Ifahamu ‘paradiso’ ya baharini iliyopo Kaskazini mwa Tanzania

February 20, 2020 9:20 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Paradiso hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 552.
  • Kati ya kilometa hizo, kilometa za mraba 85 tu zipo nchi kavu huku zilizosalia zikiwa baharini.
  • Jjina lake ni samaki aliyesadidkika kutoweka duniani miaka milioni 65 iliyopita.

Dar es Salaam. Inawezekana umesikia mengi kuhusu mkoa wa Tanga. Stori za mapenzi, viwanda miaka ya nyuma na hata “pepo” ya Magoroto iliyopo wilaya ya Muheza. Hata hivyo,  kwa namna moja ama nyingine, Hifadhi ya Bahari ya Silikanti- Tanga (Hibasita) inaweza kuwa kitu kigeni maskioni mwako.

Hifadhi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2009,  jina lake limetokana na uwingi wa samaki aina ya Silikanti (Coelacanth) ambaye alidaiwa kutoweka duniani zaidi ya miaka milioni 65 iliyopita. 

Usichokijua kuhusu tabia ya Silikanti ni ukubwa wake unaoweza kufikia futi 6.2 huku makazi yake yakiwa ni kwenye mapamgo ya baharini yaliyopo kwenye urefu wa hadi mita 500.

Samaki aina ya Silikanti alitangazwa kutoweka kwenye uso wa dunia kwa miaka zaidi ya milioni 65 iliyopita. Picha| Bodi ya Utalii ya Tanzania (TTB).

Hisabita ambayo kwa mujibu wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania ni hifadhi ya baharini yenye ukubwa wa kilometa za mraba 552 huku kilometa za mraba 85 pekee zikiwa nchi kavu.

Ukiwa kwenye hifadhi hii utafurahia kuwaona samaki hao ambao walidaiwa kupotea huku sauti za Pomboo almaarufu kama “dolphin” zikiburudisha masikio yako. Kama hujawahi kuwaona, hii ni nafasi yako wakati ukiwa katika mapumziko.

Pia, kama hujawahi kuwaona Kasa utapata nafasi ya kutembelea vituo vya kutotoleshea mayai ya kobe huyo wa baharini sanjari na kupumzika kwenye bustani za matumbawe zilizopo kwenye miamba ya Shengue, Upangu, Kitanga, Taa na maziwe zikikusubiri.

Haijaishia hapo! magofu yaliyopo kwenye kisiwa cha Toten na Tongoni na mabaki ya kihistoria ya Ndumi ni vivutio utakavyoviona pia.


Gharama na tozo

Ili kufurahia utalii wa kwenye fukwe safi, kuogelea kwa kutumia vifaa maalumu yaani “snokering and diving” ama kufurahia maji ukiwa kwenye boti na uvuvi wa burudani itakuhitaji utoboe mfuko kidogo.

Usiogope! Kama ni Mtanzania, ulipia Sh2,360 endapo una miaka zaidi ya 15. Chini ya miaka hiyo ni Sh1,180  na mtoto wako ama ndugu mwenye miaka chini ya mitano hatotozwa chochote.

Kama mgeni, utahitaji Sh54,508 kama una miaka zaidi ya 15 na kama ni chini ya hapo, Sh27,254 itakuhusu huku ndugu ama mwanao mwenye miaka chini ya hapo akifurahia uzuri huo bila tozo.

Fahamu kuwa gharama hizo hazihusiani na tozo za hotelini lakini endapo utahitaji kuweka kambi kwenye hifadhi hii kwa usiku mmoja, mtu mmoja atahitajika kulipia Sh54,280 na kama utahitaji kuchukua video na picha kwa shughuli za biashara, Sh2.71 milioni itakutoka kwa kufidia siku saba.


Zinazohusiana


Unafikaje? 

Hauwezi kufika kimazingaombwe. Baada ya kutumia masaa mawili kwenye usafiri wa ndege kutokea Jiji la Dar es Salaam ama masaa matano kwa usafiri wa basi utakuwa umefika kwenye pepo hii. 

Endapo utahitaji kupumzika kwenye hoteli, huduma hizo zipo zikiwemo hoteli ya Royal Naivera, Mapumziko ya Peponi beach na nyinginezo zilizopo maeneo ya jirani. 


 Uvuvi haramu unavyotishia vivutio vya baharini

Pamoja na vivutio vya utalii vya habari kuwa maarufu siku za hivi karibuni bado zinakabiliwa na tishio la uharibifu wa mazingira kutokana na uvuvi haramu. 

Uvuvi haramu ambao unaishia kuharibu bustani za matumbawe na kuua mazalia ya samaki na kuchafua bahari.

Serikali kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2018,  iliendesha operesheni katika Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi na kukamata mabomu ya milipuko 720 na vifaa vingine vikiwemo V-6 explosive (600), detonators (360), mbolea ya urea kilo 324, mitungi ya gesi (68), vifaa vya kuzamia jozi 252 na compressors ambazo hutumiwa kuharibu uzuri huo.

Safari yangu na wewe imeishia hapa. Hadi siku nyingine kwenye Nukta Safari, kwaheri.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW