Internews, Nukta Africa wafungua fursa ya mafunzo kwa wanahabari Tanzania

September 16, 2019 2:33 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mafunzo ya uthibitishaji habari (Fact Checking) yatakayofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam.
  • Yanalenga kuongeza ujuzi wa kukabiliana na habari za uzushi zinazosambaa kwa kasi zaidi duniani kwa sasa.
  • Wanahabari wanawake wahimizwa kuchangamkia fursa hiyo. 

Dar es Salaam. Wanahabari waliokuwa wakisaka maarifa ya uthibitishaji taarifa (Fact Checking) sasa wana sababu ya kutabasamu baada ya Shirika lisilo la Kiserikali la Internews kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia na habari ya Nukta Africa kuzindua mafunzo ya siku tatu ya namna ya kukabiliana na habari za uzushi. 

Mafunzo yamelenga kuwawezesha wanahabari nchini kuandika habari kwa ubora na kuepuka kuchakata taarifa za uongo ambazo zimeongezeka kwa kasi zaidi siku za hivi karibuni kutokana na ukuaji wa matumizi ya mitandao ya kijamii.

Mafunzo hayo, yatakayotolewa na Internews na Nukta Africa, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Boresha Habari unaofadhiliwa na Shirika la Misaada kutoka kwa Watu wa Marekani (USAID). 

Taarifa iliyotolewa na Nukta Afrika leo (Septemba 16, 2019) inaeleza kuwa mafunzo hayo ya siku tatu yatafanyika katika kituo cha kijamii cha Internews Media Lab, Jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 30 hadi Oktoba 2, 2019.

“Mabadiliko ya teknolojia ya habari hususan mitandao ya kijamii yamechangia kwa kiwango kikubwa usambazaji wa habari za uzushi nchini na duniani kote,” amesema Alakok Mayombo, Mkufunzi Mwandamizi wa Internews nchini na kubainisha kuwa,  

“Habari hizi za uzushi baadhi zinapenyeza hadi kwenye mfumo wa vyombo vya habari na kuzidi kusambaza uongo ambao kuna wakati unaweza kusababisha hata vifo.” 

Amesema Internews imeamua kutoa mafunzo hayo kwa wanahabari nchini kwa kuwa vyombo vya habari vinatakiwa kutoa habari za ukweli na kuzingatia viwango vya juu vya maadili.


Soma zaidi: 


Miongoni mwa masuala ambayo wanahabari hao watajifunza ni namna ya kubaini uhalali wa machapisho mtandaoni kama Twitter, Facebook, mbinu za kisasa za uthibitishaji taarifa ikiwamo kujua historia ya uchapishaji habari wa tovuti mbalimbali tangu zilipoanzishwa.

Mkurugenzi Mtendaji na Mhariri Mkuu wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema mafunzo hayo yatajumuisha mbinu za uthibitishaji taarifa zinazoendana na teknolojia ya kisasa ya akili bandia (artificial intelligence). 

“Mafunzo ya aina hii mara nyingi hutolewa zaidi kwenye nchi zilizoendelea lakini kwa sasa tunayafanya nyumbani kwa kutumia mbinu na teknolojia zile za wenzetu wa ng’ambo. Hii ni fursa adimu kwa wanahabari wenzangu kujifunza zaidi kwa kuwa maarifa hayazeeki,” amesema Dausen.

Ili upate fursa ya kuwa miongoni mwa Wanahabari 10 watakaokuwa na sifa ya kupata mafunzo hayo unatakiwa kutuma maombi yako hapa. Mwisho ya kutuma maombi ni Septemba 21,  2019 Saa 5:59 usiku.

Wanahabari wanawake watapewa kipaumbele zaidi, hivyo ni wakati kwa wanawake waliopo katika tasnia ya habari kuchangamkia fursa hii ambayo gharama zote za mafunzo zitagharamiwa na waandaaji. 

Enable Notifications OK No thanks