Hii ndiyo hifadhi ya Taifa Rumanyika

February 3, 2020 1:46 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

Kuona wanyama kama twiga, tembo, swala na hata ndege wa aina mbalimbali, Rumanyika itakukaribisha vilivyo mwezi Disemba hadi Februari. Picha| Pixabay.


  • Ina ukubwa wa kilometa za mraba 800
  • Milima na mabonde yake, ni kivutio cha nyani na wanyama wengine wengi.
  • Vipepeo, maua pori na ndege ni sehemu tu ya uzuri utakaokuvutia ukiitembelea

Dar es Salaam. Ni miongoni mwa hifadhi za Taifa mpya tano zilizoanzishwa mwaka 2019, ikiwa na vivutio vingi ambavyo ni fursa kwa watalii na kuiingizia Serikali mapato. Ni hifadhi ya Taifa ya Rumanyika. 

Endapo umezowea kuona Twiga na kusikia mtikisiko wa ardhi pale tembo anapotembea, hakika unahitaji kuitembelea hifadhi hii kwa ajili ya kubadilisha taswira yako ya kitalii kwani kati ya hifadhi za nchini, hifadhi ya Taifa ya Rumanyika itakupatia safari ya aina yake.

Siyo kwamba utashuhudia wanyama adimu tu kama ilivyo katika Hifadhi Taifa ya Mto Ugalla lakini Rumanyika inaenda mbali zaidi kwa kukupatia fursa ya kushuhudia sokwe na nyani wanavyoruka kutoka kwenye mti mmoja hadi mwingine.

Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika ambayo ina ukubwa wa kilometa za mraba 800 ni hifadhi inayoipamba ardhi ya mkoa wa Kagera huku uzuri wake ukizidi kuwa wakipekee kwenye ardhi hiyo inayopakana na Ziwa Victoria.

Je, mara yako ya mwisho kuona vipepeo ni lini? Rumanyika itakupatia muda mzuri wa kuwashuhudia viumbe hao wanaofanya maua ya hifadhi hiyo kuzidi kuchanua kwenye kiwango cha joto kinachofikia Sentigredi 41.


Zinazohusiana


Unahisi imeishia hapo, ndege ambao husafiri kutoka maeneo mengine huipamba hifadhi hii kwa rangi huku miruzi wanayoitoa ikikusahaulisha “earphone” zako na muziki unaousikiliza.

Kuyaona hayo (maua pori na vipepeo) itakulazimu uitembelee hifadhi hii mwezi Juni hadi Agosti huku kama wewe unapendelea kuona wanyama kama twiga, tembo, swala na hata ndege wa aina mbalimbali, Rumanyika itakukaribisha vilivyo mwezi Disemba hadi Februari.

Hakika umepata sehemu kwa ajili ya kutalii mwishoni mwa mwaka ambayo inafikika kwa wepesi kwa barabara.

Kwa mujibu wa Tanzania Zalendo, Hifadhi hii inafikika kwa kutumia mabasi yanayotokea Kata ya Kaisho mkoani Kagera ambapo utasafiri umbali wa kilometa18.4 na kama utatokea Kaitambuzi (kagera), utasafiri umbali wa kilometa 27.1 hadi kuifikia hifadhi hiyo.

Enable Notifications OK No thanks