Jinsi ya kuepuka ‘presha’ ya kuoa, kuolewa

January 21, 2021 8:33 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Kuoa/ kuolewa siyo jambo linaloangalia umri, linahitaji akili iliyopevuka.
  • Uvumilivu, mawasiliano na uwazi ni vitu muhimu kabla na baada ya ndoa.
  • Usioe au kuolewa ni uamuzi binafsi na haupaswi kushikizwa na mtu yeyote.

Dar es Salaam. Ndugu: Utaoa, utaolewa lini? 

Mimi: “Bado nipo nipo kwanza” 

Ndugu: Eeeh! Jamani bado tu? 

Hayo ni kati ya mazungumzo ambayo vijana wengi hupitia wakutanapo na watu ambao hawajaonana kwa muda mrefu wakiwemo rafiki na ndugu.

Hali huwa mbaya wanapowatembelea ndugu zao vijijini ambako huko, wengi walio na rika lao tayari wanafamilia zao na wanasongesha maisha. 

Jambo hilo huwafanya kuwa mate yasiyoisha katika midomo ya rafiki wa wazazi wao ambao vijana wao tayari wamewawezesha kuitwa wakwe walio na wajukuu. 

Kwa baadi hali huwa mbaya zaidi pale wazazi wanapoanza kuwatambulisha kwa watoto wa rafiki zao na kuwataka waoane nao huku wengine wakichaguliwa wenza wa kuwaoa.

Unawezaje kuepuka msukumo huo? Yapo mambo ya msingi ya kufahamu kabla hujaingia kwenye ndoa kama kijana na ambayo jamii pia inaweza kuyazingatia:

Umri sahihi kwa kuoa

Baada ya kuvuka miaka 25, kwa baadhi ya vijana macho ya ndugu na jamaa huhamia vidoleni yakitafuta pete ya uchumba au ya ndoa. 

Kwa ambao hadi umri huo hawana pete, huulizwa wapi wanakwama na kwa vijana wa kiume huonekana kuwa ni wahuni “wanaoharibu binti za watu.”

Mbunifu wa katuni na picha, Taurus Mangi amesema kwake anaamini inahitaji mwanaume kuwa amepevuka kiakili kuwa na uwezo wa kuoa. 

Kwa upande wake anashauri ndoa walau iwe kwa mwanaume ambaye ana miaka 35 kwani ndiyo atakiwa na hekima ya kummudu mke wake kama kichwa cha familia.

“Sasa hivi kila mdada chini ya miaka 28 anafikiri yeye ni mwanaharakati, mtetea haki za wanawake na ana nafasi sawa na mwanaume. Kitu ambacho hakiwezi kujenga ndoa yenye mahusiano mazuri. 

Vijana wakiume chini ya miaka 35 watakufa kwa presha,” amesema Mangi.

Endapo mtu atafunga ndoa bila ya kuwa na utayari wa kukabiliana na changamoto za ndoa, huenda ndoa hiyo isidumu kwa muda mrefu. Picha| freepik.com

Mwanandoa aliyedumu kwenye ndoa yake kwa miaka mitano Nsajigwa Mwakatobe amesema hakuna umri muafaka wa kuoa bali “ni vile mtu mwenyewe akiona kwamba anaweza kuishi na binti wa watu basi anaoa tu.”

Mwakatobe liyeoa akiwa na miaka 27 anaamini ndoa ni kitu rahisi endapo wote mtakuwa kitu kimoja na kuheshimiana.

“Mimi na wife (mke wangu) tunashirikiana sana kwa kila kitu aisee. Ila mkishajiwekea matabaka kwamba baba ni baba na mama ni mama hapo mnaweza kukwama ingawa heshima kwa kila mmoja lazima iwepo kwa maana ya Baba lazima ajulikane kuwa ni kichwa cha familia.

Hata hivyo, amekiri kuwepo kwa presha ya muda hasa kwa wanawake. 

“Presha ya kuolewa ipo sana upande wa wadada. Wao time inawalimit sana, wanaamini ikifika “30” bado hajapata mtoto basi anakua mzee,” ameelezea Mwakatobe.

Unahitaji kuwa na nini kabla ya kuingia kwenye ndoa?

Kwa vijana wengi huenda hitaji likawa ni nyumba ya kuishi, “mkoko” wa kutembelea na mali. Lakini wapo watu walikuwa na vitu hivyo, wakaoa na kuolewa lakini hawajafanikiwa.

Mtaalamu wa mawasiliano na Mkurugenzi Mtendaji wa Crimson Communications Ltd, Myoma Kapya amesema kikubwa ni kuitambua nafasi yako kabla ya kuoa au kuolewa

Akitoa mfano wake kutoka kitabu cha Biblia, Myoma amesema imeandikwa kuwa mwanaume ni “kicha cha familia” hivyo ili kuwa kichwa inahitaji kuwa thabiti ya kuwa unaweza kuishi na kuitunza ndoa yako pamoja na changamoto zote zitakazokuja nayo.

“Mwanaume anahitaji kujua kuwa yeye ni kichwa na mke wake ni msaidizi wake kwani ameumbwa kutoka kwake. Ndoa nyingi zinavunjika kwa sasabu kizazi cha wanaume wa sasa hawachukui jukumu lao la kuihudumia familia,” amesema Kapya.

Anaeleza kuwa wapo wanaume ambao hawafanyi kazi na wanakaa nyumbani wakiachia majukumu yao wake zao. Hilo hufanya mama awe wa kumhudumia mume wake na watoto kiuchumi na kijamii.

“Kwa sisi Wakristo, unahitaji kuzungumza na Mungu na Roho Mtakatifu akuongoze. Muulize Mungu kama mtu huyo ni sahihi kwako na kama Mungu ndiye amemleta. Kama usipoongea na Mungu, utaishia katika ndoa ambayo siyo yako. Sali na Mungu atakuonyesha mwenzi wako sahihi,” amesema Kapya.

“Mwanaume anahitaji kujua kuwa yeye ni kichwa na mke wake ni msaidizi wake kwani ameumbwa kutoka kwake. Ndoa nyingi zinavunjika kwa sasabu kizazi cha wanaume wa sasa hawachukui jukumu lao la kuihudumia familia,” Picha| freepik.com

Kwa mwanaume, ndoa ni wito kamili

Ndoa ni zaidi ya mali, zaidi ya mjengo na zaidi ya cheo lakini huenda hivyo vikabaki visaidizi katika kuipatia furaha ndoa yako japo siyo vya lazima.

Mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Magdalena Mandawa anaamini kuwa kwa mwanaume mwenye wito hahitaji chochote ili kuoa. 

Ni ule msukumo wa ndani ndiyo unasababisha kuoa na ataiweza ndoa yake hata iwe ina shida kiasi gani. Kwa mwanamke kikubwa ni kupata upendo wa kweli.

“Mara mwanaume mwenye wito wa ndoa anapokutana na mwanamke moja kwa moja huyo mwanaume ataweza kumpatia upendo mwanamke (hapa mwanamke lazima atahisi upendo wa dhati) basi hii inatosha sana kwa mwanamke kuolewa,” ameeleza Mandawa ambaye ndoa yake imedumu kwa miaka saba.


Soma zaidi:


Kwanini baadhi ya ndoa hazifanikiwi?

Miaka mitatu iliyopita, nilifanikiwa kuhudhuria harusi ya ndugu yangu wa karibu. Ilikuwa ni harusi kubwa na wageni waalikwa tulikula, tukarudia, na tukanywa hadi kusaza. Nguo za maharusi hazikuwa za bei ndogo bila kusahau zawadi kedekede ambazo wageni waalikwa tulizitoa kuwapongeza wapendwa wetu.

Mwezi mmoja  baada, nilipokea taarifa kuwa ndoa ile imevunjika na ni siku nyingi tu. Nilistaajabu ya firauni kabla ya kuyaona ya Musa!

Tatizo liko wapi? Kukosekana kwa mawasiliano baina ya mume na mke. Baada ya kuendelea kufuatilia chanzo cha kuvunjika ndoa hiyo, nilibaini kuwa ndugu yangu alikuwa na mtoto wa nje na mke wake alikuwa hajui.

Mjasirimali wa kukodisha magari, Jessie Francis amesema jambo lolote unalolifanya kabla na hata ukiwa kwenye ndoa, ongea na mwenzi wako.

“Mkikosana kaeni chini mutatue tatizo kwani mkilifumbia macho litaota mizizi na ni ngumu kuing’oa,” amesema Francis.


Kabla ya kuingia kwenye ndoa, usipuuzie haya 

Dondoo na Mjasiriamali wa kukodisha magari, Jessie Francis 

  • Mfanye mwenzi wako kuwa rafiki yako unayeweza kuwa huru kumwambia chochote unachojisikia kama unavyofanya kwa rafiki yako wa karibu (best friend)
  • Matatizo na mambo ambayo hapendi kwako na wewe haupendi kwake, yarekebisheni mapema kabla hamjaingia ndoani. Usiseme “nitavirekebisha ndoani”
  • Hakikisha unafahamu kiasi cha uvumilivu cha mwenzi wako kabla ya ndoa. Itakuwa rahisi kwako kufahamu ni kwa kiasi gani anaweza kukufaa katika changamoto mnazokutana nazo.
  • Pima kiwango cha upendo wako kama kinategemea vitu au utu. Kama umependa mtu kwa sababu ana vitu fulani, upendo wako utakoma pale vitu vivyo vitakapoisha au kuondoka. 
  • Usioe wala kuolewa kwa kutimiza wajibu yaani nimezaliwa, nimesoma nimepata kazi na natakiwa kuolewa au kuoa.

Mchango wa wazazi katika kujenga na kubomoa ndoa za watoto

Mara nyingi kinachojenga ndoa yoyote ni tabia baina ya wenzi. Endapo mwenzi mmoja ana tabia ambayo mwenzake hawezi kuvumilia, huenda ikiwa ni chanzo cha ugomvi na kutokuelewana katika ndoa.
Lakini endapo wenzi hao wakawa na tabia ambazo zinaendeana huenda maelewano ndani ya ndoa yakawepo.

Mpiga picha kutoka Jiji la Arusha Michael David amesema tabia ya mtu ikiwemo uvumilivu, uwezo wa kuongoza na usikivu vinaweza kuwa kiungo bora katika ndoa.

David ameiambia Nukta Habari kuwa wazazi wana mchango mkubwa katika malezi ya watoto wao tangu wakiwa wadogo na hivyo tabia ambazo mtu anakua nazo ndani ya ndoa, zinakuwa zinamchango mkubwa katika kuijenga ama kuibomoa ndoa hiyo.

Kwa maoni zaidi, tuandikie ujumbe kupitia namba +255 677 088 088

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW