Kuhoji, ufafanuzi kunavyoimarisha misingi ya tiba bora hospitalini
- Mgonjwa mzuri ni yule mwenye kiu ya kufahamu undani wa tatizo lake kwa daktari.
- Kuhoji kunasaidia kupata tiba bora inayoendana na hali ya mgonjwa.
- Pia kunaimarisha mahusiano kati ya daktari na mgonjwa.
“Hivi unaanzaje kumuuliza daktari, mfamasia au nesi kuhusu dawa au tiba au ugonjwa? Si ataona unamdharau? Kwanza nahisi huwa hawapendi utashangaa anakuambia ina maana unanidharau au?”
Hayo ni maneo niliyoyasikia hivi karibuni katika kijiwe changu cha supu ya kongoro ambayo hunisaidia kumairisha afya yangu hasa maungio ya mwili wangu.
Ni mteja kama mimi, lakini akaikuna roho yangu na masikio yangu kwa kauli hii. Nikakata shauri kwamba acha nimsikilize hoja yake kisha ndio nijaribu kumuelewesha.
Sasa tukaanza kuongea kwa mapana kidogo, sikujitambulisha kama daktari hadi pale tulipoelekea mwisho wa maongezi na yeye kunielewa. Siku hii sikulipia supu yangu, nililipiwa na rafiki yangu mpya.
Dhana imejengeka katika jamii yetu ya kwamba mtoa huduma ya afya hapaswi kuhojiwa. Na kwamba unapopewa huduma hauhitaji kuomba ufafanuzi za huduma unayopata. Dhana hii siyo sahihi.
Kupitia fikra hii isiyo na mashiko, imesababisha watu kunywa dawa ambazo zimewapa athari kutokana na kutouliza au kuomba ufafanuzi kama zinaweza chochea mzio (allergy) au haziendani na hali fulani.
Kuhoji na Ufafanuzi ni misingi mikubwa ya wewe kupewa huduma bora kila ufikapo hospitali na ni haki yako ya msingi. Tabia hii ni utamaduni unaonekana mpya lakini ni muhimu kwa sababu ni utamaduni ambao tulipaswa kuwa nao wakati wote.
Kuomba ufafanuzi wa aina ya matibabu unayopewa, dawa ulizoandikiwa, maelezo ya tatizo lako pia sababu ya aina ya kipimo unachokipata ni sehemu chache tu za kwanini ufafanuzi na kuhoji vitu hivi ni haki yako ya msingi.
Ni yako kuambiwa na daktari tiba anayokupatia kama inakufaa na tahadhari unazopaswa kuchukua. Picha|Everyday Health.
Mtaalamu wa afya anaekuhudumia kwa wakati huo ana wajibu wa kukuelekeza na kukupa ufafanuzi wa msingi wa huduma unayopatiwa pale unapoomba kufanyiwa hivo.
Utaratibu huu hukuwezesha mgonjwa kuwa na ujuzi mpana wa tiba unayopatiwa na kukupa nafasi ya kutumia kwa usahihi kabisa.
Unapopatiwa dawa au kuandikiwa vipimo, kwa utaratibu na staha muombe daktari akueleze na kufafanulia kwa upole na ukarimu kile kilicho mbele yako.
Katika maelezo yako omba pia utambue iwapo kuna tahadhari unapaswa uchukue kabla ya vipimo, tiba au dawa. Pia omba ufafanuzi juu ya aina za tiba zilizo wazi juu ya tatizo lako. Iwapo unahitaji ufafanuzi juu ya majibu ya vipimo vyako vya kimaabara, muombe daktari akuelezee kinagaubaga ili uwe kwenye sehemu bora ya ufahamu yakinifu wa tatizo lako.
Zinazohusiana:
- Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi matibabu ya figo Muhimbili
- MOI kuanza upasuaji wa ubongo kwa teknolojia ya kisasa
- Tahadhari za kuchukua kuepuka uume kuvunjika
Kuhoji na kuomba fafanuzi kuambatane na utumiaji wa kauli nzuri na ya upole yenye heshima kwa pande zote mbili. Matumizi ya kauli nzuri huepusha makwazo na kutotia doa uhusiano baina ya mgonjwa na anaemuhudumia.
Ifahamike wahudumu wa afya wana vifungu vyao vya maadili na weledi katika kazi yao. Lakini wao pia ni binadamu wenye hisia na mihemko kama binadamu wengine. Hivo basi kauli yako itakapoakisi kutothamini au kuheshimu taaluma yake, humtengenezea mwanya wa kutokupa ushirikiano mzuri.
Turejee ya kwamba wahudumu wa afya ni marafiki. Hauna budi kuwa wazi na huru kumueleza na kumuomba akupate maelezo kinagaubaga kuhusu hali ulionayo na huduma unayoipata.
Mgonjwa mzuri ni yule mwenye kiu ya kufahamu undani wa tatizo na mwenye nia ya kujua msingi wa huduma anayopewa na daktari wake. Kupitia mfumo huu, huduma itakua thabiti na madhubuti kabisa.
Katika yote, nawasihi tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona tukizingatia kwa makini maelezo ya kitaalamu katika kujikinga na ugonjwa huo.
Nipo!
Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.
Latest