizuri,” anasema Flora.
Kazi hiyo ilimuimarisha hivyo kulazimika kuhama kutoka mkoani Arusha alikokuwa ameajiliwa na kwenda Mwanza kwa ajili ya shughuli hiyo hiyo ambayo hapo baadaye aliweza kusimama mwenyewe kwa kuanzisha ofisi yake ya saluni ya kike, duka la urembo pamoja na nguo za maharusi bidhaa ambazo analazimika kizifuata nchini China
Licha ya ujasiri wake wa kuthubutu, Flora anafahamika zaidi jijini hapa kupambana na ukatili wa kijinsia hasa unaowapata wanawake. Njia anayotumia ni kutoa elimu na kuwasaidia waathirika warejee katika maisha ya kawaida.
Kuwaona watoto wakiwa na furaha wakiwa mbali na unyanyasaji, ndiyo mafanikio ya Flora. Picha| Mariam John.
Historia yamfanya kuwa alivyo
Akiwa na umri wa miaka 10 ndoto yake ilikuwa ni kuja kuwa askari, hii ni baada ya kuishi maisha ya manyanyaso aliyokuwa akifanyiwa katika familia na mtu aliyepaswa kumlinda na kumuendeleza kifikra.
Licha ya kuzaliwa mtoto wa mwisho kwenye familia ya mzee Lauwo malezi yake yalikuwa tofauti na watoto wengine ambao wazazi wao walikuwa wakiwadekeza na kuwapatia zawadi kedekede.
Ndoto za kuwa askari ziligonga mwamba baada ya kuishia kidato cha pili kutokana na mazingira aliyokuwa akiishi nyumbani kuwa magumu.
Hapo ndipo dhamira ya kujitegemea ilitawala nafsi ya Flora ambaye ni Mkurugenzi wa taasisi ya Nitetee Foundation, jambo ambalo hadi sasa anajivunia kuwa mwanamke mchakalikaji.
Zinazohusiana:
- Kutana na Aneth David mwanasayansi anayechipukia Tanzania
- Rahma Bajun: Mjasiriamali anayetamba kimataifa
- Esther Mndeme: Muongozaji aliyewashangaza wengi tuzo za filamu 2019
Aingia mtaani kusaka mali
“Kaka zangu na dada zangu wote hawakuwepo nyumbani, mama naye aliondoka na kuniacha nyumbani mwenyewe, kazi zote zilikuwa zangu na sikuruhusiwa kwenda shule kabla ya kulisha ng’ombe majani, ” anasema Flora.
Licha ya kuwa na ufaulu mzuri, aliweza kusoma kwa miaka miwili tu akaamua kuacha shule na kuamua kuingia mtaani.
“Halikuwa jambo rahisi ila nilishawishiwa na rafiki yangu kuwa tukitoroka kwenda huko tutafanya biashara na kuwa matajiri, ” Flora anasema wazo hilo aliona ni nzuri kuliko kuendelea kunyanyaswa na baba yake.
Hata hivyo, safari hiyo haikufua dafu baadaye alirudi nyumbani kuendelea na maisha lakini pia haikumfanya ashindwe kujishughulisha na biashara ndogo ndogo za kuuza karanga.
Shauku ya kutaka kufanikiwa kimaisha na kuwasaidia wengine wasipitie mateso aliyopitia akiwa mdogo ilizidi kumsumbua na kumfanya atafute ilipo hatma ya ndoto yake. Kwa sasa, ameamua kuwa mwanaharakati wa masuala ya kijinsia ikiwa ni hatua ya kufuta kumbukumbu mbaya alizopitia akiwa mtoto.
“Sipenda kuona mtoto akinyanyaswa na akifanyiwa ukatili wa aina yoyote, natamani kumsaidia,” anasema.
Nyumbani kwa Flora ni jukwaa la kuwapatia matumaini watoto yatima na waliopitia ukatili ili kutimiza ndoto zao. Picha| Mariam John.
Nyumbani kwa Flora ambaye pia ni mmiliki wa chuo cha urembo na mapambo cha NIFO jijini hapa, huwezi kumkuta peke yake na familia yake bali kundi kubwa la watoto anaowalea ambao wamepitia madhira mbalimbali kwenye maisha.
Lakini si watoto pekee, bali vijana na watu wazima wengi wameponywa mioyo, afya za miili na akili kupitia mikono ya mwanamke huyu ikiwemo familia ambayo watu wake saba wamekatwa miguu kutokana na ugonjwa wa ajabu
Kuwafungua watu vifungo vya tabu za maisha anasema ndiyo kazi inayompa amani ya roho japo si ya kipato lakini changamoto anazopitia zinamuongezea imani kwa mola wake.
Ingawa kinachomuumiza ni pale wema wake unapogeuka kuwa mtuhumiwa hasa wanaotekeleza vitendo vya ukatili kumuwinda na kumfungulia kesi ili kuhakikisha anaachana kazi anayofanya.
“Nina kesi, tena kesi kubwa nadaiwa zaidi ya Sh600 milioni nikituhumiwa kumdhalilisha mtu baada ya kufanya wema wa kusaidia mhanga aliyeungua na moto, ” anasema mama huyo.
Flora anadhihirisha kuwa mwanamke ni jeshi kamili akielimika ni mlezi na mkombozi wa jamii nzima.