Hapa ndipo NIDA wanapokwama: Ripoti ya CAG

April 9, 2020 10:29 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema inakabiliwa na changamoto za mfumo na vitendea kazi 
  • Watu wawili kati ya watu waliopewa namba za utambulisho wa Taifa hawajapata kadi zao
  • NIDA yatakiwa kuharakisha mchakato wa kutoa namba za utambulisho wa Taifa. 

Dar es Salaam. Huenda Watanzania waliopata namba za utambulisho wa Taifa (NIN) wakaendelea kusubiri kwa muda mrefu kupata vitambulisho vya Taifa baada ya ripoti ya CAG kubaini kasi ndogo ya uchapishaji inayochagizwa na changamoto za mfumo na vitendea kazi. 

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere kuhusu Serikali Kuu ya mwaka 2018/2019  imeeleza kuwa katika mapitio ya takwimu ya uzalishaji wa vitambulisho vya Taifa kwa mwezi Februari 2020 ilibainika kuwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) iliandikisha watu milioni 21.6 kati ya kadirio la watu milioni 24.

Hata hivyo, kati ya watu walioandikishwa ni watu milioni 17.1 waliopatiwa Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN), huku idadi iliyobakia ya watu 4.59 milioni sawa na asilimia 21 ikiwa bado haijapata namba hizo. Hii ina maana kuwa takriban mtu mmoja kati ya watano waliojiandikisha kupata namba hizo bado hajazipata achana na kupata kitambulisho cha Taifa. 

“Pia, nilibaini kuwa kati ya watu milioni 17.1 waliopata nambari za Vitambulisho vya Taifa, ni kadi za watu milioni 5.9 ndizo zilizotengenezwa huku idadi iliyobakia ya watu milioni 11.1 wenye Nambari za Vitambulisho (sawa na asilimia 65) wakiwa bado hawajapata Kadi za Vitambulisho,” amesema CAG Kichere katika ripoti hiyo.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa kasi ndogo ya kuchapisha kadi za vitambulisho vya Taifa inatokana na uwezo mdogo wa mfumo wa NIDA ambao unatofautiana kiutendaji na mashine mpya iliyonunuliwa.

Baada ya kubaini uzalishaji mdogo wa vitambulisho, CAG alipitia uwezo wa mfumo wa uzalishaji wa kadi za vitambulisho na kugundua kwamba Nida ilifanya ununuzi wa mashine mpya ya chapa vitambulisho kutoka kwa M/s Atlantic Zeiser GmbH kwa gharama ya Euro 3.3 milioni (Sawa na Sh8.3 bilioni) kupitia mkataba wenye Nambari EA/061/20182019/HQ/G/01-Lot 3 wa 22 Julai 2019.

“Hata hivyo, mashine hiyo ilishindwa kufanya kazi kwa sababu bakaa ya kadi haikuendana na mfumo uliopo kwenye mshine hiyo ya chapa na hivyo, kusababisha ugumu kwenye uzalishaji wa vitambulisho hivyo,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo. 

CAG Kichere amesema ucheleweshaji wa utoaji wa namba za utambulisho wa Taifa kwa raia wanaostahili utazuia upatikanaji wa mawasiliano ya simu za mkononi kwa kuwa usajili wa laini za simu unataka mtumiaji kuwa na nambari ya kitambulisho au kitambulisho cha Taifa.


Soma zaidi:


Kukosekana kwake kumesababisha makampuni ya simu kufuata maelekezo ya kuzifungia laini zote ambazo hazijasajiliwa kuanzia Januari 2020.

Pia NIDA ilianzisha ofisi kwenye wilaya mbalimbali na kuziwezesha kwa mashine mahususi za biometria za uandikishaji wa wapigakura (BVR) ili kusaidia katika shughuli za uandikishaji wa Vitambulisho vya taifa.

Hata hivyo, ukaguzi wa CAG wa taarifa ya vifaa vya teknolojia ya mawasiliano na habari ulibaini kuwa vifaa vilivyotolewa kwa ajili ya kutumika na mashine za BVR vilipotea kwenye Halmashauri mbalimbali za Mikoa ya Iringa, Tabora na Arusha.

Vifaa hivyo 33 vilivyopotea ni pamoja na kompyuta mpakato, kamera, vitunza kumbukumbu (disks) na nyaya za kuingizia umeme (Adaptors na Extension). Upotevu huu unaweza kuwa umechangia kupunguza kasi ya utoaji wa vitambulisho kwa wananchi.

NIDA imeshauriwa  ichukue hatua za haraka kuhakikisha upatikanaji mbadala wa vifaa vyote vilivyopotea ili kurejesha kasi ya uandikishaji.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW