Jinsi ya kuhimili ushindani wa soko la bidhaa, huduma

October 21, 2019 9:45 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Biashara ni ushindani, bila huo hauwezi kukua na kustawi.
  • Hakikisha unatatua matatizo ya msingi ya wateja wako, ongeza ubunifu na panga bei inayolingana na thamani ya bidha. 

Dar es Salaam. Maisha ya mafanikio wakati wote yametawaliwa na ushindani. Kila siku, utakutana na ushindani wa namna fulani unaokusudia kukuzuia kufika pale unapotaka kufika. 

Kwa wafanyabiashara, hili siyo jambo geni kwao kwa sababu wanashindania kuuza bidhaa na huduma kwa wateja. 

Kama ushindani ni sehemu ya biashara, ufanye nini kuhakikisha unawashinda washindani wako na kuifanya bidhaa au huduma yako ikubalike kwa watu na kukufanya uwepo kwenye soko kwa muda mrefu ujao? Jaribu mbinu hizi zinazoweza kukusaidia:

Tatua matatizo ya msingi ya wateja wako

Waulize wanataka nini hasa kutoka kwenye bidhaa au huduma yako. Inawasaidia kuondokana na matatizo au inakidhi mahitaji yao kama wanavyotaka?

Jambo la msingi hapa ni kutoa suluhisho kulingana na mahitaji yao na siyo kuwauzia kile unachokitaka wewe. Wakati mwingine wateja wanaona na kuichukulia tofauti bidhaa yako na unavyofikiria wewe. 

Bidhaa au huduma yako itaanza kuuzika zaidi ya mshindani wako, kama utafanikiwa kugusa kiini cha mahitaji ya wateja wako. 


Zinazohusiana:


Tumia mbinu tofauti kuikuza biadhara yako

Kama unauza bidhaa ambazo zinawashindani wengi, ni vigumu kwa biashara yako kutanuka na kustawi, kama hautatumia mbinu tofauti ukilinganisha na zile wanazotumia washindani wako. 

Tafuta kitu tofauti kabisa ambacho kitakutofautisha na washindani wako, hata kama wote mnauza bidhaa inayofanana. 

Hapa unaweza kutumia njia kama kutangaza katika mitandao ya kijamii, kutengeneza maudhui kuhusu faida na shuhuda za kutumia bidhaa yako. Usiache bidhaa usimame peke yake, itegemeze kwa njia mbalimbali ili ionekane na watu tofauti wenye mitazamo tofauti. 

Dhamiria kuwafikia wateja uliowakusudia kwa bidhaa bora na zenye uhakika katika upatikanaji na usambazaji. 

Fanya utafiti wa bei ya bidhaa unayouza

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya masoko ya Over The Top SEO ya nchini Marekani, Guy Sheetrit anasema katika moja ya makala zake kuwa bei nzuri ni moja kati ya saikolojia ya soko la bidhaa.

Kabla ya kupanga bei, ni vema ukafanya utafiti kwa washindani wako wa bei wanazotumia kuuza bidhaa zao. Je bei zao zinalingana na thamani na bidhaa wanayotoa?Hakikisha wateja wako wanaweza kuimudu bei utakayopanga na iwe na uwezo wa kuhimili ushindani wa soko. 

Bei nzuri siyo ile iliyo chini zaidi ya washindani wako ili kuwapata wateja wengi. Ni lazima iendane na thamani ya bidhaa na aina ya wateja unaotaka kuwafikia.

Sheetrit anasema soko lolote limeganyika katika makundi matatu; la watu wa chini, kati na wa juu. Kwahiyo ni muhimu kujua ni watu gani uliowalenga kuwafikia. Ukifanikiwa katika hatua hiyo utaweza kuweka bei ambayo wateja wako wataifurahia. 

Bidhaa au huduma yako itaanza kuuzika zaidi ya mshindani wako, kama utafanikiwa kugusa kiini cha mahitaji ya wateja wako. Picha|Mtandao.

Kuwa mbunifu na mgunduzi wakati wote

Mabadiliko ndiyo kitu pekee duniani ambacho hakibadiliki. Ubunifu wako na kuvumbua mbinu mpya za masoko kila siku, ndiyo uhai wa biashara yako kwani dunia inaenda kasi sana. 

Wakati wote jifunze na tafiti njia mbadala za kuboresha bidhaa yako ili kukabiliana na ushindani wa soko. Usigope kuchukua hatua au kufanya mabadiliko katika biashara yako. 

Kampuni za Nokia na BlackBerry ziliondolewa katika soko la simu janja kwa sababu zilikosa ubunifu. Wakati wote kumbuka washindani wako wanafanya ubunifu na wapo wapya wanaoingia sokoni wakiwa na bidhaa zenye ubora zaidi.

Imarisha kitengo cha huduma kwa mteja

Watu wanapenda biashara zinazowapa huduma za tofauti. Ukitoa huduma bora kwa wateja wako, ni rahisi kukuletea wateja wengine. 

Ajiri wafanyakazi wenye uelewa mpana wa bidhaa au huduma yako. Hakikisha wanakuwa wavumilivu na kutoa majibu yenye kuridhisha kwa kila mteja anayewauliza jambo. 

Lakini huduma kwa mteja itakuwa na ufanisi kama biashara yako itakuwa na watu wanaofanya kazi kwa umoja na ushirikiano. 

Dondoo hizi zinaweza kukusaidia kuinua biashara yako na kuhimili kishindo cha ushindani wa soko. 

Enable Notifications OK No thanks