Je, Black Mamba ndiye nyoka hatari zaidi duniani ?
- Ndiye nyoka mwenye kasi kubwa zaidi duniani, akiwa na uwezo wa kukimbia kwa mwendo wa kilomita 20 kwa saa, kasi inayomzidi hata binadamu wa kawaida.
Dar es Salaam. Anatajwa kuwa na uwezo wa kukimbia kwa kasi ya hadi kilomita 20 kwa saa, anaweza kufikia urefu wa hadi futi 12, na sumu yake huweza kusababisha kifo ndani ya dakika 20.
Huyu ndiye koboko au jina maarufu Black Mamba, nyoka ambaye kwa muda mrefu amehusishwa na simulizi nyingi za kutisha barani Afrika ikiwemo zinazodai kuwa nyoka huyo hamgongi binadamu mahali pengine popote isipokuwa kichwani.
Lakini je, ni kweli kuwa ndiye nyoka hatari zaidi duniani? Fuatana nami kwenye makala hii.

Katika jamii nyingi za Kiafrika, Black Mamba amekuwa sehemu ya hekaya mbalimbali ikiwemo ile ya mtu aliyeumwa na nyoka huyu hufa kabla ya kupiga hatua saba.
Lakini mbali na hofu inayozunguka jina lake, utafiti wa kisayansi umeweka bayana ukweli kuhusu uwezo na hatari halisi ya mnyama huyu.
Asili yake
Kisayansi, nyoka huyu anajulikana kama Dendroaspis polylepis. Ingawa wengi hufikiri ana rangi nyeusi kutokana na jina lake, Black Mamba ana ngozi ya kahawia na jina lake linatokana na rangi nyeusi ya ndani ya mdomo wake, ambao huufungua kwa ghadhabu anapohisi tishio.
Kwa mujibu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, nyoka huyu ana urefu unaoweza kufikia futi nane hadi 12 na anaishi kwa wastani wa miaka 11. Kichwa chake kinafanana na jeneza, jambo ambalo huongeza mvuto wa hadithi kuhusu kutisha kwake.
Kwa mujibu wa Sara Viernum, mtaalamu wa herpetolojia, Black Mamba ndiye nyoka mwenye kasi kubwa zaidi duniani, akiwa na uwezo wa kukimbia kwa mwendo wa kilomita 20 kwa saa, kasi inayomzidi hata binadamu wa kawaida.

National Geographic inabainisha kuwa nyoka huyu hupatikana katika maeneo ya savanna na miamba barani Afrika, hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, ukiwemo Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Msumbiji na Afrika Kusini.
Swali ambalo wengi hujiuliza ni kama kweli Black Mamba ndiye nyoka hatari zaidi duniani.
Hatari yake
Ingawa si nyoka mwenye sumu kali zaidi duniani (nafasi hiyo hushikiliwa na Inland Taipan wa Australia), Black Mamba hutajwa kuwa miongoni mwa nyoka hatari zaidi kwa binadamu kutokana na sababu kuu tatu: kasi kubwa ya kusambaa kwa sumu mwilini, tabia ya kushambulia zaidi ya mara moja, na ugumu wa upatikanaji wa dawa ya kuzuia sumu katika maeneo ya vijijini.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani watu 20,000 hufariki kila mwaka barani Afrika kutokana na kung’atwa na nyoka, na sehemu kubwa ya vifo hivyo hutokea katika nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika, ambako Black Mamba hupatikana kwa wingi.
Sumu ya Black Mamba ina mchanganyiko wa kemikali hatari zikiwemo neurotoxins zinazodhoofisha mfumo wa fahamu, na cardiotoxins zinazoshambulia moyo.
Mara sumu inapoingia mwilini, huanza kazi ndani ya muda mfupi sana na inaweza kusababisha kupooza kwa viungo, kushindwa kupumua, au hata kufa moyo.

Bila matibabu ya haraka, mtu aliyeumwa anaweza kupoteza maisha ndani ya dakika 20 hadi 30, hali inayofanya nyoka huyu kuwa hatari mkubwa hasa maeneo yasiyo na huduma za haraka za afya.
Tofauti na nyoka wengine, Black Mamba huinua hadi robo tatu ya mwili wake kutoka ardhini anapojihami, na huweza kung’ata adui mara kadhaa kwa haraka.
Ana uwezo wa kutoa sauti kali ya hofu kama njia ya kujihami kabla ya kushambulia. Hii huongeza uwezo wake wa kujiokoa dhidi ya adui yoyote anayemkaribia kwa hila au kwa bahati mbaya.
Kwa upande wa chakula, Black Mamba hula ndege na mamalia wadogo kama vile panya.
Akiwa na taya zenye uwezo wa kutanuka mara nne zaidi ya ukubwa wake wa kawaida, anaweza kuwameza kwa urahisi wanyama waliokwisha fariki kutokana na sumu yake.
Uzazi wake
Nyoka huyu huzaliana mara moja kwa mwaka wakati wa msimu wa joto au mvua. Dume hupambana ili kujamiiana na jike, na baada ya kushiriki tendo la ndoa, jike hutaga mayai kati ya sita hadi 25 mahali penye unyevu na joto la wastani.
Baada ya miezi mitatu, mayai huenguliwa na watoto huzaliwa wakiwa na urefu wa kati ya nchi 16 hadi 24. Tofauti na wanyama wengine, Black Mamba jike huwaachia watoto wake kujitegemea mara moja bila msaada wowote.

Ingawa Black Mamba si nyoka mwenye sumu kali zaidi duniani, mchanganyiko wa kasi, sumu kali na uwezo wa kushambulia zaidi ya mara moja unamfanya kuwa hatari halisi kwa binadamu.
Hadithi na hekaya zimeongeza hofu juu yake, lakini takwimu na tafiti za kisayansi zinathibitisha kuwa tahadhari dhidi ya nyoka huyu ni jambo la msingi, hasa kwa watu wanaoishi maeneo ambako huonekana mara kwa mara.
Latest



