Hapana: Serikali haijatangaza kazi za ukarani sensa ya watu na makazi

March 28, 2022 11:58 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Imesema wakati ukifika itatangaza.
  • Ni baada ya tovuti feki kutangaza nafasi 100,000 za kazi ya kuhesabu watu.
  • Yawaonya watu kuhusu utapeli huo.

Dar es Salaam. Baada ya kuwepo kwa taarifa zinazozagaa mtandaoni kuhusu ajira mpya takriban 100,000 za kuhesabu watu katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu, Serikali imesema haijatoa tangazo la ajira hizo.

Hivi sasa, kuna tovuti kwa jina la https://www.sensatanzania.com ambayo inatangaza kuwepo kwa nafasi za kazi za makarani wa Sensa na tayari baadhi ya watu wameshajisajili kwenye mfumo huo kwa malipo, jambo ambalo linaweza kuwaingiza katika mtego wa kutapeliwa.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) zimetoa tahadhari kwa wananchi wote kuwa hadi sasa haijatangaza nafasi za kazi za makarani wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

“NBS na OCGS inapenda kuwafahamisha wananchi wote kuwa Serikali rasmi haijaanzisha tovuti ya Sensa, tovuti https://www.sensatanzania.com si rasmi, hivyo haitambuliwi na Serikali,” imesema taarifa ya taasisi hizo mbili iliyotolewa leo Machi 28, 2022.

Nafasi za ukarani na usimamizi wa sensa zitatangazwa rasmi kupitia tovuti na mitandao ya kijamii ya NBS na OCGS, radio, runinga na magazeti mara baada ya taratibu zote za Serikali zitakapokamilika.

Kazi ya kuwapata watumishi hao wa sensa itasimamiwa na Kamati za Sensa za Mkoa ambazo wenyeviti wake ni wakuu wa mikoa husika, imeeleza taarifa hiyo.

“Nia ya Serikali kufanya hivyo ni kuhakikisha watu wote wanaotaka kufanya kazi za ukarani na usimamizi wa sensa watoke katika maeneo yao wanayoishi,” imeeleza NBS na OCGC.

Pia maombi ya kazi hiyo yatafanyika bila malipo, kinyume na maelezo yaliyotolewa na tovuti feki iliyotangaza ajira.

Enable Notifications OK No thanks