INEC yatangaza idadi mpya ya vituo, wapiga kura

October 7, 2025 1:41 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Vituo vya kupigia kura vyafikia 99,895 idadi iliyopungua kidogo kutoka 99,911 vilivyotangazwa awali.

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku 22 kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza mabadiliko mapya ya takwimu za wapiga kura na vituo vya kupigia kura vitakavyotumika katika uchaguzi huo.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima iliyotolewa leo Oktoba 9, 2025, imeeleza kuwa mabadiliko hayo yamejitokeza baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki na uchakataji wa taarifa za wapiga kura waliopo katika daftari hilo la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

“Idadi ya wapiga kura walioandikishwa ni 717,557 na idadi ya vituo vya kupigia kura ni 1,752,’’ inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hii ya INEC inakuja ikiwa ni siku 73 toka itangazwe idadi ya awali ya wapiga kura na vituo vya kupigia kura Julai 26, 2025.

Wapiga kura zaidi ya milioni 37 kuhusika

INEC imesema kuwa jumla ya wapiga kura walioandikishwa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ni 37,647,235, idadi ambayo ni ndogo kidogo ikilinganishwa na takwimu za awali zilizokuwa 37,655,559.

Kati ya wapiga kura hao, 36,650,932 wapo Tanzania Bara na 996,303 wapo Tanzania Zanzibar.

Hata hivyo, tume imeeleza kuwa idadi hiyo inaonyesha ongezeko la asilimia 26.53 ikilinganishwa na wapiga kura 29,754,699 waliokuwa wameandikishwa mwaka 2020.


Katika wapiga kura hao wanawake ni 18,950,801 sawa na asilimia 50.34 ya wapiga kura wote huku wanaume wakiwa 18,696,439  sawa na asilimia 49.66.

Vituo vya kupigia kura vyafikia 99,895

Aidha, kwa upande wa vituo vya kupigia kura, INEC imetangaza kuwa jumla ya vituo vitakavyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ni 99,895, idadi iliyopungua kidogo kutoka 99,911 vilivyotangazwa awali.


Katika vituo hivyo, Tanzania bara itakuwa na jumla ya vituo 97,348 huku Zanzibar ikiwa na vituo 2,547. Idadi hiyo mpya ni ongezeko la asilimia 22.47 ikilinganishwa na vituo 81,567 vilivyotumika kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Kwa mujibu wa kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, uandikishaji wa wapiga kura upande wa Zanzibar unazingatia sheria ya Baraza la Wawakilishi, na daftari la wapiga kura la ZEC litakuwa sehemu ya daftari la kitaifa litakalotumika kwenye uchaguzi wa Rais na Wabunge upande wa Zanzibar.

Sanjari na hilo, INEC imetangaza kuwa itavipatia vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 orodha ya vituo vya kupigia kura vitakavyotumika katika uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Kwa upande wa Zanzibar, zoezi la kupiga kura ya kuchagua Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani itafanyika Oktoba 29 mwaka huku Oktoba 28 ikiwa siku ya kura ya mapema.

Watakaopiga kura ya mapema ni watendaji wanaosimamia majukumu ya uchaguzi mkuu, wakiwemo wasimamizi wa uchaguzi, wasaidizi wa wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wa vituo, polisi watakao kuwa kazini siku ya uchaguzi, wajumbe wa tume ya uchaguzi pamoja na watendaji wa tume na wapiga kura ambao watahusika na kazi ya ulinzi na usalama siku ya uchaguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks