Siku ya Wapendanao: Zawadi zinazomfaa mpenzi wako wa kiume

February 14, 2022 3:02 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Hakikisha unasoma alama za nyakati ili zawadi yako itumike.
  • Wanaume wengi hupenda zawadi zinazodumu kwa muda mrefu.
  • Kama mfuko hauruhusu, muda wako ni zawadi tosha.

Sababu kubwa ya baadhi ya wanawake kutokuwapatia zawadi wanaume ni ugumu wa kuchagua zawadi ya mwanaume kwa sababu hupata changamoto ya kuchagua zawadi ambayo mtu mwanaume ataifurahie.

Sababu nyingine ni gharama ya vitu vya wanaume. Wakati Sh50,000 ikitosha kununua viwalo vyote vya mwanamke, pesa hiyo huenda ikaishia kwenye suruali au shati kwa upande wa wanaume, labda uende Kariakoo.

Jambo hilo huwafanya wasichana wengi wakimbilie kununua nguo za ndani (boxer) na leso, kitu ambacho baadhi ya wanaume huchukizwa nacho na kuhoji nafasi zao kwa wapenzi wao.

Makala haya yatakusaidia kuondoa changamoto hiyo walau kwa kiasi chake.

Vifuatavyo ni baadhi ya vitu ambavyo mwanaume yeyote atafurahia kama zawadi katika siku ya wapendanao na hata siku yoyote ile.

Saa ya mkononi

Wanaume ni watu wa majukumu. Kila siku walio wengi kati yao watakuwa kwenye shughuli za kutafuta kipato hivyo kwenda na wakati ni kati ya vipaumbele vya wengi.

Kama haujafahamu zawadi kwa ajili ya mpenzi wako wa kiume, unaweza kwenda kwenye maduka ya saa na kuchagua ile unayoona itampendeza.

Kuwa Makini na rangi, wanaume wengi hawapendi rangi za kuwaka hivyo saa ya kahawia, nyeusi, silver na dhahabu ni kati ya machaguo maarufu kwa ajili ya wanaume.

Kama mpenzi wako anaweza kugharamia deti yako na mavazi yako, siyo mbaya ukatenga walau Sh100,000 au zaidi kumnunulia kitu atakachokuwa akitazama kila mara na kukukumbuka.

Mpatie mpenzi wako zawadi atakayoikumbuka. Picha| Daily Express.

Kiatu cha mtoko

Kati ya vitu ambavyo wanaume wanafurahia ni kuwa na kiatu kizuri. Kiwe cha ofisini, cha mitoko ya kawaida na hata cha michezo. Kama unajua saizi yake, miundo anayoifurahia, zawadi hii ni ya kukimbilia. Uzuri ni kuwa, kiatu huja na maboksi ya kupendeza hivyo hautopata shida sana kuandaa zawadi hiyo.

Kama unamfahamu vizuri, ni vyema kuangalia akiba yake ya viatu na kuona kipi kimeshaisha upande na umsasishe kwa kipya.

Inategemea na wewe ulipozoea kununua zawadi za mpenzi wako lakini ukiwa na walau Sh100,000 una uhakika wa kupata kiatu kizuri kwa ajili ya mpenzi wako.

Ahana na boksa au leso.

Jeans nyeusi, bluu 

Jeans ni kati ya vazi maarufu miongoni mwa wanaume kwani halibagui nguo ya kuendana nayo. Wapo wanaovaa jeans na shati za mikono mirefu, tisheti za shingo ya duara na hata tisheti za kola.

Unaweza kumnunulia jeans na t-shirt nyeupe na kisha uone tabasamu lake litakavyoongezeka wakati akifungua zawadi hiyo. Kuwa na uhakika wa saizi ya kiuno chake na pia ununue jeans ya maana na siyo ilimradi jeans.

Unaweza kupata suruali nzuri na imara ya jeans ukiwa na Sh45,000 na kuendelea.

Ni muda wa kuachana na mikanda na waleti za maandishi ya mahaba.


Soma zaidi


Seti ya manukato

Kuna “meme” niliiona mtandaoni ikisema “Wanaume wanaonukia Mungu awabariki” ilinifikirisha sana. 

Kwa kazi za wanaume baadhi nguvu inahitajika, ananyanyua hiki, atatembea kwenda hapa na mambo mengine kama hayo. Asipokuwa na manukato mazuri, lazima harufu ya jasho itaanza kuwafikia watu anaopita karibu yao.

Kama mpenzi wake, ni jambo la muhimu kumsaidia kuwa huru popote alipo. Unaweza kumnunulia seti ya manukato kulingana na kiwango chake cha kutokwa na jasho.

Mfano, kwa anayetokwa na jasho jingi, unaweza kumnunulia “antiperspirant” ili kupunguza kiwango cha jasho. Kwa ambaye jasho lake ni la kawaida, “deodorant” itamfaa huku ukiisindikia za pafymu inayokaa walau kwa saa 24 kwenye nguo.

Zawadi zingine ni muda wako, chakula kizuri au chupa ya mvinyo ambayo anaifurahia zaidi. Sasa hauna sababu ya kupeleka mkanda, boxer na vitambaa vya jasho kwa mtu unayempenda. 

Enable Notifications OK No thanks