Ifahamu historia Land Rover, Tanzania ikijiandaa kuweka rekodi mpya Guinness

October 11, 2024 6:30 pm · Daniel Mwingira
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Jiji la kitalii la Arusha linatarajia kuvunja rekodi ya dunia ya Guinness kupitia tamasha la tatu la ‘Land Rover’ baada ya kupita miaka sita tangu ilipowekwa rekodi mpya. 

‘Guinness’ ni Mamlaka ya Kimataifa ambayo huwatambua watu walioweka rekodi mpya au kuvunja zilizokuwepo duniani, ambazo huitwa Rekodi za Dunia za Guiness ambazo baadae huingizwa katika kitabu cha rekodi.

Paul Makonda, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameandaa tamasha la Land Rover linalotarajiwa kuhusisha magari 1,000  yatayokuwa na msafara wenye urefu wa kilomita 12.

Kwa sasa rekodi hiyo ya dunia inashikiliwa na Mji wa Spa Town Bad Kissingen uliopo Bavaria, Ujerumani, kupitia tamasha la Land Rover lililofanyika mwaka 2018 na kukutanisha magari 632 yaliyokuwa na msafara wenye urefu wa kilomita 7.4 ambayo ni ya pili baada ya iliyowekwa Ureno mwaka 2014. 

Tamasha la Land Rover litalofanyika Oktoba 12 hadi 14 mwaka huu sio tu litaleta pamoja wamiliki wa magari hayo maarufu kwa uimara na ufahari bali litachangia kukuza utalii wa ndani ambapo Arusha ni miongoni mwa vitovu vya utalii nchini. 

Tamasha hili litahusisha vizazi (generations) vya Land Rover, kuanzia Land Rover Series108, 109, 110 Range Rover Classic, Defender ya zamani, Defender ya kisasa, Range Rovers, Discoveries, pamoja na Freelanders. 

Lakini je, unajua kuhusu vizazi (generations) vya Land Rover?

Miaka ya mwanzo (1948-1970)

Land Rover unayoiona leo ni matokeo ya mbunifu Maurice Wilks, ambaye mwaka 1947 alichora muundo wa gari la kwanza katika pwani ya Wales, akitumia mfano wa Willys Jeep, gari lililotumika sana wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Ingawa gari hilo la awali lilibuniwa kwa matumizi ya kilimo na viwanda, Wilks aliliona kama chombo cha burudani katika maeneo magumu. 

Tarehe 30 Aprili 1948, Land Rover ya kwanza, Series I, ilizinduliwa rasmi kwenye maonesho ya magari ya Amsterdam. Gari hili liliundwa kwa muundo rahisi na wa kikazi.

Mwaka mmoja baadaye, Land Rover ilianzisha muundo mpya wa gari uitwao Station Wagon, ulioandaliwa na kampuni maarufu ya Tickford, inayojulikana kwa kushirikiana na chapa kama Rolls-Royce na Lagonda.

Series II ilianzishwa mwaka 1958 kama mrithi wa Series I ya awali. Series IIA, iliyozinduliwa mwaka 1961 na kuendelea kuzalishwa hadi mwaka 1971, ikawa maarufu zaidi katika safu ya Series II.

Gari hili lilipatikana aina tofauti pamoja na toleo maarufu la 88 Soft-Top. walengwa wakuu walikuwa wakulima na wanajeshi, kutokana na uimara wake na uwezo wake wa kuvuka maeneo magumu.

Kipindi cha upanuzi na ubunifu (1970-2000)

Kati ya miaka ya 1970 hadi 2000, Land Rover ilikua kwa kasi, ikipanua bidhaa zake na kuanzisha ubunifu mpya. 

Kipindi hiki ndio kulizinduliwa kwa Range Rover Kizazi cha Kwanza na kulionesha mwanzo wa enzi mpya kwa Land Rover ambayo iliendelea kudumisha sifa yake kama mtengenezaji wa magari imara na ikawa chaguo maarufu kwa ya watalii, wachunguzi na watu wanaopenda kusafiri.

Range Rover ilikuwa moja ya SUV (Sport Utility Vehicle ) za kwanza kutengezwa kwa kiwango cha kisasa na chenye anasa, ikiwa na viti vya ngozi, kiyoyozi, na vifaa vingine vya anasa.

Katika kipindi hiki, Land Rover ilinunuliwa na BMW, ambayo iliwekeza sana katika maendeleo ya miundo mipya na teknolojia. Hii ilisababisha uzinduzi wa kizazi cha kwanza cha Discovery mwaka 1989.

Kipindi cha usasa 

Enzi ya kisasa ya Land Rover ni kipindi ambacho gari hizo zilibadilika kutoka kuwa gari la wakulima, wanajeshi na linalotumiwa kwa kazi ngumu pekee hadi kuwa kivutio kwa kundi jipya la wateja ikiwemo wanamichezo, wanamitindo, na wasanii.

Katika miaka ya 2000, Land Rover ilishuhudia mabadiliko makubwa katika muundo wa magari yake ikiwemo kuzinduliwa kwa Range Rover Sport kizazi cha kwanza mwaka 2005.

Range Rover Evoque iliyotolewa mwaka 2011 ilifanya mabadiliko makubwa zaidi gari hii ililenga watu waishio mijini na wenye uwezo kifedha na imekuwa ikijizolea umaarufu mkubwa maeneo mbalimbali ikiwemo hapa Tanzania.

Mpaka sasa baadhi ya watu hununua gari za Land Rover kwa kuamini ni imara zaidi na ishara ya ufahari, tamasha la magari hayo itakuwa fursa ya kushuhudia vizazi vyote vya Land Rover kwa watu ambao hawakupata nafasi ya kuyaona magari hayo toka zamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks