IMF yatabiri mdororo wa uchumi, Corona ikisambaa duniani

March 25, 2020 7:06 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Wawekezaji tayari wameondoa dola bilioni 83 kutoka kwenye masoko ya nchi zinazoibuka kiuchumi.
  • Yasema mdororo utakuwa kwa muda mfupi lakini mwaka 2021 hali itatengamaa. 
  • Benki Kuu zatakiwa kulegeza sera za kifedha ili kuokoa uchumi wa dunia.

Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeonya kuwa hatua madhubuti zisipochukuliwa kumaliza ugonjwa virusi vya Corona (COVID-19), dunia inaweza kuingia katika mdororo wa uchumi kama ule wa mwaka 2008. 

Mdororo uchumi wa mwaka 2008 huko Marekani na Ulaya Magharibi ulihusishwa na kile kilichoitwa janga la marejesho ya mikopo ya nyumba ambapo benki zilikopesha fedha wanunuzi wa nyumba ambao hawakuwa na historia nzuri ya kurejesha mikopo na hivyo benki kufikilisika.

Mkurugenzi Mtendaji wa IMF Kristalina Georgieva amesema hayo alipohutubia kwa njia ya video katika mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka kundi la mataifa 20 (G20).

“Gharama ya kibinadamu kutokana na COVID-19 tayari haipimiki na kwamba mataifa yanapaswa kushirikiana kulinda watu wake na kudhibiti madhara ya kiuchumi. Huu ni wakati wa mshikamano,” amesema Georgieva katika taarifa shirika hilo iliyotolewa jana (Machi 26, 2020).

Amesema ikiwa hatua za kudhibiti ugonjwa huo zitaimarishwa basi, dunia inaweza kujikwamua katika mdororo wa kiuchumi ifikapo mwaka 2021.

“Kwa mwaka huu wa 2020 ni hasi, mdororo ambao angalau ni mbaya  kama ilivyokuwa wakati wa janga la kifedha duniani au mbaya zaidi. Lakini tunatarajia kukwamuka mwaka 2021,” amesema bosi huyo wa IMF na kuongeza kuwa,

“Tunaunga mkono kwa dhati hatua za kipekee za kifedha zinazochukuliwa na mataifa mengi ambayo tayari yamechukua hatua kuimarisha mifumo ya afya na kulinda wafanyakazi kazi walioathirika.”

Amesema nchi zilizo mbele kiuchumi ziko katika nafasi nzuri ya kukabiliana na janga la COVID-19 ilhali nchi zinazoibuka kiuchumi zinakabiliwa na changamoto ya kuondoka kwa mitaji na shughuli za ndani kiuchumi zimedorora kwa kuwa zinakabiliana na janga la Corona. 


Soma zaidi: 


Tangu kuanza kwa corona, amesema wawekezaji tayari wameondoa dola bilioni 83 (Sh191.5 trilioni) kutoka kwenye masoko ya nchi zinazoibuka kiuchumi, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa.   

Kutokana na hali hiyo wanawasiliana na Benki ya Dunia kusaka suluhu ya jambo hilo kwani linawatia hofu kubwa.

Aidha, amesema wanakaribisha hatua za Benki Kuu za kulegeza sera za kifedha akisema kuwa hatua hizo ni si kwa maslahi ya nchi husika pekee bali pia kwa uchumi wa dunia nzima na kwamba hata zaidi za aina hiyo zitahitajika.

“Tutakusanya fedha za dharura. Takribani mataifa 80 yameomba msaada wetu na tunashirikiana na taasisi nyingine za fedha za kimataifa ili kuwa na suluhu inayoratibika na itakayokuwa na manufaa makubwa,” amesema Mkurugenzi Mwendeshaji huyo wa IMF.

Ameongeza kuwa hivi sasa wanajazia mfuko wa kujenga unafuu kwa majanga ili kusaidia nchi maskini zaidi na wanakaribisha wale ambao tayari wameahidi huku akitoa wito kwa wengine kusaidia. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW