Gambo akubali yaishe, afuta kauli na kuomba radhi

April 24, 2025 11:01 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Aomba radhi na kutaka kauli yake ifutwe kwenye kumbukumbu za Bunge.
  • Sasa sakata hilo halitafikishwa kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge.

Dar es Salaam. Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo, ameomba radhi na kukubaliana na ufafanuzi uliotolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, kuhusiana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika mradi wa ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Akizungumza bungeni katika kikao cha kumi cha mkutano wa kumi na tisa, mbele ya Bunge, Gambo ameomba radhi na kuomba kufutwa kauli na tuhuma alizozitoa hapo awali katika kumbukumbu za Bunge la Tanzania 

“Nimefuta na naomba radhi,” amekiri Gambo na wabunge wote wakaunga mkono hoja hiyo kwa kupiga makofi 

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, amesema kuwa baada ya Gambo kufuta kauli yake ya awali ya kuwa Waziri Mchengerwa  alisema uongo, jambo hilo halitafikishwa tena katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

“Baada ya mheshimiwa Gambo kuomba radhi na kufuta maneno hayo kwamba Waziri amesema uongo, kwa kuwa yameondoka rasmi kwenye taarifa zetu za Bunge, anakuwa haendi tena kwenye kamati yetu ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge,” amebainisha Spika Tulia.

Gambo ameomba radhi na kuomba kufutwa kauli na tuhuma alizozitoa hapo awali katika kumbukumbu za Bunge la Tanzania . Picha | Merciful Munuo

Tukio hilo linahitimisha mjadala wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha Halmashauri ya jiji la Arusha  ulioibuliwa na Gambo wakati akichangia bajeti ya Tamisemi.

Katika hoja yake, Gambo alidai kuwa kulikuwa na matumizi mabaya ya fedha katika mkataba wa ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Arusha, akisema kuwa gharama zinazotarajiwa kutumika katika mradi huo ni kubwa na haziakisi ukubwa wa mradi husika.

 “Gharama halisi zilitakiwa kuwa Shilingi bilioni 3.4, lakini wameingia mkataba wa Shilingi bilioni 6.2. Kuna ziada ya zaidi ya bilioni 2.8. Hili ni tatizo la watumishi wa umma wanaoshirikiana kulimaliza Jiji la Arusha.” alisema Gambo hapo awali.

Kutokana na uzito wa tuhuma hizo, Spika Tulia alimtaka Waziri Mchengerwa kuwasilisha maelezo ya kina kuhusu mchakato wa ujenzi huo.

Katika majibu yake yaliyotolewa Aprili 22 na kufafanuliwa zaidi Aprili 23, Waziri Mchengerwa alisema kuwa hakuna fedha za Serikali zilizopotea, na kuongeza kuwa baadhi ya madai yaliyotolewa ni “cheche za kisiasa.”

Hata hivyo, alikiri kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwepo kwa changamoto za kiufundi kwenye mfumo wa ununuzi wa umma (NEST), ambazo zimesababisha mchanganyiko wa vipimo. Waziri alibainisha kuwa mkandarasi tayari alifahamishwa kuhusu hitilafu hiyo na aliwasilisha majibu yake kwa mamlaka husika.

Awali, baada ya Gambo kuonesha kutoridhishwa na majibu hayo, Spika Tulia aliliagiza Bunge kupeleka suala hilo katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili kuchunguza ukweli wa tuhuma hizo.

Hata hivyo, kwa kuwa Gambo ameomba radhi na kufuta kauli zake, Bunge limeamua kulimaliza rasmi jambo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks