KANUNI YA 3: Umuhimu wa nguvu ya kiasi kwa afya yako
- Nguvu ya kuwa na kiasi ni muhimu katika uimarishaji wa afya bora.
- Itakusaidia kuepuka madhara yatokanayo na kutumia vyakula kupita kiasi.
- Itakupunguzia gharama za matibabu pale unapopatwa na ugonjwa.
Kuwa na kiasi inatafsiriwa kama uwezo wa kudhibiti matumizi ya kitu ama vitu fulani kwa kiwango kinachohitajika. Waswahili wanasema unakuwa na “spidi gavana” wa mambo unayofanya.
Nguvu ya kuwa na kiasi ni muhimu katika uimarishaji wa afya bora. Ni kanuni muhimu sana iwapo ukiizingatia. Kwani hukufanya kuwa na mipaka katika kila kitu unachofanya na kutumia. Ili kufanikiwa kimwili, kiakili na kimaadili katika maisha ni muhimu kuwa na kiasi katika kila kitu kizuri na hata kile ambacho ni hatarishi.
Ili kulinda afya ni muhimu kuwa na kiasi katika kila kitu. Chakula na hata vinywaji. Huo ndiyo msingi bora wa afya. Kuwa na kiasi hutusaidia kuepuka vitu ambavyo ni hatari kwa afya yetu na pia hutusaidia kutumia na kuchagua vile ambavyo vina faida na madini ya kujenga miili yetu. Tuwe na kiasi katika mambo gani?
Kuna vitu vya kutumia kwa kiasi na kuna vitu vya kuacha kabisa ili kuweka miili yetu katika hali ya usawa na afya madhubuti. Haya ni baadhi ya mambo tutaangazia ya kuwa na kiasi na mengine ya kuacha katika kanuni hii muhimu:
Epuka matumizi tumbaku na pombe
Tumbaku ni sumu inayoua taratibu kama una uwezo wa kuacha, usiendelee kuitumia itakugharimu siku zijazo. Pia jitahidi kupunguza unywaji wa pombe. Ukiweza acha pombe kabisa.
Tumbaku na pombe huchangia sana kupata satarati za mapafu, ini na hata kusababisha upungufu wa nguvu za kiume ambazo zinahitajika katika kuendeleza vizazi duniani.
Sambamba na hilo, kaa mbali na kemikali ambazo huharibu mfumo mzima wa utendaji kazi wa mwili wako ikiwemo harufu kali.
Matumizi ya pombe na sigara ni hatari kwa afya yako. Picha| Dave Lastovskiy on Unsplash.
Punguza ulaji wa vitu vyenye sukari nyingi
Dhibiti matumizi ya kafeini iliyo kwenye kahawa kwa kiasi kikubwa. Kemikali hiyo ya kafeini huongeza sukari mwilini, hii ni hatari kwa mgonjwa mwenye kisukari tayari.
Kuwa na kiasi katika matumizi ya vitu vyenye sukari nyingi kupita kiasi ikiwemo keki, “lambalamba” na pipi. Usiwe mteja sana wa vitu hivi mara kwa mara.
Zinazohusiana:
- Jinsi unavyoweza kuishinda sonona isiharibu maisha binafsi, kazi
- Mambo yatakayokusaidia kupunguza hatari ya kupata saratani
- Fanya haya kulinda afya kazini
Matumizi ya mafuta
Unashauriwa kama utaweza, kupunguza ulaji wa nyama hasa nyama nyekundu ambayo inapatikana kwa wanyama kama ng’ombe na mbuzi. Mafuta ya wanyama hubeba magonjwa mengi ndani yake. Pia tumia mafuta ya kupikia yanayotokana na mimea kuliko wanyama.
Punguza kula nafaka zilizokobolewa
Jitahidi kutumia ngano, mahindi au mchele ambao haujakobolewa ili kupata madini na virutubisho tosha katika mlo wako. Nafaka iliyokobolewa inapungikiwa na baadhi ya virutubisho muhimu vinavyohitajika kujenga mwili wako.
Pia jitahidi kuwa na kiasi katika kuweka uwiano wa chakula chako uwe na mlo kamili. Usifanye kazi kupita kiasi na pia usiwe mzembe. Pata muda wa kutosha wa kupumzika wa. Hakikisha unakua msafi na nadhifu kila mara.
Nafaka zisizokobolewa zinasaidia mchakato wa kumeng’enya chakula kuwa mrahisi na hivyo kukuepusha na matatizo mbalimbali ya mfumo wa chakula mwilini. Picha| Margarita Zueva on Unsplash
Usisahau na haya…
Pia punguza matumizi ya chokoleti pamoja na cocoa, kwa sababu vikitumika kupita kiasi vina madhara yake mwilini kutokana na sukari iliyopo ndani yake.
Chakula chako unapokiandaa usikiwekee viungo vingi kupita kiasi. Hii husababisha shida katika kuchakata na kumen’genya chakula tumboni.
Kimsingi chochote unachofanya, uwe na kiasi na kuwa na tabia ya kuacha vitu ambavyo ni hatari kwa afya yako. Mtindo wa maisha wenye kiasi ni muhimu katika kuimarisha na kuijenga afya yako. Tukutane tena wiki ijayo katika kuangalia kanuni ya nne.
Dk Joshua Lameck Sultan ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba katika Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi Moshi (KCMC) pamoja na hospitali ya KCMC. Pia ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) ambapo hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.
Latest
