Kamala Harris alivyohitimisha ziara ya siku tatu Tanzania

March 31, 2023 9:36 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ameondoka leo asubuhi kuelekea Zambia. 
  • Aacha neema ya 2.5 trilioni na kuimarisha ushirikiano wa kati ya Tanzania na Marekani.
  • Ni ziara ya kwanza ya kiongozi wa juu wa Marekani baada ya miaka 10 kupita.

Dar es Salaam. Hatimaye, mara baada ya kukamilisha  ziara yake ya  kikazi ya siku tatu, Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris ameondoka Tanzania kuelekea Zambia huku ziara yake ikitarajiwa kuacha neema kubwa.

Kamala pamoja na ujumbe wake  wameondoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) majira ya saa tano na dakika 32 asubuhi (11:32) kwa kutumia ndege maalum ya makamu wa rais iitwayo ‘Air Force 2’.

Mapema majira ya saa tano na dakika 13 Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Philipo Mpango aliwasili uwanjani hapo akiwa ameongozana na mkewe tayari kabisa kwa ajili ya kumuaga mgeni wake ambaye aliwasili dakika nne baadaye.

Mara baada ya kuwasili viongozi hao walisalimiana kisha Kamala akaagana na baadhi ya viongozi waliomsindikiza uwanjani hapo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, Balozi wa Tanzania  nchini Marekani Dk Elsie Kanza pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk Stergomena Tax.

Milango ya ndege ya Air force 2 ilifungwa majira ya saa tano na dakika 28, mara baada ya Kamala kuwa ameshapiga picha ya kumbukumbu, na kuwapungia mikono ya kwaheri Watanzania na wageni waliofika kumuaga uwanjani hapo.

Kamala anaelekea nchini Zambia ambako anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo itakuwa hitimisho ya ziara ya nchi tatu za Afrika aliyoianza Machi 27 nchini Ghana.


Soma zaidi:


Ziara ya kiongozi huyo wa pili kwa madaraka nchini Marekani ambapo ni ya kwanza kufanywa na Makamu wa Rais wa Marekani nchini inatarajiwa kuleta neema ya fedha  ikiwemo zaidi ya Dola za Marekani milioni 500 sawa na Sh1.17 trilioni za Tanzania ambazo ni kwa ajili ya kuendeleza sekta za teknolojia na miundombinu.

Katika hotuba yake kwa vyombo vya habari aliyoifanya Machi 30, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam pamoja na kumpongeza Rais Samia kwa maboresho ya demokrasia, Kamala  amesema Marekani imevutiwa kuendelea kufanya uwekezaji nchini Tanzania.

“Nina furaha kutangaza mipango mipya ya Serikali ya Marekani kwanza kupitia Benki ya Exim tutasaini mkataba wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500 (Sh1.17 trilioni) za Tanzania ambapo zitasaidia uagizaji wa bidhaa kutoka Marekani  katika masuala ya miundombinu, usafiri, teknolojia na na nishati safi, “ alisema Kamala.

Maeneo mengine ambayo Serikali ya Marekani inapanga kufanya uwekezaji ni pamoja na teknolojia ya intaneti yenye kasi ya 5G, usalama mtandaoni, pamoja na uwekezaji katika kiwanda cha kuchakata betri za magari ya umeme ambacho kinatarajiwa kukamilika mwaka 2026.

Ziara hiyo ya kiongozi wa juu wa Marekani, inatajwa kama ishara ya kufufuka kwa mahusiano kati ya Tanzania na Marekani na imetokea baada ya kupita takribani muongo mmoja tangu Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama aizuru Tanzania Julai mosi mwaka 2013.

Kamala alitembelea kampuni changa zinazoibua suluhu mbalimbali katika jamii kwa kutumia ubunifu na teknolojia  ambapo pia alitembelea mnara wa kumbukizi wa watu waliopoteza maisha katika tukio la kulipuliwa kwa ubalozi wa Marekani nchini Tanzania mwaka 1998.

Pia alifanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan na kutembelea Makumbusho ya Taifa (NMT) jijini Dar es Salaam.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW