Halmashauri 10 zenye vitabu vichache shule za msingi Tanzania

September 24, 2022 5:53 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Halmashauri hizo ni pamoja na Kondoa, Mlele, Mafia na Newala.
  • Katika baadhi ya shule zake wanafunzi hawana vitabu kabisa.
  • Wataalam washauri wadau wa elimu kuingilia kati kunusuru hali hiyo.

Dar es Salaam. Huenda mustakabali wa elimu ya watoto katika halmashauri za wilaya 10 nchini Tanzania ikiwemo ya Kondoa ukawa mashakani baada ya halmashauri hizo kutajwa kuwa na vitabu vichache zaidi katika shule za msingi. 

Vitabu vinavyozungumziwa hapa ni vile vya kiada vinavyotumika kufundishia masomo ya  Kusoma, Kuandika, Kuhesabu, Sayansi ya Jamii, Michezo, Sanaa, Kingereza, Kiswahili, Maarifa ya Jamii, Sayansi, Uraia na Maadili darasa la I hadi la VII. 

Ripoti ya Takwimu Muhimu  za Elimu (Basic Education Data 2022) inayotolewa na  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Halmashauri ya Mji wa Kondoa iliyopo mkoani Dodoma ndiyo yenye vitabu vichache zaidi nchini katika shule za msingi mwaka huu wa 2022. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa vitabu vya kiada vilivyopo katika halmashauri hiyo ni 28,214 ambavyo vinatumiwa na wanafunzi 16,174 waliopo kwenye shule za msingi 34. 

Licha ya kuwa na vitabu vichache kuliko halmashauri zote nchini, uwiano wa vitabu hivyo kwa wanafunzi ni wa kuridhisha. Kwa wastani kitabu kimoja kinatumiwa na mwanafunzi mmoja katika halmashauri hiyo, ikiwa havitahusisha mgawanyo wa kimasomo na madarasa. 

Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inapendekeza kuwa kitabu kimoja kinasomwe na wanafunzi watatu.Vitabu vilivyopo Kondoa ni pungufu mara 11 zaidi ya vitabu vinavyopatikana katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma yenye vitabu 322,184.

Kusoma kwa makundi kunaweza kusaidia wanafunzi ambao shule zao zina upungufu wa vitabu kujisomea na kuimarisha matokeo yao. Picha | Dar 24.

“Bado havitoshelezi”

Licha ya uwiano wa kuridhisha wa vitabu kwa wanafunzi wa halmashauri hiyo iliyopo Kanda ya Kati Tanzania, yapo masomo ambayo yanakabiliwa na upungufu mkubwa wa vitabu.

Mathalan, Shule Msingi ya Maji ya Shamba iliyopo katika halmashauri hiyo ina vitabu 22 vya somo la Sayansi kwa darasa la V na tisa somo la Hesabu ambavyo vinatumiwa na wanafunzi 214.

Hiyo ina maana kuwa katika somo la Sayansi kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi tisa na somo la Hesabu kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi 23, jambo ambalo linaweza kuibua changamoto katika kupata maarifa na ujuzi.


Zinazohusiana:


Vitabu vinaathiri ufaulu?

Wachambuzi wa masuala ya elimu wanabainisha kuwa kitabu ni chenzo muhimu ya kufanikisha elimu ya mwanafunzi anapokuwa shuleni kwa sababu humsaidia kupata maarifa na ujuzi.

Katika baadhi ya shule za msingi Kondoa, uhaba wa vitabu umekuwa na matokeo hasi kwa ufaulu wa wanafunzi katika halmashauri hiyo.

Mathalani,  Shule ya Ubembeni  iliyopo wilayani humo yenye vitabu nane vya Sayansi kwa darasa la tano ilishika nafasi ya 2,619 kati ya shule 11,909 zilizopo kwenye kundi moja kwenye matokeo ya kitaifa ya darasa la saba mwaka 2021 yaliyotolewa na Baraza la Mitahani la Tanzania (Necta).


Uhaba wa vitabu ni tatizo kubwa 

Kondoa imeungana na halmashauri nyingine tisa katika kundi la halmashauri 10 zilizo mkiani kwa vitabu vichache katika shule za msingi. 

Halmashauri hizo ni pamoja na Mlele iliyopo mkoa wa Katavi yenye jumla ya vitabu 28,881, Mafia (Pwani) yenye vitabu 31,819, na Halmashauri ya Wilaya Pangani ya mkoani Tanga yenye vitabu 34,643.

Nyingine ni Madaba mkoani Ruvuma  yenye vitabu 38,005, Korogwe (Tanga) vitabu  45,131, Newala (Mtwara) vitabu  44,771, na Halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba iliyopo Mkoa wa Mtwara yenye vitabu 54,717.

Orodha hiyo imefungwa na Halmashauri ya Wilaya ya Liwale yenye vitabu 53,330 na Lindi  vitabu  54,275, zote zikiwa mkoani Lindi.

                   

Nini kifanyike?

Ili kunusuru taaluma za wanafunzi wa shule za msingi zenye uchache wa vitabu Dk. Godfrey Kimaro Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anashauri wadau wa elimu kuona namna wanavyoweza kuunga mkono pale zilipoishia juhudi za Serikali kwenye kuongeza idadi ya vitabu.

“Watafutwe wadau wa eilimu mfano watu waliosoma maeneo hayo ya vijijini wawapelekee vitabu kusapoti (kuunga mkono ) juhudi za Serikali zilipoishia” anasema Dk Kimaro

Pia anashauri ili kupunguza adha hiyo ni vyema wanafunzi wasome vitabu kwa makundi kwa kushirikiana na wanafunzi wa shule nyingine ambao wana vitabu vingi.

Tehama italeta unafuu?

Kuongezeka kwa matumizi ya Tehama nchini na ujio wa mtandao wa kasi ya 5G je unaweza kunusuru wanafunzi wenye uhaba wa vitabu na kufeli?.

Julai 29 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alitangaza vishikwambi vilivyotumika katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi vitasambazwa kwa walimu ili kuongeza matumizi ya Tehama kwenye elimu.

Dk. Kimaro ameishauri Serikali kuwapa kipaumbele walimu ambao shule zao zina upungufu wa vitabu  kwenye mpango mkakati wa kugawa  vishikwambi hivyo, ili kuwawezesha kupata nakala ya vitabu hivyo kwa njia ya mtandao.

“Hivyo vishikwambi wanataka kuwapa walimu, wafanye soft copies (nakala laini) zipatikane ili mwalimu hata akiwa kwenye mtandao ana download (anapakua) na kuwapa wanafunzi,” anasema Kimaro.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW