Jamhuri ya Korea kuikopesha Tanzania Sh 6.5 trilioni

June 3, 2024 5:36 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Fedha hizo zinatolewa chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi wa Serikali ya Korea (EDCF).

Dar es Salaam. Tanzania imesaini tamko la pamoja la kuanzisha Mkataba wa Ushirikiano wa Uchumi (EPA) na Jamhuri ya Korea utakaoiwezesha kupata mkopo wa Sh6.5 trilioni katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2024 hadi 2028.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Fedha hizo kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya maendeleo zinatolewa chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi wa Serikali ya Korea (EDCF).

Mikataba hiyo imesainiwa leo Juni 2, 2024 nchini Korea ambapo Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Yoon Suk Yeol wa Jamhuri hiyo wameshuhudia tukio hilo.

Kusainiwa kwa tamko la kuanzishwa kwa mkataba huo kunaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu barani Afrika ambazo zitafanya majadiliano hayo yatakayozaa mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Korea. 

Nchi zingine zilizopo katika nafasi ya kufanya majadiliano hayo barani Afrika ni Morocco na Kenya.


Soma zaidi:Mapato yatokanayo na utalii wa kitaifa, kimataifa yapaa Tanzania


Kupitia mkataba wa EPA Tanzania na Korea Kusini zitashirikiana kimkakati hususan katika nyanja za biashara, uwekezaji, viwanda, usafirishaji na nyinginezo.

Mbali na mkataba huo pia Tanzania na Korea zimesaini Hati za Makubaliano (MOU) mbili ambazo ni pamoja na ushirikiano katika uchumi wa buluu ambapo Tanzania itashirikiana na nchi hiyo katika maeneo ya uvuvi, viwanda vya kuchakata mazao ya bahari, ujenzi wa bandari za uvuvi, teknolojia na tafiti za masuala ya bahari. 

Vile vile, Wizara ya Madini ya Tanzania na Wizara ya Biashara, Viwanda na Nishati ya Korea Kusini zimetia saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika madini ya kimkakati.  

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na Waziri wa Biashara wa Korea Inkyo Cheong wakisaini Tamko la Pamoja la kuhusu Uanzishwaji wa Majadiliano juu ya Mkataba wa Ushirikiano Kiuchumi EPA.PichaIkulu Mawasiliano/X (Twitter).

Makubaliano hayo yataziwezesha nchi hizo shirikiana katika utafiti, uwekezaji, uchimbaji na kujenga uwezo wa kuongeza thamani ya madini ya kimkakati nchini Tanzania ikiwemo madini ya Nickel, Lithium na Kinywe.

Wakati huo huo, Rais Samia amependekeza ushirikiano wa sekta nyingine mpya zikiwemo maendeleo ya nishati ya gesi asilia; sekta ya Ubunifu ikiwemo sanaa na filamu na kufunguliwa kwa soko la ajira la nchini Korea kwa vijana wa Tanzania kupitia mpango wa Employment Permit System (EPS).

Enable Notifications OK No thanks