KFC au KEC: Kuna maana gani Serikali kuanzisha “combination” mpya kidato cha tano

March 29, 2021 2:47 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Tahasusi (combination) mpya zilizoanzishwa ni KFC, PMC, PGE, PBF na KEC.
  • Wachambuzi wa elimu wasema zitasaidia kuongeza ujuzi na maarifa yanayohitajika katika soko la ajira.
  • Wengine wasema zitasaidia kukipaisha Kiswahili kimataifa. 

Dar es Salaam. Maoni mchanganyiko yameibuka baada ya Serikali kutangaza kuanzisha tahasusi (combination) mpya tano ikiwemo ya masomo ya Kiswahili, French, Chinese (KFC) kwa wanafunzi wa kidato cha tano. 

Hata hivyo, sehemu kubwa ya watu wanaamini tahasusi za sayansi na baadhi za sanaa zinaweza kusaidia vijana wa Tanzania kuwa na ujuzi unaohitajika katika ulimwenguni wa fursa za ajira na biashara. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo amezitaja tahasusi hizo mpya kuwa ni Physics, Mathematics na Computer Studies (PMC), Kiswahili, French, Chinese (KFC), na Kiswahili, English na Chinese (KEC),

Tahasusi nyingine ni Physical Education, Biology na Fine Art (PBF) na Physical Education, Geography, Economics (PGE). 

Jafo aliwaambia wanahabari jijini Dodoma Machi 29, 2021 kuwa tahasusi hizo ni kwa ajili ya wanafunzi wanaoingia kidato cha tano mwaka huu ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa wataalam wanaohitajika katika soko la ajira. 

Shule za awali zilizopata fursa ya kufundisha tahasusi ya PMC ni Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dodoma na Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Iyunga iliyopo mkoani Mbeya ikiwa ni moja ya jitahada za Serikali kuongeza wataalam katika fani ya masuala ya sayansi hususan Tehama. 

KFC na KEC, ambazo zinahusisha zaidi kuwapika wataalam wa lugha, itafundishwa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Morogoro (Morogoro) na Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Usagara iliyopo mkoani Tanga.

Kwa wanafunzi wanaotaka kubobea katika fani ya michezo, sanaa na uchumi, wao watatakiwa kusoma tahasusi za PBF na PGE na wanatakiwa waende kati ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Makambako mkoani Njombe, Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibiti (Pwani) au Sekondari ya Mpwapwa ya mkoani Dodoma ambayo ni ya mchanganyiko.

“Nchi yetu ilikosa kuwa na wataalam wa michezo kutokana na kutokuwepo na tahasusi maalum, hivyo hili ni jambo jipya ambalo mwanzo halikuwepo,” amesema Waziri Jafo wakati akitangaza tahasusi hizo ambazo zitaanza kufundishwa mwaka huu. Hadi wakati Serikali inaanzisha tahasusi hizi mpya tayari kulikuwa na dazani ya tahasusi nyingine za sanaa na sayansi zikiwemo PCB (Physics, Chemistry, na Biology), PCM (Phyisics, Chemistry and Mathematics) na HKL inayohusisha History, Kiswahili na Language (Kiingereza). 

Uanzishwaji wa tahasusi hizo mpya umeibua mjadala nchini hususan miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya elimu. Hata hivyo, kumekuwepo na mgawanyiko wa maoni miongoni mwao. 

 

“Ni mwanzo mpya”

Muda mfupi baada ya Tamisemi kutangaza tahasusi hizo tano, baadhi ya wanafunzi, walimu na wachambuzi wa elimu wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa tahasusi hizo mpya zitasaidia zaidi vijana wa Tanzania kuwa na ujuzi unaohitajika zaidi katika soko la ajira kwa sasa. 

Nicodemus Samson ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Samora Machel ya Jijini Mbeya amesema anatamani angepata fursa ya kusoma tahasusi ya PMC lakini sasa hawezi tena kwa sababu tayari alichagua mchepuo wa PCB. 

Amesema tangu akiwa mdogo alipenda kutumia programu za kompyuta na anafikiri watakaosoma tahasusi hiyo watapata vitu vingi vizuri kwa sababu masomo ya kompyuta yanahitaka sana katika ulimwengu wa teknolojia.

“Serikali imefanya vizuri kwa sababu wanafunzi wengi bado hawajui kutumia kompyuta, kama wameanza kufundisha hiyo kozi basi itawafaidisha wengi wanapoingia chuo kikuu,” amesema mwanafunzi huyo. 

Ujuzi wa kutumia kompyuta umekuwa ni miongoni mwa vigezo muhimu ambavyo waajiri wamekuwa wakivitumia kuajiri wafanyakazi kwa sababu kazi nyingi hufanyika kwa kutumia kifaa hicho. 

“Ninapenda PMC. Hii itatengeneza wabunifu wengi wa teknolojia,” ameandika Given Edward, mwanzilishi wa programu tumishi za simu za elimu za My Elimu na Mtabe katika ukurasa wake wa Twitter. 

Hata hivyo, Edward ameshanga somo la Physical Education kuwekwa pamoja na Econimics na Geography kwa sababu anafikiri havishabihiani.

Mtumiaji mwingine wa Twitter anayejulikana kwa jina la @Phofio amesema kwa muda sasa sekta ya michezo imekosa wachumi na wakadiliaji, jambo lililozuia fursa mbalimbali kwa nchi kufaidika. 

“Hili linaenda sambamba na Geography. PE (Physical Education) inayofundishwa vyuoni inahitaji kwa sehemu Geography,” ameandilka mtumiaji huyo wa Twitter. 


Soma zaidi:


Kiswahili kupanuka zaidi

Kozi za KFC na KEC  ambazo zina masomo ya lugha ya Kiswahili, Kiengereza, Kichina na Kifaransa zinaweza kupata msukumo wa aina yake nchini Tanzania na kuongeza wataalam wa lugha hizo.

Watanzania wamekuwa wakifanya biashara na Wachina na kasi ya uhusiano na Taifa hilo la Asia Mashariki unazidi kuongezeka kila siku. 

Mwandishi wa vitabu na mchambuzi wa masuala ya elimu, Richard Mabala ameiambia Nukta Habari kuwa kuanzishwa kwa kozi hizo mbili za KFC na KEC kuna maana kubwa hasa katika uendelezaji na ukuaji wa lugha ya Kiswahili ambayo inazungumzwa nchini na kimataifa.

“Lugha ya Kiswahili inakua kwa kasi kimataifa, tunahitaji wakalimani wa lugha, hivyo itasaidia kuongeza wataalam katika eneo hilo,” amesema Mabala.

Mabala ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la HakiElimu amesema pia uelewa na matumizi ya lugha ya Kiengereza utaimarika kwa sababu umekuwa ni ugonjwa wa Taifa kwa wahitimu wengi wa vyuo vikuuu.

Hata hivyo, Mabala amesema Serikali ilipaswa kuanzisha kozi zinazohusisha stadi za kazi ambazo ni muhimu kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi wa kujiajiri na siyo kusubiri kuajiriwa kwa sababu ushindani katika soko la jira ni mkubwa.  

Kuongezwa kwa tahasusi inaweza isiwe changamoto ila bado wengi wana hofu iwapo walimu wa shule husika watakuwa tayari kuwafundisha wanafunzi kwa kiwango kinachotarajiwa ikizingatiwa baadhi ya vifaa vya kufundishia hususan katika masomo ya sayansi ni adimu. 

Kuanzishwa kwa kozi ya elimu ya mazoezi, uchumi na jiografia kutasaidia kuikuza sekta ya michezo nchini kwa sababu itapata wataalam wengi. Picha|Mtandao. 

Shule, Walimu wapo tayari kufundisha tahasusi hizo? 

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dodoma, Amani Mfaume 

amesema shule yake kuchaguliwa kufundisha PMC siyo kitu kigeni kwa sababu masomo hayo yanafundishwa shuleni hapo kwa namna tofauti.

“Masomo haya tunayafundisha hapa kwa namna tofauti lakini sasa yameunganishwa na kuwa kozi moja. Sisi tuko tayari kufundisha,” amesema Mfaume wakati akiongea na Nukta Habari kwa njia ya simu.

Amesema nchi inahitaji wataalam hasa katika fani za sayansi, hivyo ujio wa kozi hiyo utapunguza pengo la wataalam wengi kupatika vyuoni.  

“Hii ni hatua nzuri ya kuongeza wataalam, somo la kompyuta litapata wataalam hadi ya ngazi ya sekondari kama ilivyo kwa Physics na Chemistry,” amesema Mkuu huyo wa shule na kubainisha shule ina vitendea kazi vyote vinavyohitajika wakiwemo walimu, vifaa vya kusomea na kujifunzia. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW