Jinsi ya kubaini kamera zilizofichwa kwenye nyumba ya kupanga, chumba cha hoteli
- Fanya ukaguzi wa kawaida wa macho katika chumba unacholala.
- Tumia mwanga wa simu au programu tumishi za simu (Apps) zilizoundwa kubaini kamera hizo.
- Kumbuka, siyo maeneo yote kamera hizo huwekwa.
Ni dhahiri kuwa katika safari zetu tunalazimika kukaa hotelini kwa ajili ya mapumziko au shughuli za kikazi. Wakati mwingine tunakaa katika nyumba za kupanga kwa kipindi fulani wakati tukisubiri kujenga nyumba zetu.
Hoteli au baadhi ya nyumba za kupanga hufungwa kamera za usalama katika maeneo mbalimbali ikiwemo jikoni, sehemu za wazi ambazo zinajumuisha watu wengi kulingana na taratibu na kanuni za kiusalama za eneo husika.
Lakini ni nadra vyumba vya kulala vya hoteli au nyumba za kupanga kufungwa kamera hizo kwa ndani lakini inaweza kutokea na kuathiri faragha yako ambayo ni haki ya kila mwanadamu.
Sasa unawezaje ukabaini kamera ya usalama ambayo siyo rahisi kuonekana katika chumba chako cha hoteli au nyumba ya kupanga ikitokea imewekwa? Kuna baadhi ya mbinu zinazoweza kukusaidia kung’amua vifaa hivyo vya kieleketroniki vya kung’amua matukio.
Fanya ukaguzi wa kawaida
Hapa unatumia macho yako kuangalia mpangilio wa vitu katika chumba cha hoteli ulichofikia ikiwemo kona za kuta, dalini na hata taa za mezani na ukutani.
Hii ni njia rahisi na ya haraka ya kubaini vifaa unavyovitilia shaka lakini siyo watu wote wanakuwa na wazo la kukagua vyumba wanavyolala. Hii ni kwa sababu ni mara chache vitendo hivyo vya kuweka kamera katika maeneo hayo hufanyika na ikitokea ni kwa sababu za kiusalama zaidi.
Fanya ukaguzi wa kawaida wa macho katika chumba unacholala ili kubaini vitu visivyo vya kawaida. Picha|Mtandao.
Tumia mwanga wa simu yako
Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la Marekani CNN, kutumia mwanga wa simu yako ni njia nyingine rahisi ya kubaini kamera za video zilizofichwa.
Unachotakiwa kufanya ni kumulika kitu chochote ambacho siyo cha kawaida ikiwemo saa na vifaa vya kudhibiti moto na moshi.
Kutokana na maendeleo ya teknolojia, kamera hizo zinaweza kuwa katika maumbo tofauti na kuwekwa katika eneo ambalo siyo rahisi kugundua.
Soma zaidi:
- RC Makonda aagiza kamera, taa za usalama kufungwa kwenye maduka Dar
- Namna ya kupima ugonjwa rimoti kwa kamera ya simu
Tumia programu tumishi ya simu (App)
Unaweza kupakua apps za mtandaoni ambazo ni mahususi kwa ajili ya kubaini kamera zilizofichwa.
Apps hizo zinasaidia kusoma mawimbi ya sauti (Radio Frequency) ya vifaa vya kurekodia na kumjulisha mtumiaji uwepo wa kifaa husika na eneo kilipowekwa.
Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa kila nchi ina sheria zake za ufungaji wa kamera katika maeneo ya umma. Kwa mfano, kwa ajili ya kulinda faragha za watu, hairuhusiwi kuweka kamera katika vyumba vya kulala na chooni. Utaratibu uliopo sehemu nyingi ni kuweka kabisa ujumbe unaonyesha kuwa jengo husika linalindwa na kamera za usalama.
Lakini katika baadhi ya nchi, maafisa wa usalama wa Serikali zao hulazimika kufunga kamera hizo ili kufuatilia mienendo ya baadhi ya watu wanaotilia mashaka.
Apps hizo zinaweza kukusaidia kubaini mahali kamera ilipofungwa au kuwekwa. Picha| Mtandao.