Faida Vodacom Tanzania yapaa mara mbili hadi Sh118 bilioni miezi sita 2026
- Imeongezeka zaidi ya mara mbili ndani ya mwaka mmoja kutoka Sh41.7 bilioni ziliripotiwa nusu mwaka iliyoishia Septemba 2025.
- Ongezeko hilo la faida lilichochewa zaidi na ukuaji wa mapato ya M-Pesa na huduma za data.
Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC imeweka historia mpya baada ya kuripoti faida baada ya kodi ya Sh117.8 bilioni katika nusu mwaka inayoishia Septemba 2026, kiasi cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa na kampuni hiyo ndani ya miezi sita.
Faida hiyo imeongezeka mara mbili ndani ya mwaka mmoja kutoka Sh41.7 bilioni zilizorekodiwa katika kipindi sawa na hicho mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 182.7, ikichochewa zaidi ukuaji wa mapato ya huduma za data na M-Pesa.
Ripoti ya awali ya kifedha katika kipindi cha nusu mwaka kinachoishia Septemba 30, 2026 mapato ya Vodacom Tanzania PLC yaliongezeka kwa asilimia 19 na kufikia takriban Sh1.08 trilioni kutoka Sh905.33 bilioni iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho kilichoishia Septemba 2025.
Mapato ya kampuni hiyo yenye zaidi ya wateja milioni 29 sokoni, yanaonyesha kuendelea kuimarika kwa kampuni hiyo kubwa ya mawasiliano nchini iliyokuwa ikiripoti hasara miaka mitatu liyopita.
M-Pesa, data zatunisha mapato
Ukuaji wa mapato ya Vodacom Tanzania PLC umeenda sambamba na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na huduma zake.
Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, mapato hayo yameendelea kuwa injini kuu ya ukuaji wa biashara ya kampuni hiyo, ambayo ni kampuni pekee ya mawasiliano iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mapato yatokanayo na huduma yaliongezeka kwa asilimia 20.8 na kufikia takriban Sh1.07 trilioni kutoka Sh883.9 bilioni zilizorekodiwa mwaka uliopita, yakichangia asilimia 99 ya mapato yote ya kampuni hiyo.
Vodacom inaeleza kuwa ukuaji huo ulisukumwa zaidi na ongezeko la matumizi ya huduma za data na M-Pesa ambayo yalikuwa kwa asilimia 26.2 na asilimia 24.6, mtawalia, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wateja pamoja na matumizi makubwa ya huduma za kifedha kupitia simu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, amesema ukuaji huo umetokana na utekelezaji wa mkakati wa kampuni, uwekezaji endelevu katika miundombinu ya mtandao pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za mawasiliano na kifedha.
“Tumefanya vizuri katika kipindi cha miezi sita ya kwanza, mafanikio yanayoakisi utekelezaji madhubuti wa mkakati wetu na kuendelea kuongezeka kwa mahitaji ya huduma zetu za mawasiliano, kifedha na kidijitali,” amesema Besiimire.
M-Koba, mikopo ya kidijitali vyashika kasi
Mbali na matokeo hayo ya kifedha, ripoti hiyo inaonyesha huduma za kifedha za kidijitali zimeendelea kupanuka, zikiwemo huduma za kuweka akiba, mikopo na malipo kwa njia ya simu.
Huduma ya M-Koba inayotolewa kwa ushirikiano na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imeongeza amana kwa zaidi ya asilimia 50, huku idadi ya watumiaji ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 na kufikia karibu milioni mbili.
Katika huduma za mikopo ya kidijitali, kampuni hiyo imesema imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh2 trilioni kwa wakopaji karibu milioni saba, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.7.