Rais Samia ausia amani kujiandikisha daftari la wapiga kura Serikali za Mitaa 2024
- Asema zoezi hilo la kujiandikisha na kupiga kura ndilo linalobeba taswira ya uchaguzi mkuu 2025.
- Aeleza sababu ya Serikali kuichagua Novemba 27 kuwa siku ya uchaguzi.
Arusha. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kujitokeza na kujiandikisha katika daftari la wapiga kura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utaofanyika Novemba 27, 2024, huku akisisitiza amani na utulivu wakati wa mchakato huo.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza baada ya kujiandikisha katika daftari la wapiga kura leo Oktoba 11, 2024 katika Kijiji cha Chamwino mkoani Dodoma amesema zoezi hilo la kujiandikisha na kupiga kura ndilo linalobeba taswira ya uchaguzi mkuu 2025.
“Niwaombe sana zoezi lifanywe kwa usalama lifanywe kwa amani ili tusitie doa kwenye nchi nchi yetu, tumalize chaguzi zetu za awali hizi salama…
….nataka niwakumbushe zoezi hili ndilo linalotoa taswira ya uchaguzi ule mkubwa tunaokwenda nao, niwaombe sana wananchi twendeni tukachague vyema ili tupate taswira halisi ya kule tunapokwenda,” amesema Rais Samia.
Zoezi la kujiandikisha katika daftari la kupiga kura la Serikali za Mitaa litafanyika kwa siku tisa kuanzia leo Oktoba 11 hadi Oktoba 20, 2024.
Mara baada ya zoezi la kujiandikisha, litafuata zoezi la kampeni kwa siku saba na kisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27 mwaka huu zoezi linalotarajiwa kufanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 10 jioni.
Aidha, Rais Samia ameeleza sababu za Serikali kuichagua siku ya Jumatano ya Novemba Novemba 27 kuwa siku ya uchaguzi ikiwemo kutokuwa siku ya ibada kwa madhehebu yote nchini.
“Tumechagua jumatano kwa sababu Waislamu wanakwenda msikitini Ijumaa, Wasabato Jumamosi, Wakristo wengine waliobaki ni Jumapili, Jumatano ni yetu sote,itakuwa siku ya uchaguzi wetu naitakuwa siyo siku ya kazi tutaitangaza ili watu wote wapate nafasi waende kupiga kura,” ameongeza Rais Samia.