Hakuna siri tena: Ifahamu ndege inayoweka wazi yaliyojificha ndani ya nyumba

January 9, 2023 10:02 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Hutumia mwanya ambao watafiti huita udhaifu katika usalama wa intaneti kupima umbali halisi kati ya ishara na kitu.
  • Watafiti wapendekeza kuboreshwa kwa usalama wa mfumo wa intaneti ya umma i kuhakikisha ulinzi mtandaoni.

Dar es Salaam. Kuzidi kukua kwa teknolojia na matumizi yake kumekuwa na faida duniani hasa kuboresha maisha ya watu lakini pia kunasababisha wasiwasi na tishio la usalama, faragha na umiliki wa data katika siku zijazo. 

Timu ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Waterloo, Ontario nchini Canada,  imeunda kifaa kinachotumia ndege zisizo na rubani (drone) ambacho kinaweza kuona kinachoendelea ndani ya kuta za majengo kwa kutumia mtandao wa intaneti.

Kifaa hiki (Wi-Peep) kinaweza kurushwa karibu na jengo na kisha kutumia mtandao wa WiFi unaotumiwa na wafanyakazi au wakazi kutambua kwa haraka vifaa vyovyote vinavyotumia intaneti ndani ya jengo husika.

Wi-Peep hutumia mwanya ambao watafiti huita udhaifu katika usalama wa intaneti ya umma. Hata kama mtandao umelindwa kwa nenosiri, vifaa tajwa hujibu kiotomatiki majaribio ya mawasiliano kutoka kwa kifaa chochote kilicho ndani ya masafa.

Wi-Peep hutuma jumbe kadhaa wakati kifaa kinaporuka na kisha kupima muda wa kujibu wa kila kifaa janja kilicho karibu na kuiwezesha ndege isiyo na rubani kutambua eneo kifaa kilipo ndani ya jengo.

Dk. Ali Abedi, Profesa Msaidizi wa sayansi ya kompyuta katika Chuo Kikuu cha Waterloo, amesema “vifaa vya Wi-Peep ni kama taa katika wigo unaoonekana, na kuta ni kama kioo, kwa kutumia teknolojia kama hiyo, mtu anaweza kufuatilia mienendo ya walinzi ndani ya benki kwa kufuata eneo la simu zao au saa zao za kisasa.

“Vilevile, mwizi anaweza kutambua mahali na aina ya vifaa janja nyumbani, ikiwa ni pamoja na kamera za usalama, kompyuta ndogo na runinga mahiri, ili kupata mtu anayefaa kwa ajili ya kuvunja. Kwa kuongezea, utendakazi wa kifaa kupitia ndege isiyo na rubani inamaanisha kuwa inaweza kutumika haraka na kwa mbali bila uwezekano mkubwa wa mtumiaji kugunduliwa.” 

Dhumuni la ugunduzi huu ni kuangalia uwezekano wa kuathiriwa kwa watumiaji na usalama wa mitandao ya WiFi. Timu hiyo ya watafiti imeweza kuunda kifaa hiki kwa kutumia ndege ya kawaida isiyo na rubani na vifaa vingine vinavyogharimu Sh47,000 tofauti na gharama kubwa zilizokuwa zikitumika awali.

“Mara tu mwanya wa heshima wa WiFi ulipogunduliwa, tuligundua aina hii ya shambulio linawezekana,” Dk Abedi amesema.

Timu hiyo pia imesema Wi-Peep imeundwa ili kujaribu nadharia yao na ikagundua haraka kuwa mtu yeyote aliye na utaalamu unaofaa angeweza kuunda kifaa sawa na chao kwa urahisi.

“Katika kiwango cha kimsingi, tunahitaji kurekebisha mwanya wa usalama wa WiFi ili vifaa vyetu visijibu wageni…Tunatumai kazi yetu itafahamisha muundo wa itifaki ya kizazi kijacho.”  watafiti wa  Chuo Kikuu cha Waterloo Dk. Abedi na Vasisht.

Utafiti huo huenda ukasaidia kuimarisha ulinzi wa vifaa vya vinavyotumia intaneti ya umma katika maeneo mbalimbali kwa kubuni teknolojia rafiki zitakazoepusha uvamizi na wizi wa data muhimu za watu binafsi na taasisi mbalimbali.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW