Kanuni za kuzingatia unapo andaaa unga wa lishe kwa mtoto

September 23, 2025 7:07 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni muhimu kuzingatia mchanganyiko sahihi wa vyakula ili kuepuka madhara ya kiafya kwa mtoto.

Dar es Salaam. Unga wa lishe ni chakula chenye virutubisho vingi na muhimu kwa makundi mbalimbali ya watu kama vile watoto, wajawazito na wazee. 

Unga huu huandaliwa kwa kuchanganya nafaka na jamii ya mikunde ili kutoa mlo kamili na wenye virutubisho muhimu vinavyohitajika mwilini.

Kwa mujibu wa Afisa Lishe mkoa wa Dar es Salaam, Mwanamvua Zuberi, ameeleza kuwa uji wenye lishe bora unatakiwa kuandaliwa kwa mchanganyiko wa vyakula tofauti, si nafaka pekee kama jamii ilivyozoea.

“Ukiangalia kazi za hivi vyakula zipo kulingana na aina ya kundi au viini lishe, vina kawaida ya kuwa na wingi kulingana na aina ya kundi ya hicho chakula , kwa mfano vyakula vya jamii ya nafaka kazi yake ni kukusaidia kuupa mwili nguvu na joto…

…Lakini vyakula vya jamii ya wanyama na jamii ya mikunde kazi yake ni kusaidia katika kutengeneza seli, kusaidia katika ukuaji, vyakula vya jamii ya matunda na mboga mboga hivi husaidia kuupatia mwili vitamini na madini,” ameeleza Zuberi.

Mwanamvua ameongeza kuwa watoto wanapopewa uji ulioandaliwa kwa nafaka pekee hukosa virutubisho muhimu, jambo linaloweza kusababisha kudumaa na matatizo mengine ya lishe. 

Kwa kuzingatia umuhimu wa lishe makala hii imeandaliwa mahsusi kukusaidia kuelewa vitu vya kuzingatia unapohitaji kuandaa unga wa lishe kwa mtoto.

Changanya nafaka na mikunde kwa uwiano sahihi, ili mtoto wako apate nguvu na ukuaji bora. Picha/ Canva.

Mchanganyiko sahihi wa nafaka na mikunde


Watu wengi huamini kuwa kuchanganya nafaka nyingi kama mahindi, mchele, mtama na uwele kunatoa uji wenye virutubisho zaidi.

Zuberi anaeleza kuwa kufanya hivyo huongeza gharama za utengenezaji bila kuongeza faida ya kiafya kwa mtoto.


Badala yake, ni bora kuchagua aina moja au mbili za nafaka, kisha kuzichanganya na jamii ya mikunde kama vile maharage, choroko, kunde au njugu. 

Mchanganyiko huu husaidia kumpa mtoto wanga kwa ajili ya nguvu na joto, pamoja na protini ambayo ni muhimu sana kwa ukuaji.

Hapa mtengenezaji anaweza kuongeza viungo kutoka makundi mengine ya vyakula.

Ni muhimu kupata vyakula vyenye kiwango cha kutosha cha omega -3. Picha/ Canva.


Ili kuongeza virutubisho zaidi, unaweza kuongeza viungo vingine kama, maziwa ya unga, mbegu za mafuta (kama vile mbegu za maboga), mboga za majani zilizokaushwa kitaalamu na kusagwa.

Lakini pia kwa ajili ya kuboresha afya ya ubongo, ni muhimu kupata vyakula vyenye kiwango cha kutosha cha omega -3,ambayo unaweza kuipata kwenye samaki (samaki waliokaushwa na kusagwa) na mbegu za haradali (mustard seeds).

Hii huongeza vitamini na madini zaidi, na hivyo kufanya uji wa mtoto kuwa na virutubisho vingi na salama kwa afya yake. 

Mbegu, maharage na mboga za majani hufanya uji kuwa na ladha ya kipekee. Picha/ Canva.

Kulingana na tovuti ya Abiteafya inasisitiza kuwa unga wa uji wa lishe unapaswa kuwa na nafaka chache kwani uwepo wa nafaka nyingi huleta changamoto katika kutayarisha chakula hicho kwasababu kuna nafaka zingine huchukua muda mrefu kuiva.

Zingatia ladha na uwiano sahihi


Ni muhimu kuzingatia ladha ya chakula, kama wewe mzazi huwezi kunywa uji huo, mtoto wako pia atapata shida kuukubali.

Pia, unga wa lishe unatakiwa kuandaliwa kwa kuzingatia uwiano sahihi wa viungo vyake iwapo ukikosewa, unaweza kuathiri usalama na ubora wa lishe ya mtoto.

Kwa upande wa tovuti Wema herbal clinic, kiwango cha virutubishi anavyohitaji mtoto hutofautiana kulingana na mahitaji ya ukuaji na maendeleo ya mtoto.

Hakikisha ladha ya uji ni rafiki kwa mtoto, ili uji wa lishe ukubalike na kuleta matokeo. Picha/ Canva.

Tovuti hiyo imeendela kusisitiza kuwa katika kuchanganya virutubisho hivi inatakiwa angalau kuwa na kiwango kikubwa cha wanga ili kusaidia kuupatia mwili nguvu.

Iwapo utahitaji kuanda unga wa lishe inapaswa kuwa na kundi la chakula la wanga angalau kilo moja, protini nusu kilo na kundi la vyakula vya mafuta robo kilo.

Usalama na ubora

Unga wa lishe una nafasi kubwa katika afya na ukuaji wa mtoto ili kupata matokeo bora ni muhimu kuandaa unga kwa kuzingatia mchanganyiko sahihi na kwa viwango vinavyokubalika ili kuleta matokeo bora kwa afya na ukuaji wa mtoto. 

Iwapo ikitokea kiungo kimoja kikazidi kingine huweza kusababisha kupata ladha usiyotarajia au madhara ya kiafya kwa mtoto.

Tukutane tena kwenye makala ijayo ambayo tutaangazia hatua kwa hatua namna ya kuandaa unga lishe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks