Jinsi vijana wanavyoweza kuepuka presha ya kupata mafanikio

March 11, 2021 1:00 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Vijana wanatakiwa kuelewa kuwa mafanikio ni mchakato na siyo kushinda mchezo wa bahati na sibu.
  • Pia, kuepuka kuishi maisha nje ya uwezo kutawasaidia kuishi maisha mazuri, kuweka akiba na kuwekeza katika kitu unachokipenda.
  • Kuna haja ya mfumo wa elimu kuongeza msisitizo kuhusu vipaji na masomo ya stadi za kazi.

Dar es Salaam. Siku za hivi karibuni wakati nakuja ofisini, nilikaa karibu na kijana kwenye daladala. Mavazi yake yalionyesha utanashati wake huku akionekana kutokutaka kuzungumza na mtu yeyote kwani alikuwa ameweka “earphones masikioni” kiasi cha kutokusikia salamu yangu.

Macho hayana pazia bwana! Katika kuangaza angaza, macho yangu yalitua katika skrini ya simu yake na alikuwa anaandika ujumbe wa “WhatsApp status” akisema, “People dont post their failures on social media. Only success.” licha ya kuwa sipo katika kitabu chake cha mawasiliano, ujumbe huo ulinifikia pia.

Kwa tafsiri ya Kiswahili, ujumbe wake unamanisha, “Watu hawaposti madhaifu yao katika mitandao ya kijamii. Ni mafanikio tu.” jambo linalowafanya vijana kukimbilia mafanikio bila kujipanga. 

Mhandisi wa masuala ya usalama anayeishi Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Zamdazitta Kumbakumba ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kwa baadhi ya vijana, mafanikio “ni vile mtu anavyoonekana Instagram and kwenye mitandao mingine ya kijamii,” ikihusisha mavazi anayovaa, wapi anatembelea na mali anazomiliki.

Hata hivyo, kwa mhandisi huyo, mafanikio ni amani ya moyo na kuweza kutimiza baadhi ya majukumu yaliyopo ndani ya uwezo wako.

Vijana wafanye nini kuepuka presha/ msukumo usio wa kawaida wa kupata mafanikio kwa haraka?

Hakuna anayeposti madhaifu yake mtandaoni. mafanikio ni hatua kwa hatua. Picha| freepik.com. 

Maisha siyo mashindano

Licha ya kuwa baadhi ya watu hufanya maigizo mitandaoni ikiwemo kuposti vyakula vizuri, wakiwa katika maeneo ya kifahari na yenye kuvutia, huenda hayaakisi maisha ya halisi wanayoishi kwenye jamii.

Mtu kupiga picha kwenye nyumba nzuri haimaanisha kuwa ni ya kwake. 

Kwa mujibu wa Taurus Mangi, Mbunifu wa grafiki (picha), vijana wengi kinachoongeza pupa sio mafanikio halisi bali muonekano feki unaotengenezwa kwenye mitandao ya jamii.

Mzazi huyo wa watoto watano amesema, “wengi wanataka kuonyesha mafanikio ambayo hawana. Wanadanganyika na wenzao na hivyo kuishia kupata msongo wa mawazo unaopelekea kuanza kupaparika kutafuta mafanikio,” amesema Mangi.

Mangi ameshauri kujifunza kufanya ulinganifu kati ya kutafuta fedha, kuwa na amani na kufanya kile unachopenda. 

“Penye hela hamna furaha na penye furaha hapana mafanikio. Jifunze kubalance,” amesema Mangi.


Soma zaidi:


Amini kuwa pole pole ndio mwendo

Ninapenda kutumia methali ya “mji wa Roma haukujengwa kwa siku moja” kwani nina imani ya kuwa mafanikio hutafutwa hatua kwa hatua. Ni kama kujenga nyumba, leo utaanza na msingi, kesho ukuta na hatimaye utaezeka na kuhamia kwenye nyumba yako. 

Na pia, siyo rahisi kiasi hicho kwani katika ujenzi, kunakuishiwa pesa, utakopa kwa marafiki, utadaiwa, saruji zitapanda bei. Kuna kuibiwa vifaa ni changamoto ambazo haziwezi kuisha lakini hatimaye, nyumba itakamilika na siyo kwamba ndiyo ujenzi utakua umeisha kwani utakuwa unarekebisha mabomba, utabadilisha taa na kadhalika. Hivyo ndivyo maisha yalivyo.

Mjasiriamali na mkazi wa Dar es Salaam, Neema Simbo ameshauri kuwa baada ya kumaliza masomo,  ni  vyema kuwa na mipango maalum ya kukubaliana na uhalisia wa maisha. 

“Kama hauna pesa, likuballi hilo na hakuna sehemu iliyoandikwa kuwa unapaswa kuwa umefanikiwa kwa umri ulionao. Pangilia maisha yako, kuwa mvumilivu na acha kujipa msongo wa mawazo kwa vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wako,” ameshauri Simbo.

Ishi, weka akiba, fanya unaloliweza

Baadhi ya vijana wamekuwa na presha ya maisha kwa kutaka kufanya vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wao. Watataka kumiliki gari ilhari hata llikipata ajari leo, litapaki wiki nzima bila kurekebishwa.

Wanataka kwenda kwenye migahawa ya gharama ilhari watashangaa bei ya chipsi kavu iliyopo kwenye menyu.

Ili kuepukana na hayo yote, zingatia kuishi ndani ya uwezo wako, weka akiba pale unapopata fedha kwani itakusaidia katika dharura. Usilazimishe kufanya kitu ambacho hauwezi kukifanya kifedha na kuishia kuwa na madeni usiyoweza kuyalipa.

Msimamizi wangu wa kazi (mentor) aliwahi kuniambia, kila sekunde ya maisha yako inahesabika na hauwezi kuipata tena. 

“Unaweza kukuta katika kipindi hiki ndicho kipindi umeandikiwa kuwa na fedha kuliko kipindi chochote katika maisha yako. Kesho hauijui, unapopata pesa, weka akiba kwa ajili ya kesho, wekeza katika vitu unavyovipenda na pata muda wa kufurahi,” ni maneno yake ambayo sijayasahau mpaka sasa. 

Mafanikio ni kama kujenga nyumba, leo utaanza na msingi, kesho ukuta na hatimaye utaezeka na kuhamia kwenye nyumba yako. Picha| freepik.com.

Ni wakati wa kubadili mfumo wa elimu

Vijana kuwa hivi huenda ni sababu ya mtizamo walionao ambao umejengwa na mfumo wa elimu huku wengi wakiamini kuwa baada ya elimu ni ajira na wanapaswa kulipwa mishahara minono. Inapokuwa sivyo, ndipo tafrani inaanza.

Mtaalamu wa masuala ya teknolojia ya mawasiliano Jensen Seth amesema, mfumo wa elimu haujaweka ulazima au umakini katika kukuza vipaji vya wanafunzi na hivyo kusababishwa vijana kuangalia mifumo rasmi ya ajira.

Anasema kuna umuhimu wa mitaala ya elimu kusisitiza na kuviendeleza vipaji na stadi za kazi ambazo vijana wanaweza kutumia kuboresha maisha yao.

“Serikali ingetengeneza mfumo wakati mtu anasoma lazima awe na somo la ziada la kipaji chake au michezo nje ya somo la kawaida na kuwe na semina za ufundishaji kutengeneza vitu vya kawaida kama kushona, upishi na mengineyo,” amesema Seth.

Zaidi ya hapo, zingatia hili

Naye Mwanasaikolojia Josephine Tesha ameshauri vijana kuwa makini na maisha yao na kuacha kufata mikumbo, kupunguza tamaa, kupanga mipango yao bila kuyumbishwa na kujua wanachotaka na kukifanyia kazi. 

“Utafikia malengo yako na kupata mafanikio unayoyataka kama utakuwa ni mtu wa kujielewa. Wanachoshindwa kuelewa hakuna shortcut ya kufikia mafanikio, kama unataka kupata mafanikio ni lazima ufanye kazi kwa bidii sana,” amesema Tesha.

Enable Notifications OK No thanks