Gharama ya ukimya: Ukosefu wa taarifa unavyohatarisha maisha ya wenye uziwi Tanzania

Dar es Salaam. Joel Amiri alishangazwa na mabadiliko ya ghafla ya tabia za watu waliomzunguka mwanzoni mwa mwaka 2020 akiwa nyumbani kwao mkoani Tabora.
Alianza kuona majirani zake na wanafamilia wakiwa wamevaa barakoa na kila alipojaribu kuwasogelea karibu, walimuonesha ishara ya kumtaka akae mbali nao.
Wakati yeye akishangaa mabadiliko hayo ya ghafla, wanajamii nao walimshangaa kwa kutoelewa kilichokuwa kinaendelea. Kipindi hicho ulimwengu ulikuwa ukikabiliwa na mlipuko wa virusi vya corona (UVIKO-19).
“Nilikuwa nyumbani Tabora, wakati wa jioni niliona watu wengi wanatembea wakiwa wamevaa barakoa, na mimi sikuwa nimevaa, wao wakawa wananishangaa mimi, na mimi nawashangaa wao, nikiwasogelea karibu wanarudi nyuma, nikawa sielewi, mpaka dereva boda naye alikuwa amevaa barakoa, nikiwauliza wanaongea kwa mdomo na mimi siwaelewi,” anasema Joel mwenye umri wa miaka 43.
Kwa Joel na maelfu ya wengine wenye ulemavu wa kusikia nchini Tanzania, mlipuko wa UVIKO-19 haukutangazwa kwao kwa lugha wanayoielewa.
Wakati redio, televisheni na mitandao ya kijamii ikisambaza taarifa kila kona, jamii hii iliendelea na maisha bila kuelewa hatari iliyokuwa inakaribia.
Taarifa zinachelewa kuwafikia
Tamko la Shirika la Afya Duniani (WHO) la mwaka 2022 lililozitaka nchi washirika kuandaa miongozo ya kujikinga na Uviko 19 yenye lugha jumuishi lilibainisha kuwa watu wenye ulemavu hasa wa kusikia walikosa taarifa za msingi kuhusu namna ya kujikinga, kupata matibabu au hatua za tahadhari zilizotangazwa na Serikali.
Wengine walitegemea ndugu au jamaa kuwatafsiria, jambo lililowaweka kwenye hatari ya kupokea taarifa zisizo sahihi au kwa kuchelewa.
Kwa Joel, elimu ya Uviko-19, anasema alianza kuipata baada ya tangazo lililotengenezwa kwa lugha anayoielewa miezi minne baadaye.
Tangazo hilo lilitengenezwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Sign Language Translation Development au (BILAT) inayojihusisha na utafsiri wa maandishi mbalimbali kwa lugha ya alama.

Kwa Joel na maelfu ya wengine wenye ulemavu wa kusikia nchini Tanzania, mlipuko wa UVIKO-19 haukutangazwa kwao kwa lugha wanayoielewa. Picha. Goodluck Gustaph | Nukta Africa
Joel si mtu mwenye ulemavu pekee ambaye hutaabika kupata elimu kuhusu afya kutokana na taarifa mbalimbali kutolewa bila kujali mahitaji yao.
Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa Tanzania ina watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali milioni 12.1 wakiwemo zaidi ya watu 539,186 wenye ulemavu wa kusikia kama wa Joel.
Watu wenye ulemavu wa kusikia ni kundi linalohitaji taarifa za afya kupitia lugha ya alama mfumo unaokosekana katika maeneo mengi ya nchi, jambo linalowaweka hatarini kiafya hususan kipindi cha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, M pox, pamoja na Uviko 19.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta TV katika matangazo yaliyochapishwa kwenye kurasa rasmi ya Wizara ya afya inayotoa elimu ya afya kwa umma umebaini kuna upungufu wa taarifa Jumuishi, hususan kwa watu wenye ulemavu wa kusikia.

Hali ni mbaya zaidi kwa wenye ulemavu zaidi ya mmoja
Hali ni mbaya zaidi kwa watu wenye zaidi ya aina moja ya ulemavu kama Sophia Mbaga mwenye ulemavu wa kusikia na kuona, jambo linalomfanya ategemee wakalimani wanaoelewa lugha maalumu.
Kwa Sofia mkazi wa Moshi, ili afahamu jambo, mtafsiri wake ni lazime afanye mawasiliano kwa kumshika mikono.
Mlezi wa Sophia, Mwalimu Onesta Mollel ameiambia Nukta TV kwamba pamoja na watu wenye ulemavu kukosa taarifa kwa wakati, pia hupata changamoto zaidi kuwasiliana na watu wengine hususan anapohitaji msaada wa kiafya.
“Unaweza ukafika hospitalini, mtu mwenye uziwi akaelezea jinsi anavyoumwa, dokta akatibu tofauti, kiziwi anaweza akasema anaumwa tumbo lakini daktari akabaki anajiuliza tumbo kuumwa linasababishwa na nini na asipate majibu, mwisho wake anampa dawa ya isiyotibu anachoumwa mgonjwa,” ameeleza Mollel.
Ukosefu wa taarifa za afya kwa watu wenye ulemavu wa kusikia si tu kunaweka rehani maisha yao kwa kuwa afya zao zinakuwa hatarini bali kunawakosesha pia haki yao ya kikatiba ya kupewa taarifa na kutoa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote.
Upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi ikiwemo masuala ya kijamii, uchumi, na kisiasa.
Haki inayopotea
Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyoridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD), ambao unazitaka nchi wanachama kuhakikisha kuwa taarifa muhimu, hasa kuhusu afya, zinapatikana kwa njia zinazofikiwa na watu wote bila ubaguzi.
Hata hivyo, wadau wa haki za binadamu wanadokeza kuwa utekelezaji wa mkataba huo kwa watu wenye ulemavu wa kusikia bado ni changamoto kubwa hapa nchini kama anavyoeleza wakili wa kujitegemea William Maduhu.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu wa mwaka 2006 ambao Tanzania ni nchi mwanachama wa mkataba huo na imeutungia sheria namba tisa ya mwaka 2010 ya watu wenye ulemavu pamoja na ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania vyote vinatoa haki ya mtu kupata taarifa kutoka kwa mamlaka zake.

“Kwa ujumla hapa nchini kwetu bado kuna changamoto, wengi wenye ulemavu wanakosa matibabu, hasa wenye ulemavu wa kusikia , matangazo mengi na programu nyingi hazina option (kipengele) cha mtafsiri wa lugha ya alama kuwafanya wajue nini kinazungumzwa kwa wakati huo,” ameeleza Maduhu.
Tatizo kubwa kwenye vituo vya afya
Ukosefu wa taarifa jumuishi ni sehemu tu ya changamoto kubwa zaidi.
Hata pale ambapo watu wenye ulemavu wa kusikia wanapofika kwenye vituo vya afya, vikwazo vya mawasiliano kati yao na wahudumu wa afya vinaendelea kudhoofisha haki yao ya kupata huduma bora.
Kukosekana kwa wakalimani wa lugha ya alama, maandishi ya kueleweka, au mifumo mbadala ya kuwasiliana, kumeacha wengi wao wakihudumiwa kwa kubahatisha au kupuuzwa kabisa.
Matokeo yake ni huduma zisizoeleweka, vipimo visivyofanyika kwa usahihi, na wakati mwingine, maamuzi ya kiafya yasiyozingatia mahitaji halisi ya mgonjwa kama anavyosimulia Joel ambaye amewahi kupewa dawa za tumbo ilihali alikuwa anaumwa Malaria.
“Nilimueleza daktari kuwa ninaumwa kichwa na kuharisha, dokta akanitibu kuharisha akasahau kuhusu kichwa, alinipa dawa za tumbo za kuzuia kuhara, nilitumia zile dawa lakini shida iliendelea, baadaye nilikutana na rafiki yangu ambaye ni kiziwi, akanishauri nikapime malaria, na nilipopima nikabainika kuwa na malaria,” anasimulia Joel kwa huzuni.
Daktari Bahati Fungo kutoka Kituo cha Afya Buguruni Angilikana ameiambia Nukta TV kuwa mgonjwa kupata matibabu yasiyo sahihi inatokana na wataalamu wa afya kutokuwa na uelewa wa lugha ya alama hivyo kutoa tiba kutokana na namna alivyoelewa taarifa.

“Inapotokea daktari anahitaji usaidizi kumuelewa mgonjwa na mgonjwa anahitaji mtu mwingine kumueleza daktari kunakuwa na changamoto kwa sababu katika tasnia ya matibabu sio vitu vyote vitahusisha watu watatu.
Nitakapokwambia taarifa wewe mkalimani ukamueleza mgonjwa inategemeana wewe umeelewa nini, na mgonjwa atakapokueleza tatizo lake hautawasilisha vile yeye ametaka, tunawahudumia hawa watu (wenye ulemavu wa kusikia) lakini kuna hiyo changamoto ya mawasiliano,” amesema Dk Fungo.
Hata hivyo, Dk Fungo ambaye amehudumu katika taaluma hiyo kwa zaidi ya miaka 23, anasema pamoja na kuwa mawasiliano kwa njia ya wakalimani yanaweza yasiwe sahihi kwa asilimia 100 bado wana umuhimu.
Kauli hiyo inapigiliwa msumari na Dk Editha Cosmo wa hospitali hiyo anayesema kuwa ni vyema ukawekwa utaratibu kwa kila kituo cha afya nchini kuwa na mkalimali wa lugha ya alama.
Daktari huyo anatoa wito kwa watoa huduma za afya kujifunza lugha hiyo ili kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
“Ni muhimu kuwepo madaktari wanaoweza kutafsiri kwa lugha ya alama hiyo inakuwa bora zaidi kuliko kumtumia mkalimani, kwa sababu utamtibu kwa vile ulivyoelewa sio alichokueleza mkalimani, amesema Dk Cosmo.
Ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa usawa kwa kila Mtanzania, Wakili Maduhu ambaye pia ni Afisa Programu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) anashauri Serikali kutunga Sheria ya adhabu kwa taasisi au watendaji wa afya watakaoshindwa kutoa huduma jumuishi.
Maduhu anasema hatua hiyo itakuwa kichocheo cha mabadiliko ya kweli katika kuwahudumia watu wenye ulemavu kwa usawa na heshima inayostahili.
“Ni sheria kufanyiwa mabadiliko na kuongezwa makali na iainishe adhabu kwa wanaotoa hizo huduma zisizo jumuishi kwamba asiyefanya anachukuliwa hatua gani,” ameeleza Wakili Maduhu

Hali ni mbaya zaidi kwa watu wenye zaidi ya aina moja ya ulemavu kama Sophia Mbaga mwenye ulemavu wa kusikia na kuona, jambo linalomfanya ategemee wakalimani wanaoelewa lugha maalumu. Picha. Goodluck Gustaph l Nukta Africa
Serikali yakiri uwepo wa tatizo, yaahidi kutafuta ufumbuzi
Serikali inakiri kuwa bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa taarifa jumuishi kwa watu wenye ulemavu wa kusikia, hali inayowaweka hatarini kukosa huduma muhimu za afya, hasa wakati wa majanga.
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Dk. Ona Machangu anaeleza miongoni mwa vikwazo katika utoaji taarifa jumuishi za afya ni uwepo wa gharama kubwa katika uzalishaji wa maudhui mahsusi kwa kundi hilo.
Licha ya changamoto hizo, Dk Machangu anasema Serikali inaendelea kutengeneza vielelezo vya mawasiliano vinavyolenga kuwafikia watu wenye ulemavu wa kusikia, ingawa kwa sasa vinafanyika kwa uchache kutokana na uhaba wa rasilimali.
“Bado tunachangamoto kutokana na gharama za kutengeneza materials (vielelezo) ambazo zinalenga haya makundi kidogo ziko juu lakini hiyo haituzuii sisi kuendelea kuhakikisha kwamba hilo kundi linapata taarifa sahihi hususan wakati wa magonjwa ya mlipuko, tunalifanya jambo hilo kwa uchache ila ni jambo endelevu,” amesema Dk Ona
Ili kutatua uhaba wa wakalimani katika vituo vya afya, Dk. Machangu anasema Serikali imeweka kipaumbele hitaji la kuwa na wataalamu wa afya wenye uelewa wa lugha ya alama.
Hii anaeleza kuwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa usawa na kwa kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Latest



