Kiatu chako, utambulisho wako
- Kiatu siyo tu kwa ajili ya kukanyagia ardhi, ni sehemu ya unadhifu wako.
- Chagua kiatu kulingana na eneo unaloenda na pia zingatia afya yako.
- Pia kiatu kizuri siyo kile kinachombana mtumiaji.
Dar es Salaam. Zipo video nyingi mtandaoni za kina dada waliovalia viatu virefu na wanachechemea kutembea navyo. Tabu yote hiyo ya nini?
Urembo siyo tu ni kuvutia bali kuendana na vitu vyote ulivyovaa. Nguo ikae mahala pake, nywele ziwe mahala pake vivyo hivyo harufu, tabasamu, na hata tembea yako pia.
Katika unadhifu, utawezaje kuwa na amani ikiwa chaguo lako la kiatu siyo sahihi?
Saikolojia inasema, unaweza kubashiri umaridadi wa mtu kwa kuangalia kiatu chake tu. Siyo mimi, ni saikolojia.
Chuo Kikuu cha Utafiti cha Kansas cha nchini Marekani kimewahi kufanya utafiti wa suala hili na matokeo ya utafiti huo ni kuwa, kiatu kinaeleza mambo mengi kuhusu mvaaji ikiwemo usafi wake.
Ili kutokufanya kiatu chako kikuharibie muonekano wako, hizi ni baadhi ya dondoo unazoweza kuziangazia.
Kiatu kinachokutosha vizuri kitaonngeza umaridadi katika kutembea kwako na pia kujiamini. Picha| Stocky.
Vaa kiatu kinachokutosha
Kila siku unatumia miguu yako kutembea hivyo uzito wa mwili wako wote, unaishia kwenye miguu hiyo. Kuvaa kiatu ambacho hakikutoshi ama hakikukai vizuri inaweza kukupa tafrani ya namna fulani ikiwemo miguu kuuma na hata kuchubuka kutokana na kubanwa.
Tovuti ya Fair View imeandika, “kiatu sahihi kitailinda miguu yako lakini kiatu ambacho siyo sahihi kitasababisha matatizo zaidi.”
Inashauriwa kununua kiatu ambacho kinaendana na umbo la mguu wako. Baadhi hutaja tu namba ya kiatu lakini wanashindwa kuzingatia umbo la miguu yao na hivyo kupata viatu vinavyowabana.
“Usinunue kiatu kutokana na saizi yake peke yake. Jaribisha viatu kwani saizi zinatofautiana kulingana na makampuni yanayotengeneza viatu,” Fair View imeandika.
Vaa kiatu kutokana na sehemu unayoenda
Kuna viatu kwa ajili ya kila sehemu, hapo wabunifu hakika wametufaa. Vipo viatu vya ufukweni, viatu kwa ajili ya “kutoka out” na hadi viatu kwa ajili ya kwenda kuwasalimu wakwe. Kila mtu ana uwanda mpana sana wa kuchagua.
Tunaoongelea kuchagua kiatu sahihi katika sehemu sahihi ni muhimu kwani itakusaidia kuendana na eneo hilo.
Mathalan, kuvalia viatu vya mchuchumio unapoenda kutembelea ufukweni, huenda lisiwe jambo la busara kufanya kwani hakika vitakupa changamoto kuvitembelea na hivyo kukulazimu kuvibeba.
Unapovalia viatu vya ofisi ofisini, ni jambo zuri lakini siyo kuvivaa viatu hivyo kwa ajili ya kukimbia.
Kuna kiatu kwa ajili ya kila sehemu. Fanya uchaguzi sahihi. Picha| Okay Africa.
Vaa kiatu kulingana na afya yako
Afya ina mawanda mapana sana. Kuanzia afya ya mwili na mambo mengine ikiwemo akili na ngozi. Baadhi ya watu afya yao ya miguu ina changamoto na hivyo miguu yao hutoa harufu mbaya.
Mtaalam wa afya kutoka kituo cha afya cha TMH kilichopo Mwenge jijini Dar es Salaam, Dk Isaac Maro amewahi kuiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kiatu sahihi kinaweza kuwa msaada kwa watu wenye changamoto mbalimbali ikiwemo kiharusi na magonjwa mengine.
Hivyo chagua kiatu ambacho kitaendana na hali ya afya yako na pia kulingana na shughuli zako ikiwemo umbali utakaovitembelea viatu hivyo na kazi yake.
Pamoja na hayo yote, unapovaa kiatu, zingatia kama vinaendana na mavazi yako. Mfano, viatu vya ofisi hupendeza zaidi vinapovaliwa na mavazi ya kiofisi huku kwa mavazi ya kawaida (casual) yakiwa na machaguo mengi kwa ajili ya kuendana nayo.
Ni pamoja na raba, viatu vya wazi (sandals) mabuti na viatu vingine. Kiatu chako, siyo tu cha kukanyagia ardhi, ni utambulisho wako pia kwa watu wasioweza kukutazama usoni.
Latest
