Katuni: Mwalimu wa watoto anayepaswa kuchunguzwa- 2

February 15, 2022 10:40 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Utazamaji wa TV kwa muda mrefu huathiri kufikiri na makuzi yao.
  • Inashaurwa mzazi kutazama katuni kabla ya kumpatia mtoto.
  • Wazazi washauriwa kutokukwepa jukumu la kufundisha watoto wao.

Dar es Salaam. Baada ya kuona namna katuni zinavyoweza kuathiri tabia za watoto, katika andiko hili tutaangalia mbinu za kupambana na maudhui mabaya yanayoambatana na kutazama katuni.

Cha muhimu kufahamu ni kuwa, mtoto kuathiriwa na tabia kutokana na katuni ni kama mtu mzima kukariri wimbo ambao haupendi.

Inaanza na kuusikiliza au kusikilizishwa mara kwa mara hadi wimbo huo kumkaa kichwani na mtu kujikuta ameukariri walau maneno mawili matatu na kuanza kuuimba kadri siku zinavyoenda. 

Hivyo ndivyo ilivyo kwa watoto na katuni. Kwa mujibu wa mwalimu Priya Sharma katika andiko lake la 60school,  Kadri mtoto anapoona jambo linafanywa na mhusika anayemuangalia kila siku, akili yake inaona kuwa ni jambo jema na la kawaida. 

Sharma ameeleza, endapo mtoto hatodhibitiwa, anaweza nasa tabia mbaya ikiwemo matusi, kiburi, changamoto za kiafya na vurugu.

“Kuna katuni nyingi zinazochochea tabia zisizokubalika kwa kuwapatia watoto jumbe zisozofaa. Zipo katuni zenye tabia mbaya, kuchochea ngono na kadhalika. Hii inaweza KUathiri ukuaji wa mtoto hasa kwenye umri mdogo,” ameandika Sharma. 

Kama maudhui hayapaswi kutazamwa na mtoto, asipokuwepo mzazi wa kutoa maelekezo maudhui hayo yatamwathiri mwanao. Picha| iStock.

Kwa mujibu wa Wanasaikolojia, watoto wanaotumia saa tatu hadi nne kutazama katuni wapo hatarini kuambukizwa tabia za wahusika kwenye katuni wanazozitazama.

Mtaalamu wa masuala ya watoto kutoka Shirika la Watoto, Save the Children, Wilbert Muchunguzi ameiambia Nukta Habari kuwa, kinachosababisha yote haya ni wazazi kuhisi kuwa katuni ni za watoto tu, jambo ambalo siyo sahihi kwani zipo katuni za watu wazima.

Katuni hizo zinapotazamwa na watoto, zinaweza kuwaambukiza tabia na maadili yasiyo sahihi. 

“Nyingine zinawaelekeza kuanza kufukiria mambo ya mahusiano ya kiutu uzima, nyingine wawe na fujo na kutukanana,” amesema Muchunguzi. 

Kama mzazi, iIli kuepukana na hali hiyo, zingatia haya;

Weka ukomo wa muda wa kutazama katuni

Unatakiwa kujua kuwa maisha mengine ya mtoto lazima yaendelee mfano michezo, kujifunza kazi za ndani, kufanya kazi za shuleni na siyo katuni muda wote. 

Sharma anashauri kukaa mezani na mtoto wako na kumweleza mabaya yanayoweza kuambatana na kutazama katuni muda wote lakini pia umuhimu wa michezo nje ya sebule.

“Weka ukomo wa muda wa kuangalia katuni. Unaweza kuweka saa moja kwa siku,” ameshauri Sharma.


Soma zaidi


Tazama katuni na mtoto wako

Mtoto anahitaji mtu wa kumweleza kizuri na kibaya ili aweze kuuliza maswali yake pia.

Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Neema Simbo amesema yeye hutazama katuni kabla ya kumruhusu mtoto wake kuzitazama.

“Ni kweli zinajenga lakini kama mzazi huwa naziangalia kwanza. Nikikuta kuna mambo siyaelewei, niajiandaa kabisa kumwelewesha kuwa hili siyo sahihi,” amesema Simbo.

Mzazi huyo amesema, hauwezi kumficha mtoto wako na maudhui kwani asipoona nyumbani, huenda akaona shule, kwa jirani na hata kuambiwa na watoto wenzie.

Ni vyema kuweka ukaribu na mtoto wako ili awe huru kuuliza swali lolote na kupata majibu sahihi kutoka kwako kuhusu utazamaji wa katuni.

Chagua katuni za mtoto wako kutazama

Kama mzazi, una nguvu ya kuchagua katuni zipi mtoto aangalie. Hiyo ni nafasi ya kumchagulia mtoto katuni zilizo na maudhui ya elimu kwa ajili yake kujifunza.

Mfano, kwenye baadhi ya ving’amuzi mzazi anaweza kufunga baadhi ya chaneli na kuruhusu zile unazoona zinamfaa mtoto wako.

“Unaweza kufunga baadhi ya chaneli zenye katuni mbaya ukabakiza zile zenye katuni za kuelimisha,” amesema Monica Meshack, mkazi wa Shinyanga.

Naye Afisa Mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Getrude Gyabene amesema hata sheria ya mtoto tanzania inakataza mtoto kuonyeshwa maudhui ya kiutu uzima. 

Kulizuia hilo ameshauri mzazi kutafuta njia za kuhakikisha mtoto anatazama maudhui ambayo anauhakika nayo kwani watoto wanatazama maudhui wasiyotakiwa kuyaona kwa “asilimia 85”.

“Tafuta katuni ambazo utazipenda, ziseti au ziweke kwenye CD na umpatie mtoto awe anaangalia kuliko umwache atazame televisheni peke yake,” amesema . 

Mengine yanayoshauriwa ni kumuelimisha mtoto wako kuwa katuni siyo uhalisia ili ajue kuwa baadhi ya vitu havipo kwenye ulimwengu halisi.

Hadi hapo, nakutakia malezii mema kwa mtoto wako. Natumaini makala haya yamekupatia cha kujifunza. Unaweza kuendelea kufuatilia makala mengine ya malezi kupitia www.nukta.co.tz

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks