Kenya yafunga mpaka wake na Tanzania, Somalia
- Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta amesema itasaidia kudhibiti maambukizi ya COVID-19.
- Malori ya mizigo pekee kutoka Tanzania ndiyo yataruhusiwa kupita mpakani.
Dar es Salaam. Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amefunga mipaka kati ya nchi hiyo na Tanzania na Somalia kuanzia usiku wa Mei 16 ili kudhibiti kusambaa zaidi kwa ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19).
Kenyatta aliyekuwa akilihutubia Taifa kutoka Ikulu Jijini Nairobi leo (Mei 16, 2020) amesema ni malori ya mizigo pekee kutoka katika nchi hizo ndiyo yataruhusiwa kupita mpakani.
Hatua hiyo itafanya sasa Watanzania na Wakenya waliokuwa na mipango ya kuzuru nchi hizo mbili kwa masuala ya kijamii na kibiashara kukosa fursa hiyo hata hadi hapo siku 30 alizotangaza Rais Kenya zitakapokoma.
“Madereva wote wa malori ya mizigo watalazimika kupima COVID-19 na wataruhusiwa kuingia katika mpaka wa Jumhuri ya Kenya ikiwa vipimo vitaonyesha hawana maambukizi,” amesema Kenyatta.
Amesema wiki iliyopita wamelipoti wagonjwa 166 wa Corona ambao kati yao 43 wanatoka katika nchi za jirani za Somalia na Tanzania.
Kati ya wagonjwa 43 wa Corona, 14 waliripotiwa katika mpaka wa Wajir, Namanga (16) na Lunga Lunga (2) na mmoja Loitoktok.
Mpaka sasa Kenya imeripoti visa 830 vya wagonjwa wa ugonjwa huo hatari duniani ambapo kati ya hao 50 wamefariki dunia.
Soma zaidi:
- Dk Mpango: Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 4 mwaka 2020
- Zanzibar yapokea mashine moja ya kupima Corona
Kenya inakuwa nchi ya pili kufunga mpaka wake na Tanzania baada ya Zambia kufunga mpaka wa Nakonde unaotenganisha nchi hiyo na Tanzania Mei 11 na baadaye kufunguliwa usiku wa Mei 14. Hatua hiyo ilikuja baada ya kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wa COVID-19 kufikia 76 katika mji wa Nakonde.
Kufungwa kwa mpaka wa Nakonde kulikwamisha malori mengi ya Tanzania katika pande zote mbili na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.
Katika siku hivi karibuni kumeripotiwa vikwazo mipakani hususan kwa madereva wa malori baada ya kila nchi ya Afrika Mashiriki na Kati kuzidi kukaza uzi katika upimaji wa COVID-19 kuhakikisha watu wanaoingia katika mataifa hayo wasambazi zaidi virusi hivyo.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba Kabudi ameendelea kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuacha wazi mipaka yake licha ya tishio la janga la Corona ili kuruhusu bidhaa muhimu kufika katika nchi zisizo na bandari.
“Corona ni hatari, lakini kukosekana kwa mahitaji muhimu kwa nchi zisizo na bandari kama chakula, dawa na mafuta ya petroli ambavyo vinapitia katika bandari yetu kuelekea katika nchi zisizo na bandari kunaweza kuwa ni hatari zaidi,” amesisitiza Prof Kabudi Bungeni jijini Dodoma Mei 13, 2020.
Latest
