Hatua zitakazokusaidia umalize mchakato wa ‘Airport’ bila usumbufu
- Hakikisha una pasi ya kusafiri na kitambulisho kitakachosaidia kukutambua kwa haraka.
- Fika mapema uwanjani na fuata maelekezo yote utakayoambiwa na maafisa wa usalama.
- Wakati unasubiri ndege unaweza kuburudika kwa maonyesho ya sanaa, muziki, bustani, manunuzi, kusoma vitabu na matembezi mafupi.
Dar es Salaam. Usalama wa abiria na mizigo ni jambo la kwanza na muhimu katika viwanja vya ndege. Abiria wote kabla ya kuingia kwenye ndege hupitia mchakato wa ukaguzi ili kuhakikisha safari inakuwa salama na yenye mafanikio.
Kwa waliowahi kusafiri na ndege hili halina tatizo kwao lakini kwa wanaopanga kusafiri na ndege kwa mara ya kwanza hawana budi kufahamu kubwa ni lazima wapitie hatua mbalimbali za ukaguzi na usalama kuwawezesha kutumia usafiri huo wa anga.
Ufahamu wa mchakato wa ukagauzi wa ‘Airport’ unakuweka katika hali ya kuepuka usumbufu wa kukatiza safari au kuchelewa kwasababu tu hujafuata taratibu ambazo zimewekwa na mamlaka husika kwa watumiaji wa huduma za ndege.
Utapitia hatua mbalimbali za ukaguzi ambazo zimewekwa kwenye vituo vilivyopo ‘Airport. Ni muhimu kukumbuka kuwa ukaguzi hutofautiana toka nchi moja na nyingine lakini kwa sehemu kubwa unalingana kwasababu utatakiwa kuonyesha pasi ya kusafiria, kadi ya kitambulisho cha kazi au uraia, mizigo uliyobeba na mwisho kukaguliwa kama umetimiza vigezo vya kutumia usafiri wa ndege.
Inspekta Mkuu Kitengo cha Usalama wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Burhani Majaliwa anabainisha kuwa mchakato wa kwanza kabisa kwa msafiri ni kufika mapema uwanjani kulingana na maelekezo ya ndege anayosafiria na mabadiliko yanayoweza kutokea kabla ndege haijapaa.
“Abiria anapaswa afike uwanja wa ndege masaa mawili kwa safari za ndani ya nchi na masaa matatu kwa safari za nje ya nchi kabla ya muda wa kuondoka ndege yake akiwa na tiketi halali na kitambulisho au passport hai (ambayo haijakwisha muda wa matumizi),” anasema Majaliwa. .
Ufikapo ‘ Airport’ unapaswa kuwa msikivu na mwangalifu huku ukisikiliza matangazo yanayotolewa kuhusiana na mfumo wa usalama na hatua moja hadi nyingine za kufuata kukuwezesha uingie ndani ya ndege.
Usalama wa msafiri na mizigo yake ni jambo la kwanza na muhimu kwa mtu yeyote anayetumia usafiri wa ndege. Picha| DW.
Shirika la ndege unalosafiria litakagua kitambulisho, pasi ya kusafiria na kupima mizigo uliyobeba ili kuhakikisha kama umetimiza uzito unaotakiwa . Ikiwa uzito umezidi kiwango kile kinachoendana na gharama ya tiketi, utalazimika kulipia. Ukifanikiwa kupita kihunzi hiki cha awali utajulishwa namba ya siti utakayokaa, maelekezo mengine muhimu.
Hatua inayofuata ni kukagua tena pasi ya kusafiria kwa wanaoenda nje ya nchi au kitambulisho chcchote kilichotolewa na Serikali kama leseni ya udereva, cha mpiga kura au kitambulisho cha Taifa. Ukaguzi huu unafanywa na maofisa Uhamiaji na Mamlaka ya ya Viwanja vya Ndege (TAA) ambao wamepewa dhamana ya kulinda usalama wa viwanja vya ndege nchini. Wakati wote weka pamoja tiketi na kitambulisho chako ili kurahisisha utambuzi kwa kila hatua unayopitia, kushindwa kufanya hivyo kunaweza kukwamisha safari yako.
Zinazohusiana:
- Fastjet yafanya mabadiliko makubwa huduma za vyakula, mizigo
- Mkimbizi wa zamani wa Afghan azunguka Dunia kwa ndege
- Mambo unayotakiwa kuyafanya ukifika mapema ‘Airport’
Hutaishia hapo lakini utahitajika kufanyiwa ukaguzi wa mwili na vitu alivyovaa kama vinaendana na taratibu za usalama zilizowekwa kwa kutumia mashine maalum ya kielektroniki ya utambuzi.
Hapa utalazimika uvua vitu vyote vizito mwilini ikiwemo sweta, koti, mkanda na viatu na kuviweka kwenye kikapu ambacho kitapita kwenye mashine ili kubaini vitu vyote vyenye ncha kali. Mizigo yako yote itapitishwa katika mashine ikiwa imefunguliwa ili kubaini kama kuna vitu ambavyo haviruhusiwi.
Pia kama una kompyuta mpakato (laptop) utatakiwa kuitenganisha na vifaa vingine vya elektroniki, sarafu, funguo na simu. Mizigo yako itapita upande wa pili na kama kutakuwa na kitu chochote kisichotakiwa itapekuliwa na utawajibika kuiacha hapo au kutoa maelezo yake.
Hatua ya mwisho ni wewe kupita kwenye mashine maalum kwaajili ya ukaguzi wa mwili wako. Pia ukaguzi huu unaweza kufanyika na Afisa kukagua sehemu mbalimbali za mwili wako. Ikiwa kuna kitu chochote chenye asili ya chuma chochote, kengere itapiga kelele na utalazimika kurudi kuondoa kitu kisichotakiwa mwilini.
Kwa sababu mashine haiwezi kutambua kila kitu kwenye mwili au mizigo yako, maafisa wa usalama wanaweza kukagua mizigo yako yote. Hili hutegemeana na taratibu za nchi husika.
Mashine ya kielektroniki inayotumika kukagua mizigo na abiri wanaotumia usafiri wa ndege. Picha| aol.co.uk
Shirika la Kimataifa la Viwanja vya Ndege la Kimataifa (ICAO) linawashauri wasafiri kuepuka kuvaa viatu vyenye visigino virefu au soli ya chuma.
Vaa viatu vitakavyokuwezesha kutembea kirahisi na soski ili kuepuka vumbi kwenye sakafu. Pia upeka kuvaa au kubeba vitu visivyotakiwa utavyolazimika kuvua wakati wa ukaguzi.
Epuka kuvaa vitu vyenye asili ya chuma kama bangili, mikufu, ondoa vitu vyote mfukoni vinaongeza uzito na kuibua maswali kwa mkaguzi. Unaweza kutakiwa kutoa maelezo ya kifaa chochote cha umeme ulichobeba, hakikisha kina umeme wa kutosha kutoa maelezo yanayojitosheleza.
Baada ya kukamilisha hatua zote za ukaguzi unaingia kwenye eneo salama (Airside) ukisubiri kuingia kwenye ndege. Eneo hilo linatenganisha wasafiri wa ndani na nje ya nchi. Ikiwa utaondoka kwenye eneo la kusubiri ndege utalazimika kurudia tena zoezi la ukaguzi na kama hauna nyaraka zozote unaweza kupata tabu sana.
Kulingana na ukubwa wa eneo la kusubiri ndege, viwanja vingine vya kimataifa vina maduka makubwa, eneo la burudani, sanaa na bustani (Artificial gardens) ambazo unaweza kutembea na kujifunza mambo mengi wakati ukisubiri muda wa kuondoka. Pia unaweza kupata huduma za baa na intaneti, maeneo ya kuchaji simu, hata maktaba za kusoma vitabu.
“Pia anapaswa kusoma matangazo ya kiusalama katika uwanja husika. Hii pia itamsaidia kujua ni vitu vipi vinaruhusiwa na vipi haviruhusiwi au vinavyopaswa kufuata utaratibu maalum,” anashauri Majaliwa kutoka TCAA.
Muda ukifika Maafisa wa shirika la ndege watakagua tena pasi ya kusafiria na kitambulisho chako na kukuruhusu kuelekea ndege ilipo ambapo unaweza kutembea kwa miguu, kupanda gari au ndege ndogo kutegemeana na ukubwa wa kiwanja na idadi ya abiria.
Hata hivyo, bado utakuwa na kazi ya kujifunza na kufuata taratibu zingine muhimu wakati wote ikiwa ndani ya ndege ili kukuhakikishia usalama wako na safari yenye mafanikio.